loader
Uamuzi mdogo kesi ya kina Sabaya Desemba 6

Uamuzi mdogo kesi ya kina Sabaya Desemba 6

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha inatarajiwa kutoa uamuzi mdogo Desemba 6, mwaka huu kama mfanyabiashara Francis Mroso (44) akamatwe kutokana na ombi la wakili wa utetezi alililowasilisha mahakamani hapo akidai shahidi huyo alitoa rushwa ya Sh milioni 90.

Mroso ni shahidi wa 10 wa Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita.

Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Patricia Kisinda, Desemba 2, mwaka huu alitoa muda kwa mawakili wa mashitaka kujibu hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi mahakamani hapo. Desemba Mosi, Wakili wa Utetezi, Fridolin Bwemelo aliwasilisha ombi la kukamatwa kwa shahidi huyo akidai alitoa rushwa ya Sh milioni 90 na yupo uraiani na aliowapatia rushwa ni washtakiwa kwenye kesi hiyo ya uhujumu uchumi.

Alidai, Sheria ya Kupambana na Rushwa kifungu cha 15 (1) (b) kimeeleza wazi hatua za kuchukuliwa kwa mtu atakayetoa na kupokea rushwa na hakuna kifungu kinachoeleza kutoa rushwa ya kulazimishwa. Alidai kwa mujibu wa kifungu hicho cha sheria, hakuna sehemu imezungumzia suala la kutoa rushwa kwa kulazimishwa bali mtoaji na mpokeaji wa rushwa watakuwa wametenda kosa.

Aidha, wakili huyo aliomba kupata tafsiri ya mahakama kwa kuwa kesi hiyo ilifunguliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na ilitakiwa kuendeshwa na mawakili wake, badala ya mawakili wa serikali kama ilivyofanyika. “Hakimu tunajiuliza, ni kwa nini mtu aliyetoa rushwa na kukiri mbele ya mahakama hii bado yupo huru, lakini waliopokea rushwa wameshtakiwa na wapo ndani, maombi yetu ili kuondoa utata kwenye jamii inayotuzunguka tunaomba shahidi huyu akamatwe.”

“Jamii yetu yenye sera ya kazi iendee na kuepuka upendeleo kwa kuwa kupitia hayo ili jamii ielewe kwamba haki inatendeka kwa watu wote, hivyo tunaiomba mahakama kupitia sheria ya makosa ya jinai inaweza kutoa amri ya kumkamata mtu yeyote aliyekiri makosa mbele yake kwa kutenda kosa hilo,” alidai.

Wakili huyo alidai kwamba, mahakama imejiridhisha kupitia kwa shahidi huyo ambaye yupo chini ya kiapo na kukiri kwamba alitoa rushwa ya Sh milioni 90. Awali, mawakili wa serikali, Filex Kwetukia na Tersila Gervas walidai kuwa, wametuhumiwa kwamba hawakutakiwa kusikiliza kesi hiyo, hivyo watawasiliana na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) ili kutoa ufafanuzi kwa nini walipewa ridhaa ya kusimamia kesi hiyo badala ya Takukuru.

Akijibu hoja za mawakili wa utetezi, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tersila Gervasi alidai kwamba, Katiba ya nchi, ibara ya 59 (b), imempa mamlaka DPP kuendesha mashauri yote ya jinai. Alidai sheria imeeleza kuwa, DPP anaweza kutoa mamlaka kwa wasaidizi wake, wakiwamo mawakili wandamizi wa serikali kuendesha mashauri hayo kwa niaba yake.

Wakili Tersila alidai sheria ya huduma ya mashtaka, kifungu cha nne, imetoa mamlaka kwa mahakama zote kuendesha mashtaka kwa niaba ya DPP. Kuhusu hoja wa kesi kusimamiwa na mawakili wa serikali badala ya Takukuru, alidai kwa mujibu wa sheria ya huduma ya mashtaka, DPP anafanya uamuzi na kuteua wahusika wa kuendesha kesi na wao walipewa ridhaa ya kusimamia shauri hilo.

“Katika nchi yetu, mamlaka za uchunguzi zipo chini ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), lakini baada ya serikali kuona kuna umuhimu polisi kuchunguza na baadae walihamishia kwenye taasisi nyingine ikiwamo Takukuru kufanya uchunguzi kwa kuwa taasisi hii inatambulika kisheria na ilifanya uchunguzi wa shauri hili na kupeleka kesi mahakamani baada ya upelelezi kukamilika,” alidai Tersila. Wakili wa Serikali Mwandamizi, Filex Kwetukia alidai kwamba, ombi la kukamatwa kwa Francis Mroso limepelekwa kinyume cha kifungu cha 17 cha sheria ya mwenendo wa makoa ya jinai kwa kuwa ilitakiwa kusomwa pamoja na kifungu cha 13 cha sheria hiyo.

Alidai kimsingi kifungu cha 13 (1), sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kinataka taarifa kutolewa kwa kesi ambayo ipo mahakamani kwa kuwa sheria inataka kutolewa kwa hati ya kukamatwa na sababu. Aidha, alidai hakuna hati ya mashtaka ya Mroso, bali amesimama kama shahidi wa mashtaka dhidi ya Sabaya na wenzake sita.

“Hakimu suala la shahidi na ushahidi wa shahidi mahakamani umeratibiwa na kifungu cha 141 cha sheria ya ushahidi na kifungu hiki kipo wazi na hakuna kesi inayoweza kufunguliwa dhidi shahidi wetu kwa kuwa amezungumza ukweli mahakamani kwa kuwa alilazimishwa kutoa fedha,” alidai.

Baada ya kujibiwa kwa hoja hizo, Hakimu Kisinda aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 6 mwaka huu atakapotoa uamuzi mdogo.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/a947906f75f0dd8c9c81a147b4848fb9.jpeg

NAIBU Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde, ...

foto
Mwandishi: Na John Mhala, Arusha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi