loader
Wanaobambikia makosa walimu wasipande madaraja wakemewa

Wanaobambikia makosa walimu wasipande madaraja wakemewa

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais-Tamisemi, David Silinde amewataka kaimu makatibu wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kutowabambikia makosa walimu ili tu wasipandishwe madaraja kwa kuonekana si watendaji bora.

Akifungua kikao kazi cha siku mbili cha kaimu makatibu hao wasaidizi kutoka wilaya 139, Silinde alisema hataki kusikia walimu wanabambikiwa makosa na makatibu hao na endapo atabaini hilo hatua kali za kisheria dhidi yao zitachukuliwa.

“Sitaki kusikia suala la kubambikiziana makosa walimu kwani hiyo inachangia kumkosesha mwalimu nafasi ya kupandishwa daraja,” alisema Silinde.

Silinde pia alipiga marufuku makatibu wasaidizi hao kuomba rushwa kwa walimu ili wapendekezwe kupandishwa madaraja.

Alisema hakuna sababu ya kuweka bifu na walimu na kuwabambikizia makosa na kusababisha uadui baina yao.

Alisema Ofisi ya Rais Tamisemi ikibaini kwamba kuna baadhi ya kaimu makatibu wasaidizi wanafanya vitendo hivyo hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.

Aliipongeza pia TSC kwa utaratibu wa kuwapandisha walimu madaraja lakini akaomba kufanya hivyo bila kutumia rushwa bali wapandishe walimu wenye sifa.

Alisema rushwa ni adui wa haki na haipaswi kuingizwa kazini hivyo ni vema wakawapa nafasi walimu wenye sifa kupandishwa vyeo na kuwatia moyo wafanye kazi kwa bidii bila makandokando.

Akizungumzia Sh trilioni 1.3 zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Ofisi ya Rais Tamisemi imepata Sh bilioni 536 na kati ya hizo Sh bilioni 304 zilitengwa kwa ajili

ya kutekeleza miradi ya kujenga miundombinu ya elimu hivyo akataka ziende zikatumike ipasavyo na akatoa mwito kwa walimu kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya elimu hapa nchini.

Silinde alizitaka halmashauri kuhakikisha zinawapatia walimu ofisi zenye hadhi na si kuwaacha wakifanya kazi katika mazingira ambayo hayastahili.

Alisema ofisi yake itaangalia suala la bajeti ili kuhakikisha wanafanya kazi katika mazingira yenye weledi ambayo yatamfanya mwalimu kufanya kazi yake kwa weledi mkubwa.

Kwa upande wake, Katibu wa TSC, Paulina Nkwama alisema Tume hiyo itahakikisha fedha zilizotolewa zinatumika ipasavyo katika miradi ambayo inatekelezwa hapa nchini.

Aliihakikishia Tamisemi kwamba kila kitu kilichopangwa kitakwenda ipasavyo ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati.

Mwenyekiti wa TSC, Profesa Willy Komba alisema vitendo vya uonevu havitakuwa na nafasi katika tume hiyo hivyo watahakikisha kila mmoja anafanya kazi yake bila ya kuonewa na mtu.

Alisema Tume hiyo inasimamia haki hivyo suala la rushwa halitapewa nafasi kwenye utendaji wao wa kila siku.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/30dc84735c69971114a85c3a3b7f6021.png

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi