loader
Majadiliano yaanza kupeleka gesi Uganda

Majadiliano yaanza kupeleka gesi Uganda

WAZIRI wa Nishati, January Makamba ameseme wataalamu wa Tanzania na wale wa Uganda wanaanza rasmi Jumapili Novemba 28, majadiliano ya kuanza ujenzi wa bomba la gesi kutoka Dar es Salaam hadi Kampala, Uganda ikiwa ni sehemu ya kuimarisha diplomasia ya uchumi katika nchi hizo.

Lengo jingine ni kuhakikisha rasilimali zilizopo katika ardhi zinanufaisha na kuwezesha uchumi wa ukanda wa Afrika Mashariki kukuwa kwa pamoja.

Makamba amesema katika Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uganda lililofanyika katika viwanja vya Ikulu Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni kuwa Wizara yake imepokea maelekezo ya kuhakikisha majadiliano ya utekelezaji Mradi mkubwa wa kuchakata gesi (LNG) yanafanyika na kukamilika.

“Kazi hiyo tumeianza na mazungumzo yanaendelea vizuri na imani yetu ni kwamba mara baada ya kukamilika mradi huu ramani ya Afrika Mashariki kwenye sekta ya nishati itabadilika,” alisema na kuongeza kuwa ramani itakayo kuwa ikionekana huko mbeleni sio mipaka ya nchi bali mistari ya barabara, mabomba ya nishati na umeme.

Nchi zetu zinachora ramani mpya kwenye uso wa dunia, aliongeza, Waziri Makamba. Haijafahamika ikiwa mpango huo pia utahusisha mpango wa awali wa Serikali ya Tanzania kupeleka nishati hiyo nchini Kenya. Marais wa Tanzania na Kenya walitangaza mwezi Mei kuwa nchi hizo mbili zimeingia makubaliano ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka jiji la Dar es Salaam mpaka Mombasa.

Katika hotuba zao kwa waandishi wa habari baada ya kufanya kikao cha faragha katika Ikulu ya Nairobi, Rais Kenyatta pamoja na mgeni wake Rais Samia wa Tanzania walisema kuwa bomba hilo litakuwa muhimu katika maendeleo ya nchi zote mbili.

Tanzania imegundua gesi katika mikoa yake ya pwani ya kusini ya Lindi na Mtwara na tayari gesi hiyo imefikishwa katika jiji la Dar es Salaam ambapo imeunganishwa na viwanda kadhaa lakini pia inatumika kuzalisha umeme unaoingia moja kwa moja katika gridi ya taifa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/ebc533996dc2f4710c81abe40c899ce3.jpeg

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments