loader
Bil 150/- kutumika bima ya afya kwa wote

Bil 150/- kutumika bima ya afya kwa wote

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameruhusu Sh bilioni 149.7 zitumike kwa ajili ya Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote katika Mwaka wa Fedha 2022/2023.

Majaliwa amesema serikali ina lengo la kuongeza wigo wa matumizi ya bima ya afya kupitia mpango huo.

Taarifa ya ofisi ya Waziri Mkuu ilieleza kuwa Majaliwa alitoa kauli hiyo juzi usiku Dar es Salaam alipomwakilisha Rais Samia katika maadhimisho ya Siku ya Diwali inayoashiria kuanza kwa mwaka mpya wa Kihindu 2078.

“Hatua za awali kuhusu mpango huo zimekamilika na katika Bajeti ya Serikali Mwaka wa Fedha 2022/2023, Mheshimiwa Rais Samia ameruhusu kutenga jumla ya shilingi bilioni 149.7 kwa ajili ya mpango huo,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Aliipongeza Jumuiya ya Kihindu nchini kutokana na mchango inaotoa kwenye jamii hususan katika utoaji wa huduma za kijamii zikiwemo za afya, elimu, maji, michezo na huduma za kiroho. 

Taarifa hiyo kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa Majaliwa alisema sambamba na suala hilo la kiroho, pia serikali inatambua mchango unaotolewa na Shree Hindu Mandal kwa upande wa huduma za afya.

“Jambo lililonivutia zaidi kwenye eneo hilo ni kitendo cha hospitali zenu kupokea wagonjwa ambao asilimia 95 wanatumia bima ya afya ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),” alieleza Majaliwa.

Majaliwa aliihakikishia Jumuiya ya Kihindu Tanzania kuwa serikali inaendelea kuheshimu uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na itaendelea kushirikiana nao na taasisi nyingine za kidini kwa ajili ya ustawi wa taifa na watu wake. 

“Serikali inapongeza na kuthamini mchango wenu katika kujenga jamii yenye kutii mamlaka na sheria za nchi. Nitoe rai kwenu kutumia vema fursa ya uwepo wa kamati za amani kujadili pamoja na kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa na amani na utulivu,” alisema. 

Alisema huduma ya kiroho imekuwa na mchango katika kuimarisha amani, umoja na mshikamano nchini.

“Nitumie fursa hii kuipongeza tena Taasisi ya Shree Sanatan Dharma Sabha kwa kuwekeza nguvu kubwa kwenye mafunzo ya kiroho hususan kwa jamii ya Wahindu nchini.”

Aliongeza, “Elimu mnayoitoa inawafikia vizuri waumini na wanaizingatia. Nataka niwakumbushe tena viongozi wote wa dini neno lenu ni muhimu sana, viongozi wa dini mnaaminiwa sana na ndiyo kwa sababu serikali inaendelea kuwaahidi kuwapa ushirikiano katika kusimamia mwenendo shughuli zenu na haitaingilia ila itashirikiana nanyi.”

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/71634189a8225913ac442ec61d77826e.jpg

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi