loader
Kocha Simba alia na bahati

Kocha Simba alia na bahati

KOCHA msaidizi wa Simba, Selemani Matola amesema kukosa bahati ndio kumesababisha timu hiyo kushindwa kupata ushindi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam juzi.

Simba licha ya kuutawala mchezo na kutengeneza nafasi nyingi za mabao, washambuliaji wake walionesha kujawa na papara na kushindwa kuzitumia ipasavyo nafasi hizo kwenye vipindi vyote viwili.

Akizungumza na gazeti hili mara baada ya mchezo huo kumalizika, Matola alisema anaamini haikuwa bahati yao kwani wachezaji wao walipambana kwa dakika zote 90 na kutengeneza nafasi zaidi ya 10, lakini walishindwa kuweka mpira wavuni.

“Naweza kusema hatukuwa na bahati leo (juzi), sababu tulicheza vizuri, hasa kipindi cha pili ambacho tulitengeneza nafasi nyingi, lakini Denis Kibu na John Bocco walishindwa kuzitumia vizuri… Lakini hivyo ni vitu vya kawaida kwenye mchezo, tunarudi kujipanga kwa ajili ya mechi zijazo,” alisema Matola.

Kocha huyo alisema mbali na kukosa bahati, lakini wapinzani wao Coastal Union nao walicheza vizuri na kuziba vyema nafasi ambazo walipanga kuzitumia kupata mabao, hivyo anawapongeza kwa kutimiza majukumu yao ipasavyo.

Kwa upande wake kocha wa Coastal Union, Melis Medo, aliwapongeza wachezaji wake kwa kazi kubwa waliyoifanya na kuweza kuondoka na pointi moja mbele ya mabingwa watetezi Simba ambao walikuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani tena mbele ya kundi kubwa la mashabiki wao.

Kocha huyo Mmarekani alisema haikuwa kazi rahisi kwao kupata suluhu hiyo kwani asilimia kubwa ya wachezaji wanaounda kikosi cha Coastal ni wapya na wengi wao wanatokea kwenye michuano ya mtaani ‘ndondo’, hivyo kwa kazi waliyoifanya ya kuwadhibiti Simba wanastahili pongezi.

Tangu Ligi Kuu kuanza, hii ni mara ya pili kwa Simba kutoka suluhu baada ya ile dhidi ya Biashara ya Musoma, Mara na kujikusanyia pointi nane katika michezo minne.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/5c117c664f7b32f41daad5f0ed6b50e0.jpeg

TAASISI ya Mama Ongea ...

foto
Mwandishi: Mohamed Akida

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi