loader
Mahakama yataja mafanikio miaka 60 ya Uhuru

Mahakama yataja mafanikio miaka 60 ya Uhuru

MAHAKAMA ya Tanzania inajivunia mafanikio iliyopata ndani ya miaka 60 ya uhuru ikiwamo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) yaliyoiwezesha kuharakisha kesi na kuepuka athari za janga la ugonjwa wa Covid-19.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Wilbert Chuma alisema hayo jana ofisini kwake Dar es Salaam alipokuwa akitoa taarifa kuhusu mafanikio ya uendeshwaji wa mashauri katika kipindi cha miaka 60 tangu uhuru.

Alisema katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19, shughuli za mahakama hazikusimama na mashauri yalifunguliwa na kusajiliwa kwa njia ya mtandao.
Alisema mashauri katika hatua za kusikilizwa yalisikilizwa kwa njia ya mahakama mtandao inayowezesha kuendelea bila washitakiwa kupelekwa mahakamani.

 Chuma alisema katika kipindi cha Januari hadi Oktoba, mwaka huu, mashauri 15,970 yalisikilizwa kwa mfumo huo na katika kipindi cha Oktoba peke yake mashauri 1,292 yalisikilizwa katika vituo ikiwamo cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na vilivyoko katika Mahakama Kuu nchini kote.

"Ni katika kipindi hicho tuliona umuhimu wa matumizi ya Tehama katika shughuli za mahakama kwa sababu mashauri mengi zaidi yalisikilizwa na inawezekana kwa wakati ujao mahakama zote zitafanyika kwa mfumo wa mahakama mtandao," alisema.

Alisema kupitia mfumo wa JSDS II, wadau wa mahakama wanaweza kufungua, kusajili na kupata taarifa zinazohusiana na mashauri zikiwamo kesi zilizosajiliwa na zilizotolewa uamuzi kuanzia Mahakama ya Mwanzo hadi Mahakama ya Rufani.

Chuma pia alielezea mafanikio waliyoyapata kupitia maktaba mtandao inayohifadhi na kutoa taarifa za mashauri yanayoendeshwa na kutolewa uamuzi katika mahakama za Tanzania.

 Aidha, alisema kupitia mfumo wa TAMS, mahakama imesaidia wananchi kuepukana na utapeli wa mawakili wasio na usajili kwa kuwapatia taarifa za mawakili wenye usajili wanaoweza kuwatumia katika mashauri yao na pia kuwawezesha wadau wa mahakama kutoa mrejesho kuhusu huduma za mahakama kupitia mfumo OFA unaopatikana katika aplikesheni ya mahakama kwa njia ya simu za mkono.

Chuma alisema mafanikio mengine ni kuanzishwa kwa mahakama inayotembea ambayo iliwezesha mashauri 1,611 kufunguliwa na tayari 1,537 kati ya hayo yalimalizika kutokana na utaratibu uliowekwa kwa mahakama hiyo kumaliza mashauri ndani ya siku 30.

Alisema mfumo wa mahakama mtandao unaoendesha shughuli zote za mahakama bila kuhusisha matumizi ya karatasi umefanikisha kusikiliza mashauri 308, mashauri 285 yakiwa yamefunguliwa mwaka huu katika mahakama ya mfano ya Kigamboni.

Alisema mafanikio yote hayo yamefanikisha ushirikishwaji wa wananchi katika utoaji haki, kuweka uwazi, uwajibikaji na kuleta utulivu na amani kwa sababu haki imekuwa ikipatikana kwa wakati bila kuchelewa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/4f168e381897c38e0af2baed950786e8.jpg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Anna Mwikola

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi