loader
Agizo la kudhibiti mbolea lifanyiwe kazi

Agizo la kudhibiti mbolea lifanyiwe kazi

JUZI wakati akiahirisha Mkutano wa Tano wa Bunge la 12 jijini Dodoma, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema nchi inakabiliwa na upungufu mkubwa wa mbolea.

Kutokana na Covid-19, alisema baadhi ya nchi zimeacha kusafirisha mbolea kutokana na gharama kubwa za usafirishaji na kupungua kwa malighafi kutokana na sababu hizo hizo za usafiri. 

Kwamba kuadimika kwa mbolea kumesababisha bei kupanda kwa takribani asilimia 96 ikilinganishwa na bei ya mwaka jana. Hii yote inatokana na viwanda vya ndani kutozalisha mbolea ya kutosha.

Kama inavyojulikana, mbolea ya kupandia na ya kukuzia ni muhimu katika kuwezesha wakulima kupata mavuno yenye tija, hususani katika maeneo mengi ya nchi ambayo kama hakuna mbolea mkulima anaambulia kuvuna mabua!

Ni kutokana na hali hiyo, serikali imewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya, hususani waliopo katika maeneo ya mpakani, kuhakikisha mbolea inayotoka nje ya nchi kuingia nchini haizuiwi.

Lakini pia wameagizwa kuzuia mbolea yoyote inayosafirishwa kutoka ndani ya nchi kwenda nje.

Majaliwa alisema serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuzalisha, kuagiza na kusambaza pembejeo kwa wakulima kulingana na mahitaji na ikolojia ya kilimo.

Waziri Mkuu alisema serikali pia inawasiliana moja kwa moja na wazalishaji wa mbolea katika nchi rafiki ili kupata mbolea kwa gharama nafuu.

Alisema hatua nyingine inayochukuliwa ni kuruhusu wafanyabiashara kuingiza mbolea nchini bila kutumia zabuni za mfumo wa ununuzi wa pamoja na kuuza kwa bei ya ushindani.

Alisema hatua hiyo tayari imesaidia kuongeza kiwango cha mbolea kilichoingizwa nchini kati ya Julai na Oktoba, mwaka huu. 

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, serikali pia imechukua jukumu la kuhamasisha matumizi ya mbolea mbadala ya kupandia (DAP) na ya kukuzia (Urea) kama vile NPK, NPS, NPSZinc, Nafaka+ ya Minjingu, mbolea za asili, chokaa na mbolea ya Fomi Imbura inayozalishwa na Kiwanda cha Fomi cha Burundi.

Hatua nyingine inayochukuliwa na serikali, ni kuendelea kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya ndani vya kuzalisha mbolea kama suluhisho la muda mrefu.

Kwa vile tatizo la uhaba wa mbolea litakuwa pia linakumba nchi nyingine, tunaamini kwamba viongozi, kila mmoja katika eneo lake, atakuwa mlinzi katika kuhakikisha mbolea haitoki Tanzania kwenda nje.

Tunasema hivyo kwa sababu kunaweza kukawa na soko zuri nje na wafanyabiashara wasio waaminifu wakataka kuchepusha mbolea kwenda huko. Hii itakuwa sawa na kuchukua mboga ya watoto na kuwapa majirani na wao kushinda njaa.

Kucheza na kilimo ni kucheza na maisha kwani kilimo kinaajiri asilimia 65 ya Watanzania, kinahakikishia wananchi chakula, kinaingiza fedha za ndani na za kigeni na pia kinatoa malighafi kwa viwanda.

Kila mmoja wetu aunge mkono na kufanyia kazi maagizo ya serikali hadi pale hali itakapobadilika.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/59521d38591fc7c46c73d0abd320fa97.jpeg

KATIKA ukurasa wake wa habari za kimataifa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi