loader
Kigogo Vodocom aeleza alivyochunguza simu ya Sabaya

Kigogo Vodocom aeleza alivyochunguza simu ya Sabaya

MENEJA Ulinzi na Ushirika wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wa Kampuni ya Vodacom (T) Makao Makuu Dar es Salaam, James Wawenje (39), ameieleza mahakama jijini hapa kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa Arusha ilimuagiza achunguze namba za simu ya kiganjani za washitakiwa watatu akiwemo alyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya.

Wawenje ni shahidi wa sita katika kesi ya uhujumu uchumi, kuongoza genge la uhalifu na kutakatisha fedha inayomkabili Sabaya (34) na wenzake sita katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha.

Washitakiwa wengine ni Enock Mnkeni (41), Watson Mwahomange (27) maarufu Malingumu, John Aweyo (45), Sylvester Nyengu (26) maarufu Kicheche ambaye ni msaidizi wa Sabaya, Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31).

Akiongozwa na Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa Serikali, Ofmen Mtenga mbele ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Patricia Kisinda, Wawenje alidai namba za simu alizokabidhiwa ni za Sabaya, Mnkeni na Macha ambazo Takukuru ilitaka taarifa zake za Julai 20, mwaka huu za kupiga, kupigiwa simu na jumbe mfupi.

Wawenje alizitaja namba hizo alizokabidhiwa na Takukuru kuwa ni namba 0758 707171 iliyosajiliwa kwa jina la Lengai Ole Sabaya, 0757 978686 iliyosajiliwa kwa jina la Enock Mnkeni na namba 0746 935569 iliyosajiliwa kwa jina la Ramweli Jackson Macha.

Alisoma nyaraka za mtandao za Vodacom zikionesha watuhumiwa Sabaya, Mnkeni na Chacha walivyokuwa katika Jiji la Arusha maeneo ya Mbauda, Sombeni, FFU Kwa Mrombo na Makao Mapya kati ya saa 8.44 mchana, saa 9.52 na saa 9.55 alasiri.

Wawenje alidai alitoa taarifa zake kwa Kamanda wa Takukuru Mkoa Arusha kama alivyotakiwa ikiwa ni pamoja na taarifa za kupiga, kupokea na ujumbe mfupi wa sms kwa tarehe iliyotajwa kwa mujibu wa sheria ya nchi.

Alidai kuwa yeye ndiye mwenye mamlaka ya kutoa taarifa za mteja kwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini pindi vitakavyohitajika.

Alisema tangu Agosti 25, 2014 amekuwa akifanya hivyo kwa ushirikiano mkubwa kwa kuzingatia sheria ya nchi na kwa kuzingatia misingi ya sheria ya usalama kwa kuwa ndio mtunza kumbukumbu zote za Vodacom (T) za kupiga, kupokea na ujumbe mfupi wa sms kutoka kwa wateja wote wa mtandao huo.

Alidai kumbukumbu za kupiga, kupokea na jumbe za sms za wateja wa Vodacom hukaa zaidi ya miaka 10 kwa mujibu wa sheria.

Alikabidhi mahakamani nyaraka ya barua kutoka Takukuru kwenda Vodacom kama ushahidi katika kesi hiyo na upande wa utetezi haukuwa na pingamizi kuhusu nyaraka hiyo.

Nyaraka zingine ambazo zilipaswa kuwasilishwa mahakamani hapo kama kielelezo cha ushahidi wa Jamhuri ni taarifa ya mteja ya kupiga, kupokea na ujumbe mfupi wa sms za Sabaya, Mnkeni na Macha.

Wakili wa utetezi wa washitakiwa wa tano, sita na saba, Edmund Ngemela alipinga na kudai kuwa sheria inapingana kupokelewa vielelezo hivyo.

Mahakama ilikataa pingamizi hilo hivyo vilipokelewa kama ushahidi.

foto
Mwandishi: John Mhala, Arusha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi