loader
Wamachinga wafunguka kwa Samia

Wamachinga wafunguka kwa Samia

SHIRIKISHO la Umoja wa Machinga Tanzania limemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi cha Sh bilioni tano kwa ajili ya kuwatengenezea mazingira mazuri ya biashara kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, wameomba kukutana na kuzungumza na Rais Samia ili wamueleze changamoto zinazowakabili na mbinu zitakazoweza kutumika kuboresha kazi zao.

Kauli ya wafanyabiashara hayo imetolewa kwa niaba yao na Makamu Mwenyekiti wa shirikisho hilo Taifa, Stephen Lusinde wakati wa mkutano na vyombo vya habari Dar es Salaam jana.

“Kwetu tunajiona kama tupo katika mikono salama ya mama, kitendo cha kutoa shilingi bilioni tano kwa ajili ya kutatua kero zetu mbalimbali, kinamfanya kuwa Rais wa kwanza kuonyesha kuwajali machinga, huko nyuma fedha kama hizo zilikuwa zikitumika katika Operesheni ya kuwaondoa maeneo mbalimbali,” alisema Lusinde.

Alisema licha ya ushirikiano mzuri wanaoupata sasa kutoka serikali hasa kupitia utaratibu wa kuwapanga machinga katika maeneo sahihi, bado kuna haja ya kuangalia namna ya ushirikiano utakavyoweza kuwa na matokeo bora zaidi ili kufanikisha utatuzi wa baadhi ya changamoto wanazosema kama zikifanyiwa kazi zitasaidia kuondoa lawama.

Lusinde alisema wamekuwa wakifanya vikao vya pamoja na serikali kuratibu mazingira mazuri ya ufanyaji kazi katika mikoa yote nchini ukiwemo wa Dar es Salaam ambako kunatajwa kuwa na idadi kubwa ya wafanyabiashara wanaokadiriwa kufikia 13,000.

“Tuchukue nafasi hii kuwashukuru serikali kwa ushirikiano inaoendelea kutupatia wakati ikiendelea kujipanga kututafutia maeneo mengine ya kufanya kazi, kwetu tumekuwa tukilitekelexza jukumu la kutoa elimu kwa wafanyabiashara wenzetu kuzingatia kile tunachoaswa,” alisema kiongozi huyo wa wamachinga.

Alisema asilimia 85 ya wamachinga wote wa Dar es Salaam hususani wale waliokuwa katika mazingira yasiyo rasmi, wametekeleza agizo la kuondoka katika maeneo yasiyo rasmi.

Aliiomba serikali iwashirikishe na kuwapa ulinzi wanapoenda kuwaondoa wachache wanaopinga anaoamini kuwa si wenzao.

Lusinde alisema anaamini Serikali ya Awamu ya Sita ni sikivu hivyo kama kuna changamoto zinazoweza kufanyiwa kazi, hakuna ugumu wowote kuzitatua na kwamba suala la kuwapanga wamachinga lisifanywe la kisiasa.

Alisema wanaamini wakipata fursa ya kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan, waatampa kuhakikisha wamachinga wanapungua katika mijini kwa kuibua fursa ambazo zitaweza kuwawezesha kufanya biashara katika mikoa yao.

Alisema kinachotokea kwa sasa kisitafsiriwe kama kuna ugomvi kati ya wamachinga na serikali isipokuwa kinafanyika kwa nia njema inayolenga kutengeneza fursa nzuri ya kila mfanyabiashara kuendesha maisha yake huku akisisitiza uwepo wa Rais Samia kwao ni faraja hasa kwa namna anavyowajali wafanyabiashara.

Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Dar es Salaam, Namoto Yusuph alisema walipanga kukutana na waandishi wa habari mapema kabla ya kuanza kwa mchakato wa uhamishaji ila waliona vyema wasubiri hadi kazi hiyo ianze ili kuondoa mtazamo wa kuwa walipanga kuleta fujo.

Namoto alisema vurugu za juzi zilisababishwa na baadhi ya watu ambao si wafanyabiashara na alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kuwadhibiti watu hao.

Septemba 13, mwaka huu, Rais Samia aliwaagiza wakuu wa mikoa nchini kuwapanga upya wafanyabiashara ndogo maarufu kama wamachinga, bila kutumia nguvu ili wafanye biashara kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

Aidha, katika matumizi ya fedha kiasi cha Sh trilioni 1.3 zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19, Rais Samia ametoa Sh bilioni tano kwa ajili ya wajasiriamali wadogo.

Kwa mujibu wa Waziri wa Tamisemi, Ummy Mwalimu, fedha hizo zimepangwa kutumika katika mpango wa kuboresha mazingira ya kufanyia shughuli za wajasiriamali ambako uchambuzi umeonesha kuwa maeneo yenye wafanyabiashara wadogowadogo ni majiji ya Arusha, Dar es Salaam, Mbeya, Dodoma, Tanga, Mwanza na Manispaa za Ubungo, Kinondoni, Temeke na Morogoro.

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi