loader
JK: Jamii ielimishwe masuala ya mirathi kuepuka migogoro

JK: Jamii ielimishwe masuala ya mirathi kuepuka migogoro

RAIS Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amezitaka taasisi zinazojihusisha na masuala ya kisheria na utoaji haki nchini kuielimisha jamii kuhusu suala la mirathi ili kupunguza migogoro inayojitokeza katika jamii.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu cha utoaji wa elimu ya mirathi kwa mujibu wa dini ya Kiislamu kilichoandikwa na Mjumbe wa Baraza la Ulamaa la Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata) Shehe Issa Othman, Kikwete pia aliwataka waumini wa dini hiyo kukisoma kitabu hicho ili kupata maarifa kuhusu mirathi.

Alisema kama ilivyo kwa migogoro mingine ikiwemo ya ardhi, migogoro inayohusu mirathi imekuwa na malalamiko mengi katika maeneo mbalimbali na kusababisha kuwepo kwa mashauri mengi mahakamani, jambo linalopaswa kushughulikiwa kikamilifu.

“Suala la mirathi ni jambo linalostahili kuwekwa sawa kutokana na umuhimu wake, ni vizuri taasisi zetu za kisheria na wadau wote wa masuala ya utoaji haki kutumia nafasi zao katika kuielimisha jamii,” alisema Kikwete.

Alisema anaamini kuz-induliwa kwa kitabu hicho kutasaidia kuondoa changamoto nyingi zilizopo katika utolewaji wa mirathi na kuwatendea haki makundi ya wanawake, wazee na watoto ambao ndiyo waathirika wakubwa wa mirathi hiyo.

Alimpongeza mwandishi kwa kuandika kitabu kinachotoa muongozo kuhusiana na mirathi hasa baada ya kuchambua mambo magumu na kuyaweka katika maandiko rahisi kiasi cha kufanya kila mtu kukielewa.

Kwa upande wake Mufti wa Tanzania, Shehe Abubakar Zuberi alimpongeza Shehe Issa Othman kwa kutekeleza mpango wake wa kuandika kitabu hicho kama ambavyo viongozi wa Bakwata walikubaliana katika jambo hilo na mengine.

Alisema vitabu vingi vya mirathi vimeandikwa lakini kilichoandikwa na Shehe Issa kina ubora, na kikiwa katika lugha nyepesi.

Kwa upande wake, Shehe Issa Othman, alisema kitabu kimejielekeza katika kile ambacho mwanadamu anapaswa kukiacha baada ya kufa na nani anapaswa kugawiwa kile kilichoachwa.

Alisema kitabu hicho kitamwezesha muislamu kufuata muongozo wa ugawaji wa mali zake baada ya yeye kufa kikidadavua nani anapaswa kupata nini na nani hapaswi.

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi