loader
Serikali yawagusa Watanzania ujenzi wa madarasa

Serikali yawagusa Watanzania ujenzi wa madarasa

SERIKALI chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kulipatia ufumbuzi suala la uhaba wa madarasa kwa shule za msingi na sekondari ili shule zitakapofunguliwa Januari 2022 wanafunzi wasikose elimu.

Kutokana na hilo, hivi karibuni ilikopa Sh trilioni 1.3 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Ujenzi wa madarasa, utengenezaji wa madawati na kumalizia ujenzi wa vyuo vya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) 32 ni sehemu ya matumizi ya fedha hizo.

Sh trilioni 1.3 serikali ilizokopa IMF hazitatekeleza miradi ya shule tu, zitatumika katika miradi mingine ikiwemo ununuzi wa magari 25 yakuchimba visima vya maji, mitambo mitano ya kujenga mabwawa ya maji, kujenga vyumba vya wagonjwa mahututi 72, magari ya kubeba wagonjwa 295 na ya chanjo 214, mifumo ya upumuaji kwa hospitali 82 na mitungi ya gesi 4,640.

Kwa upande wa ujenzi wa madarasa na madawati, baada ya kuanzishwa elimu bila malipo mwaka 2016 kumekuwa na ongezeko kubwa la udahili kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na uhaba wa madawati nao ukiwa sehemu mojawapo ya changamoto hizo.

Kutokana na hali hiyo serikali ilikuwa ikishirikiana na wazazi kuchangia ujenzi wa madarasa na utengenezaji wa madawati kila mwanzoni mwa muhula wa kwanza jambo lililokuwa ni mzigo kwa wananchi lakini sasa serikali imeamua kutafuta mbadala wa kutatua tatizo hilo kwa wakati.

Hadi ifikapo mwishoni mwa mwezi huu (Desemba) serikali itakuwa imejenga madarasa ya shule za sekondari 15,000 nchi nzima na madarasa ya shule za msingi 3,000, madawati 462,795. Hatua hii inapaswa kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo.

Maagizo ya utekelezaji wa ujenzi wa madarasa yalitolewa na Waziri katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu na kuwataka wakuu wa mikoa wote kutotoka kwenye mikoa yao kukamilisha miradi hiyo hususani ya madarasa ili wanafunzi watakapofungua shule wasipate shida.

Aidha, Waziri Ummy anasema kwa yeyote atakayetoka nje ya mkoa wake sharti apate kibali cha rais na awe ameandika barua ya kuomba kufanya hivyo kupitia Katibu Mkuu Tamisemi.

Kwa kufanya hivyo tatizo la uhaba wa madarasa litakuwa historia nchini. Kwa sasa inakadiriwa kwamba kuna upungufu wa madarasa 11,000 nchi nzima na Rais Samia ameamua kuondoa mfumo wa zimamoto ambapo kila mwanzoni mwa mwaka wazazi wanalipishwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa aidha ya sekondari au ya msingi.

Wadau wa elimu nchini wakiwemo walimu, wazazi na wanafunzi wameipongeza serikali kwa uamuzi wake huo.

Mwalimu Angela Mahimbo wa Shule ya Msingi Mbagala Kizuiani anasema uamuzi huo uliofanywa na Rais Samia ni wa busara na wa kuungwa mkono kwani amekopa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

“Kila serikali duniani inakopa, hakuna serikali iliyojitosheleza, kama tunakopa kwa ajili ya maendeleo ni jambo jema sioni shida, na kwa ujenzi wa madarasa hayo kutatufanya walimu tumalize mitaala kwa wakati maana wanafunzi wanakuwa pamoja lakini unapokuwa na darasa lenye mgawanyiko suala la kumaliza mitaala kwa wakati ni shida,” anasema Mahimbo.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibasila kwa nyakati tofauti wanasema uhaba wa madarasa ni kero kwao kwani hupunguza morali ya kusoma kutokana na msongamano darasani kitu ambacho hupunguza umakini.

“Uhaba wa madarasa huchangia matokeo mabovu tunapohitimu masomo yetu, kwani wataalamu wanasema muda mzuri na tulivu wa kupokea maarifa ni asubuhi hadi saa sita mchana, unapovuka muda huo ubongo unakuwa na uwezo mdogo wa kupokea maarifa na kutunza kumbukumbu,” anasema Suleiman Mtafya mwanafunzi wa Kibasila.

Justa Kimario ni mwanafunzi wa darasa la sita, Shule ya Msingi Mkoani iliyopo pembezoni mwa Barabara ya Kawawa katika Halmashauri ya Jiji la Ilala, anasema kuongezwa kwa madarasa kwa baadhi ya shule kutapunguza msongamano katika shule yao kwani wanafunzi wengi wanaosoma shuleni hapo na shule ya jirani ya Ilala Boma hawaishi Ilala bali hutoka mbali kutokana na ongezeko la wanafunzi huko wanakoishi.

Justa anasema darasani wanakaa wanafunzi 60 kwa 65 (utaratibu unatakiwa ni uwiano wa watoto 45 kwa mwalimu) hivyo inawawia vigumu wakati wa kuandika kwani hufikia hatua ya kusukumana na kudondoka.

Abdallah Kitwana mkazi wa Mwandege, wilayani Mkuranga anasema uamuzi wa Rais Samia kukopa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na utatuzi wa kero za kudumu huwapunguzia wananchi mzigo hivyo aendelee kukaza buti asisikie maneno ya watu.

“Kimsingi mama anafanya vizuri na kwa kufanya hili kesha kata ‘ngebe’ za mahasimu wa serikali wanaozusha kuwa Januari 2022 wanafunzi watatozwa ada, kama angewatoza ada kwanini akope na kuwajengea madarasa si angeacha na badala yake angetulipisha ili madarasa yajengwe,” anasema Kitwana.

Ujenzi wa madarasa hayo sanjari na utengenezaji wa madarasa umekwishaanza katika mikoa mbalimbali hususani katika shule ambazo zina uhitaji wa kuongezewa vyumba vya madarasa ili kufikia malengo ya serikali kupitia maagizo ya Waziri Ummy ili Januari asiwepo mtoto atakayeshindwa kuingia shule kwa tatizo la madarasa au madawati.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/c46b94974bb4db4632f3289a5a47d1c0.jpg

Chama cha wanafunzi wa Kike wa Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: DUNSTAN MHILU

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi