loader
Serikali Z’bar kununua   mwani, bei kuongezeka

Serikali Z’bar kununua  mwani, bei kuongezeka

SERIKALI ya Zanzibar imesema itaanza kununua mwani kutoka kwa wakulima huku bei ikiongezeka kutoka Sh 600 hadi Sh 2,000.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alibainisha kuwa Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC) litaanza kununua mwani kutoka kwa wakulima, hatua ambayo itaongeza ari kwa wakulima.

Dk Mwinyi alisema hayo katika mahojiano maalumu na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) Ikulu mjini Zanzibar.

Alisema uamuzi huo umechukuliwa ili kuongeza ari kwa wakulima wa zao hilo ambao kwa asilimia 80 linalimwa na wanawake waliopo vijijini, maeneo ya mwambao wa Pwani ya Kisiwa cha Unguja na Pemba.

Aliongeza kuwa kuongezeka kwa bei ya mwani mara nne ni hatua moja kubwa ambayo itawawezesha wakulima wa zao hilo kupiga hatua ya maendeleo kupitia zao hilo na kujikomboa kiuchumi na kwamba sasa kilio cha wakulima hao kimepata ufumbuzi wa kudumu.

“Serikali ya Awamu ya Nane imekisikia kilio cha muda mrefu cha wakulima wa mwani, sasa Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC) limeanza kununua zao hilo moja kwa moja kutoka kwa wakulima, hatua ambayo tunaamini itaongeza ari kwa wakulima hao na kupiga hatua kubwa ya maendeleo,” alisema. 

Kwa kutambua mchango mkubwa wa wakulima wa mwani, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga jumla ya Sh bilioni 36 zinazotokana na ahueni ya ugonjwa wa Covid-19 kwa ajili ya kutumika moja kwa moja kwa uchumi wa buluu na kujikita katika kilimo cha mazao ya baharini.

Akitoa mfano alisema katika matumizi ya fedha hizo wakulima wa mwani wapatao 6,000 watanufaika na fedha hizo ambazo zitatumika katika kuwapatia wakulima hao vihori vitakavyotumika kuvuna na kuimarisha mashamba ya mwani yaliyopo katika maeneo yenye kina kirefu cha maji.

Aidha, alisema fedha hizo pia zitatumika kuwasaidia wakulima na wafugaji wa mazao ya baharini yakiwemo majongoo ya Pwani pamoja na kaa, pweza na ngisi ambao ni tegemeo kwa watalii katika kupata vyakula vya baharini.

“Katika fedha za ahueni za kupambana na Covid-19 serikali imewalenga wakulima wa zao la mwani, tutaangalia namna wanavyoweza kupatiwa mbegu ikiwemo kamba tai tai pamoja na vihori vinavyotumika katika kuimarisha mashamba ya mwani katika kina kikubwa cha maji,” alisema.

Aidha, alisema tayari mipango inaendelea kwa kuwashirikisha wawekezaji binafsi pamoja na Shirika la Taifa la Biashara kujenga kiwanda kitakachosarifu na kuongeza thamani ya zao la mwani.

Dk Mwinyi alisema kiwanda hicho kitakachojengwa Chamanangwe Mkoa wa Kaskazini Pemba, kinatarajiwa kugharimu jumla ya Sh bilioni tano ambacho kitasaidia kuongeza thamani ya zao la mwani.

Mapema Dk Mwinyi alisema serikali ya Zanzibar haina mpango wa kubinafsisha zao la karafuu ambalo ni tegemeo la uchumi na kuingiza mapato ya nchi.

Dk Mwinyi alisema ni bahati nzuri bei ya zao la karafuu imeendelea kuwa imara bila ya kutetereka katika soko la dunia na hivyo serikali imeendelea kununua kutoka kwa wakulima karafuu kilo moja Sh 14,000.

Alitaja juhudi zinazochukuliwa sasa kuwa ni pamoja na kuwapatia wananchi wenye sifa na uwezo wa kuyahudumia mashamba ya karafuu huku serikali ikiimarisha vitalu vya miche ya karafuu na kuvigawa kwa wakulima bure.

“Serikali ya Zanzibar haina mpango wa kuachana na zao la karafuu kwa hiyo tutaendelea kununua karafuu kutoka kwa wakulima na kujenga mazingira mazuri ikiwemo kuwapatia wakulima miche na kuimarisha mashamba baada ya kuwapatia wakulima wenye uwezo wa kuyahudumia,” alisema.

Mapema Dk Mwinyi aliwataka wakulima kujikita zaidi katika kilimo cha mazao ya viungo ambacho bei yake ipo ya uhakika katika soko la ndani na nje kufuatia kuimarika kwa sekta ya utalii.

Alisema serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo inatekeleza miradi mbalimbali ya kilimo cha mazao ya viungo kwa kulima kwa kutumia mbinu za kisasa chini ya uangalizi wa wataalamu ikiwemo mabibi shamba na mabwana shamba.

Kwa mfano alitaja mazao ya viungo kama pilipili manga na vanilla kwamba hivi sasa bei yake katika soko la dunia ipo juu ambayo inaweza kubadilisha maendeleo ya wakulima hao na kuwakomboa kiuchumi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/2e2b0e6bae6a839298887116d96b4d12.jpeg

NAIBU Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde, ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Zanzibar

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi