loader
Rekodi Simba yavunjwa

Rekodi Simba yavunjwa

TANZANIA imepoteza nafasi ya uwakilishi wa timu nne kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao, baada ya Simba kushindwa kuingia hatua ya makundi kwa kufungwa mabao 3-1 na Jwaneng Galaxy ya Botswana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam jana.

Galaxy imevunja rekodi ya Simba iliyoiweka tangu mwaka 2013 kwa kutofungwa uwanja wa Mkapa, ambapo mpaka jana ilicheza mechi 13 za kimataifa na kushinda 10, sare tatu.

Simba ingeshinda jana, ingefuzu hatua ya makundi na hivyo kulinda pointi za uwakilishi wa timu nne msimu ujao kama ilivyokuwa msimu huu.

Simba ni miongoni mwa timu 10 zilizoanza raundi ya kwanza ya michuano hiyo baada ya kufanya vizuri msimu uliopita.

Imeaga michuano hiyo kwa sare ya mabao 3-3 lakini wapinzani wao wamesonga mbele kwa vile wameshinda mabao mengi nyumbani. Simba ilishinda 2-0 ugenini.

Matokeo hayo yanaipeleka Simba kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, ambapo sasa itahitaji kushinda mechi moja nyumbani na ugenini ifuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Mabao ya Galaxy yalifungwa na mshambuliaji Rudath Wendel mawili na la tatu likifungwa na Gape Mohutsiwa.

Bao pekee la Simba kwenye mchezo huo lilifungwa katika dakika ya 40 kupitia kwa kiungo wake, Larry Bwalya ambaye aliitumia vema pasi ya Benard Morrison.

Mchezo huo uliokuwa na presha zaidi kwa wageni, Simba ilikuwa ya kwanza kulifikia lango la Galaxy baada ya kiungo Bwalya kupiga shuti kali lililookolewa na kipa Ezekiel Morawke na kuwa kona ambayo haikuzaa bao.

Simba walirudi kwa kasi katika lango la Galaxy dakika ya 26 lakini mashuti yaliyopigwa na Shomari Kapombe na Morrison yaliokolewa na kipa Morake.

Dakika ya 27 waliendelea kuliandama lango la Galaxy lakini safari hii shuti la Bwalya lilienda nje ya lango na katika dakika hiyo mwamuzi Abongile Tom alimuonesha kadi ya njano Mphoyamodimo Keiponye kwa kumfanyia madhambi Kapombe.

Kiungo Sadio Kanoute nusura aipatie Simba bao la uongozi katika dakika ya 34 lakini uimara wa Morake uliendelea kuwa kikwazo kwa Wekundu wa Msimbazi.

Dakika ya 46 Simba ilifanya mabadiliko ya kwanza kwa kumtoa Hassan Dilunga na nafasi yake kuchukuliwa na Peter Banda ili kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji nao  Jwaneng waliwatoa Thabang Sesinyi na Themba Dladla na nafasi zao kuchukuliwa na Rudath Wendell na Tshephang Boithatelo.

Jwaneng walisawazisha bao lao katika dakika ya 47 kupitia kwa ingizo jipya Wendell ambaye alitumia vema makosa ya safu ya ulinzi ya Simba.

Dakika ya 58 Mohamed Hussein alionywa kwa kadi ya njano na mwamuzi Tom kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa kumfanyia madhambi Resaobaka Thatanyane.

Dakika ya 59 Jwaneng Galaxy walipata bao la pili kupitia kwa Wendell baada ya safu ya ulinzi ya Simba kushindwa kuondoa mpira wa hatari langoni kwake.

Simba ilifanya mabadiliko mengine dakika ya 74 kwa kuwatoa  Morrison na Thadeo Lwanga na nafasi zao kuchukuliwa na Duncan Nyoni na Erasto Nyoni kuimarisha eneo la ulinzi na kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji.

Dakika ya 85 Simba ilifanya mabadiliko mengine kwa kumtoa John Bocco na nafasi yake kuchukuliwa na Meddie Kagere, wenyeji walifanya mabadiliko mengine katika dakika 92 kwa kumtoa Sadio Kanoute na nafasi yake kuchukuliwa na Israel Patrick.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/a1d17a680ce37ab0a7af974fb1b9d7f8.jpg

TAASISI ya Mama Ongea ...

foto
Mwandishi: Martin Mazugwa

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi