loader
Wakulima wa korosho wilaya 4 wajiingizia bil 51.1/-

Wakulima wa korosho wilaya 4 wajiingizia bil 51.1/-

WAKULIMA wa Mkoa wa Lindi na Morogoro wanaohudumiwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha RUNALI, wamejiingizia jumla ya Sh bilioni 51 na milioni 100 katika minada sita ya korosho iliyoendeshwa na chama hicho hadi sasa.

Kauli hiyo ilitolewa na Mhasibu Mkuu wa Chama hicho, Hashim Abdallah wakati akielezea maendeleo ya malipo kwa wakulima wanaohudumiwa na chama hicho kwenye mnada wa saba  wa korosho uliofanyika mwishoni mwa wiki wilayani Ruangwa.

Runali wanahudumia wakulima wa wilaya ya Ruangwa, Nachingwea na Liwale. Wilaya hizo tatu zilipata Sh bil 51.

Pia kwa msimu huu wamekuwa wakihudumia wakulima wa Ulanga waliopo Mkoa wa Morogoro. Ulanga kutokana na upya wao katika kilimo hicho wameomba Runali kusaidia wakulima wao kupata soko la korosho na hadi mnada wa sita unakamilika wameshalipwa Sh milioni 100.

Alisema kutokana na mikakati waliyoiweka wamekuwa makini na kasi katika malipo na kwamba wale ambao hawajalipwa ni wenye matatizo katika akaunti zao.

Akizungumzia fedha hizo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ruangwa, Mikidadi Mbute aliwataka wakulima kujenga utamaduni wa matumizi bora ya fedha ikiwa ni pamoja na kuweka akiba kwa mwaka ujao.

Alisema fedha walizozipata katika msimu huu kutokana na mazingira yaliyopo sasa wasimalize katika anasa na badala yake waweke kwa ajili ya msimu ujao ambao kutokana na mabadiliko ya tabianchi hawawezi kuelewa nini kitakachotokea.

Akizungumzia mnada wa saba wa Runali, Mbute alisema umeenda vyema na kwamba wakati wanaelekea mwishoni mwa msimu ni vyema wakulima wakahakikisha kwamba wanaingiza ghalani korosho nzuri zitakazosaidia kuendelea kuwa na bei ya juu katika mauzo.

Katika mnada huo wa saba uliofanyika Kijiji cha Mwenge kwenye Chama cha Msingi Mitumbati jumla ya kilo 2,934,266 ziliuzwa wakati mahitaji yalikuwa kilo 23,295,167.

Ilielezwa kuwa kampuni 17 zilishiriki katika mnada ambapo bei ya juu ilikuwa Sh 2,330 na chini Sh 2,292. Aidha, korosho za Morogoro bei ya juu  ilikuwa Sh 2,100.  Kampuni zilizonunua korosho hizo ni Export, Ospher, MGM, Thabita, Sedaco, Udhaya, Amago, Blaizing na Sibatanza.

Wakizungumza bei waliyokubali kuuza wakulima wengi waliohojiwa waliitaka serikali kusaidia kuimarisha bei ya korosho kwani wanaoipata kwa sasa inawanyima kujinasua na umaskini waliokuwa nao.

"Serikali isimamie ipasavyo ili bei iwe juu. Tulitarajia mwaka huu kwa upungufu wa korosho tufikie kilo Sh 3,000 lakini sivyo," alisema mkulima Gerlod Joseph wa Kijiji cha Mitumbati na kuongeza kuwa kuna uhaba wa korosho lakini bado bei haitaki kupanda.

Alisema kilimo cha korosho kina safari kubwa na ngumu ambapo wakati mwingine eka analazimika kutumia laki moja kuisafisha.

Aidha, alisema pamoja na kuletewa pembejeo bado wengi wanalazimika kuzinunua kutokana na za ruzuku kucheleweshwa.

Mkulima mwingine, Clara Mnani wa Kijiji cha Mwenge alisema kwamba wakati umefika kwa serikali kufikiria kusimamia bei za korosho kwa kuwa wakulima wanaumia kwa bei ya sasa.

Naye Mrajis Msaidizi wa vyama vya ushirika Lindi, Consolatha Kiluma aliwataka makarani na viongozi wa vyama vya msingi kuhakikisha kwamba wanapokea korosho bora ili bei ya zao hilo iendelee kuimarika.

Alisema uchanganyaji korosho utawafanya wanunuzi kukimbia au kununua korosho kwa bei ya chini zaidi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/1ac3c9e58e4e1f2af493281568a50135.jpg

NAIBU Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde, ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Ruangwa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi