loader
Wakulima walalamikia tozo nyingi kwenye pamba

Wakulima walalamikia tozo nyingi kwenye pamba

WAKULIMA wa zao la pamba wilayani Igunga, mkoani Tabora wameomba serikali iwasaidie kuondoa tozo za kodi wanazokatwa wakati wa maandalizi ya masoko ya zao hilo ili wanufaike zaidi.

Wakulima kupitia Chama cha Msingi Igunga Balimi walitoa ombi hilo wakati wakizungumza na mwandishi wa gazeti hili. Olingo Sombe ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho, aliishukuru serikali kwa kuwarahisishia upatikanaji wa pembejeo kwa wakati lakini alilalamikia wingi wa tozo wakati wa mauzo ya zao hilo.

Alisema katika msimu uliopita wa 2020/2021, walifanya vizuri kwa kuvuna kilogramu 200,000 za pamba, choroko kilogramu 700,000 na waliuza kwa bei nzuri iliyowaongezea mapato. “Tozo zilichangia kupunguza mapato yao,” alisema. Alitaja tozo hizo kuwa ni gharama ya kupakia ambapo kila gunia wanakatwa Sh 300 kwa kila mkulima, kushindilia ujazo wa gunia wanakatwa Sh 300 na kusindikiza gari kupeleka mzigo kwa kampuni wanakatwa Sh 50,000 ili kumlipa mhusika.

“Haya makato yanatuumiza, tumeshafikisha kilio chetu kwa viongozi mbalimbali akiwemo ofisa ushirika, mkuu wa wilaya na juzi tumemweleza Balozi wa Pamba nchini, Aggrey Mwanri ili waangalie namna ya kutusaidia,” alisema. Adelina Braz ambaye pia ni mkulima wa pamba na choroko wilayani humo alisema tozo hizo ni kilio cha muda mrefu ambacho hakijatatuliwa. Aliomba gharama ya kupakia na kusindikiza mzigo ilipwe na kampuni husika kama ilivyokuwa zamani na wao walipe gharama ya kushindilia pekee kuwapunguzia mzigo wa makato.

Pia alishauri kila kampuni ibebe mzigo wake wanaponunua kuepusha gharama za usindikizaji. Akitolea ufafanuzi malalamiko hayo, Kaimu Meneja Mkuu wa Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Pamba mkoani hapa (Igembensabo), Juma Mrisho alisema tozo hizo ni makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha pamoja baina ya wakulima na wadau wa pamba kutegemeana na bei ya soko.

Aliongeza kuwa gharama za tozo hizo zipo kwenye mkokotoo wa bei kulingana na soko la dunia hivyo haziwezi kuondolewa mara moja hadi vikao vya pamoja vikae na kuafikiana.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/1f580b789d8f8f5402318ef03e8884fe.jpeg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Na Lucas Raphael, Igunga

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi