loader
Wanafunzi watakiwa kuelimisha jamii umuhimu wa sensa

Wanafunzi watakiwa kuelimisha jamii umuhimu wa sensa

KAMISAA wa Sensa Tanzania Bara, Anne Makinda amewataka wanafunzi wa Sekondari ya Wasichana ya Kondoa mkoani Dodoma wawe wajumbe katika jamii wa kuwahimiza na kueleza umuhimu wa kushiriki katika sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwakani.

Akizungumza kabla ya Maadhimisho ya Siku ya Takwimu barani Afrika inayofanyika leo kitaifa wilayani Kondoa mkoani Dodoma, Makinda aliwataka wanafunzi hao wawahimize wazazi wao kushiriki sensa.

“Mnatakiwa kuwa wajumbe kuhusu umuhimu wa sensa kwa wananchi, wazazi, ndugu, jamaa na marafiki ili washiriki kusajiliwa katika sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwakani,” alisema. Makinda alisema sensa ya mwakani itakayofanyika kisayansi zaidi kwa kutumia vishikwambi badala ya karatasi, itafanyika baada ya miaka 10 tangu iliyopita mwaka 2012.

Alisema wanafunzi hao watakapokuwa likizo wanatakiwa kuwa mabalozi kutoa elimu kwa jamii kushiriki katika sensa ili kupata takwimu zitakazosaidia serikali kupanga mipango yake. Alisema sensa ni nyenzo muhimu katika taifa lolote katika kupata takwimu sahihi na bora kwa ajili ya serikali kupanga mipango kutokana na idadi ya watu na mahitaji.

Makinda ambaye ni Spika Mstaafu pamoja na kutembelea sekondari hiyo na kuwatia hamasa wanafunzi hao wa kidato cha tano na sita kusoma na kuelimisha kuhusu umuhimu wa sensa, pia aliwaeleza umuhimu wa Siku ya Takwimu Barani Afrika ambayo inafanyika kwa mara ya kwanza wilayani humo.

Alipongeza NBS kwa kufanya maonesho hayo kabla ya siku hiyo kwa kutoa elimu kuhusu umuhimu wa takwimu kabla ya siku inayofanyika wilayani humo. Mkuu wa Sekondari ya Juu ya Wasichana ya Kondoa, iliyopo wilayani Kondoa mkoani Dodoma, Flora Nussu alisema shule hiyo ya kidato cha tano na sita ina michepuo sita.

Ina wanafunzi 304 wa kidato cha tano, 368 wa kidato cha sita, walimu 29 na watumishi 14. Akizungumzia Siku ya Takwimu Barani Afrika, Ofisa wa NBS, Said Ameir alisema nchi za Afrika tangu mwaka 1990 zilikubaliana kuwa na siku ya takwimu Afrika. Kila nchi iliachiwa uhuru kuchagua siku yake na Tanzania ikachagua Novemba 28, kila mwaka kufanya siku hiyo.

Akizungumzia kwanini NBS iliamua kufanya maonesho hayo kabla ya Siku ya Takwimu Afrika, Ofisa Masoko wa NBS, Andrew Ponzila alisema wameamua kufanya hivyo ili wananchi wa wilaya hiyo wajue umuhimu wa takwimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Kaimu Ofisa Usajili wa Nida Wilaya ya Kondoa, Simon Kilala alisema wameamua kushiriki katika maonesho hayo kuwapa fursa wananchi wa eneo hilo kufika hapo na kujiandikisha kupata vitambulisho vya Nida.

Maadhimisho ya Siku ya Takwimu yanafanyika Kitaifa leo wilayani Kondoa na yatafunguliwa rasmi na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Ashatu Kijaji ambaye ni Mbunge wa Kondoa Vijijini.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/16fb2923d6b9489f6394d396251be7d2.jpeg

NAIBU Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde, ...

foto
Mwandishi: Na Magnus Mahenge, Kondoa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi