loader
RAIS SAMIA ATOA MIL 150/- KWA TIMU YA TAIFA YA WALEMAVU

RAIS SAMIA ATOA MIL 150/- KWA TIMU YA TAIFA YA WALEMAVU

RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa Sh milioni 150 kwa timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kwa wenye ulemavu ‘Tembo Warriors’, inayoendelea na maandalizi ya kufuzu Kombe la Dunia kupitia michuano ya Afrika (Canaf) itakayofanyika jijini Dar es Salaam, kuanzia kesho ambapo Tanzania ni mwenyeji. 

Akizungumza jana jioni alipotembelea kambi ya wachezaji wa timu hiyo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu aliwaeleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anafahamu kama wanajiandaa kuipigania nchi, na hivyo ametoa Sh milioni 150 ili kuwawezesha kufanya vizuri zaidi.

“Mheshimiwa Rais anafahamu mko hapa mnajiandaa kuipigania nchi, na amesema nije hapa kwa niaba yake, na ametoa kiasi cha Sh milioni 150 ili kuwawezesha mfanye vizuri zaidi. Simamieni vizuri fedha hizi na mhakikishe zinatumika kama ilivyokusudiwa.

“Viongozi na Watanzania kwa ujumla tuna imani kubwa na timu yetu, tunaamini mtafanya vizuri na sisi tutakuja hapa kuwaunga mkono,” alisema Waziri Mkuu. 

Kwa upande wake mlezi wa timu hiyo,  Riziki Lulida, ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya maandalizi, alisema kwa kuwa Tanzania ni mwenyeji wa mashindano hayo, ambayo yatajumuisha timu kutoka nchi 15 za ukanda wa Afrika, ni vema timu hiyo ikaungwa mkono ili kufanya vizuri na kuwa miongoni mwa timu nne zitakazofuzu katika michuano ya dunia.

Riziki alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha hizo na kuahidi kuwa watazitumia vizuri, ili kuhakikisha timu hiyo inashinda na kuleta heshima kwa Watanzania na hatimaye iweze kufuzu kushiriki michuano ya kimataifa. 

Aidha, nahodha Tembo Warriors, Steven Manumbu, alimshukuru Rais Samia kwa niaba ya timu nzima, na kuahidi kuwa watajitahidi kuhakikisha wanafanya vizuri katika mashindano hayo, ili waweze kushiriki katika mashindano ya dunia ya michezo ya walemavu.

Waziri Mkuu aliambatana na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, Waziri wa Nchi-Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Kazi, Ajira, Vijana  na Walemavu, Jenister Mhagama, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Hassan Abbasi, Katibu Mkuu-Ofisi ya Waziri Mkuu, Tixon Nzunda, na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/1dc31dbc6b5a1009de4ba9a3f2d5a5ae.jpeg

SIMBA Queens imekuwa timu ya ...

foto
Mwandishi: Isdory Kitunda

1 Comments

  • avatar
    Juma Jumanne
    29/11/2021

    Tembo tena !!!!

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi