loader
Kafulila ataka ushirika umsaidie mkulima

Kafulila ataka ushirika umsaidie mkulima

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila amekitaka Chama Kikuu cha Ushirika Simiyu (SIMCU) kuona namna bora ya kuboresha ushirika huo uweze kumsaidia na kumkomboa mkulima kiuchumi.

Kafulila alisema hayo jana wakati wa kongamano la ushirika la kujadili na kushauriana namna ya kuimarisha ushirika huo lililofanyika mjini Bariadi. Alisema kuna baadhi ya watu ndani na nje ya ushirika wamekuwa wakiuharibu na kufanya ushirika uwe na makandokando mengi ya kisera, kibinadamu na kiuchumi hali inayosababisha mkulima kutonufaika na kilimo chake.

“Niombe ushirika utafute na uone namna sahihi au kwa kiasi gani majukumu yao yataakisi na kutoa msaada katika maisha ya mkulima...ushirika usiwe kero kwa wakulima bali uendeshwe na kusimamia mafanikio ya mkulima,” alisema. Aliongeza kuwa ushirika uliundwa kwa lengo la kumkomboa mkulima kiuchumi hususani katika kutafuta na kuboresha masoko ili wakulima waweze kuuza mazao yake kwa tija inayostahili bila kunyonywa.

Dk Richard Msuya kutoka Chuo cha Ushirika Moshi alisema vyama vingi vya ushirika vimeshindwa kujiongoza na kusimama imara kutokana na kutokufuata misingi na maadili yake waliyojiwekea. Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba, Marco Mtunga alisema adui wa ushirika ni wana ushirika wenyewe kwani ndani yake kuna wachache ambao wako kimaslahi yao wenyewe na kushindwa kusimamia sheria zao.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika, Mwadui ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emanuel Cherehani alisema Chama Kikuu cha Ushirika Simiyu (SIMCU) kinatakiwa kujizatiti na kuhakikisha wanafufua viwanda vyote vilivyokufa ili kuupa ushirika na mkulima manufaa.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/7898ed8617a253ef74ada7f0a7f18e94.jpeg

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso ...

foto
Mwandishi: Na Happy Mollel, Bariadi

Post your comments