loader
Kasi ukuaji mawasiliano ya simu vijijini yawashusha wananchi mtini

Kasi ukuaji mawasiliano ya simu vijijini yawashusha wananchi mtini

KATIKA miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania (Tanganyika), mabadiliko mengi makubwa yameshuhudiwa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya mawasiliano ya simu mijini na vijijini.

Mabadiliko katika sekta ya mawasiliano na ufikishaji wa habari kwa wananchi umefikiwa baada ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali pamoja na sekta binafsi kwenye miundombinu ya mawasiliano.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Ashatu Kijaji anasema sekta ya mawasiliano huchangia katika uchumi moja kwa moja na kupitia sekta zingine zote ikiwa ni nyenzo ya uwezeshaji katika kuongeza ufanisi wa utendaji kupitia teknolojia ya habari.

Dk Kijaji anasema kabla ya Uhuru, Tanzania ilikuwa na mapungufu makubwa katika sekta ya mawasiliano na maeneo mengi ya nchi hayakuwa na mawasiliano.

Anasema baada ya Uhuru, sasa serikali kupitia wizara yake kwa kushirikiana na sekta mbalimbali zikiwemo wizara, taasisi za umma na binafsi inaendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya mawasiliano ya simu.

Dk Kijaji anasema, mwaka 2009 serikali iliamua kuanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ili kuwezesha jukumu la kufikisha huduma za mawasiliano maeneo ambayo hayana mawasiliano na hayana mvuto wa biashara ya mawasiliano hususani maeneo ya vijijini.

Anasema kulingana na Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa cha mwaka 2019, sekta ya mawasiliano mwaka huo imekua kwa kasi ya asilimia 7.2.

Anasema serikali katika azma ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma ya mawasiliano ya uhakika na kwa gharama nafuu, UCSAF hivi karibuni imetangaza zabuni ya Sh bilioni 37.7 za ujenzi wa minara 224 ya mawasiliano katika maeneo ya kimkakati na mipakani.

Dk Kijaji anasema, hatua hiyo ni pamoja na kuhuisha teknolojia zilizokuwa zikitumika kwenye baadhi ya minara ambazo zilikuwa zina uwezo wa 2G kwenda kwenye teknolojia ya 3G na 4G.

Pia kufikisha huduma ya mawasiliano kwenye halmashauri 10 nchini ambazo ni Mbogwe, Tanganyika, Kakonko, Malinyi, Mtwara Vijijini, Msalala Vijijini, Pangani, Bariadi, Nzega na Kilindi.

Anasema lengo ni kila mwananchi apate huduma za intaneti bila kujali yupo mjini au vijijini kwa sababu huduma ya intaneti ni huduma ya msingi kama ilivyo huduma ya mawasiliano ya simu ambayo kila mwananchi ana haki ya kuipata.

Dk Kijaji anasema kulingana na uchambuzi uliofanywa na UCSAF asilimia 66 ya ardhi ya Tanzania (Geographical Coverage) inafikiwa na huduma ya mawasiliano ya simu za kiganjani.

“Sekta hii ya mawasiliano huchangia katika uchumi moja kwa moja na kupitia sekta zingine zote ikiwa ni nyenzo ya uwezeshaji katika kuongeza ufanisi wa utendaji kupitia teknolojia ya habari (Tehama),” anasema Dk Kijaji.

Pia mifumo ya Tehama na utoaji wa taarifa kwa umma imeboresha miundombinu ya mawasiliano ya simu, redio na runinga, ujenzi wa minara ya mawasiliano, ujenzi na upanuzi wa miundombinu ya Mkongo wa Taifa.

Waziri huyo anasema hadi sasa Tanzania ina jumla ya minara ya mawasiliano 12,902, minara 2,630 inatoa huduma ya 2G pekee na minara 9,579 inatoa huduma ya mawasiliano ya 2G, 3G na 4G.

Anasema mfuko huo umewezesha kujengwa minara 1,068 kwa kutumia ruzuku ya serikali kwa kushirikiana na watoa huduma na hadi sasa takribani Sh bilioni 161 zimetumika kujenga minara hiyo.

Ujenzi wa minara ya mawasiliano umefanyika kwenye kata 2,579 za Tanzania Bara kati ya kata 3,956 ambazo ni sawa na asilimia 65 na kwa upande wa Zanzibar, minara hiyo imejengwa kwenye kata 101 kati ya kata 110 sawa na asilimia 92.

UCSAF kwa kushirikiana na Kampuni ya Simu ya Airtel imejenga mnara wa mawasiliano ya simu katika Kijiji cha Matuli, Kata ya Matuli, wilayani Morogoro na kunufaisha wananchi wa vijiji vitatu.

Dk Kijaji amezindua mnara huo na kuhitimisha kero ya wananchi wa vijiji vitatu kukusanyika kwenye mti wa mkwaju au maarufu mti wa maajabu kupata mawasiliano ya simu.

Mti huo uliopata umaarufu kutoa huduma za mawasiliano, wananchi huweka simu katika makopo na kuhifadhi simu zao katika mti huo ili ujumbe ukifika wajue nani aliwapigia.

“Kwa sasa hatuhitaji mawasiliano ya kampuni moja tu, Watanzania wanahitaji kupata mitandao yote na kwa teknolojia tuliyonayo mnara mmoja unaweza ukafungwa kutoa huduma za kampuni zote za simu na Watanzania wachague wenyewe mtandao wanayoipenda,” anasema Dk Kijaji.

Anasema sekta ya mawasiliano imo kwenye Ibara ya 60 na 61 ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020-2025 ikitaka Watanzania kufikishiwa huduma za mawasiliano kwa asilimia 100 kwa kipindi hicho ni dhamana ya serikali kuhakikisha inafikiwa.

Naye Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba, anasema Kata ya Matuli yenye vijiji vinne vyenye wakazi wapatao 6,103 ni miongoni mwa maeneo yaliyokuwa na changamoto kubwa za mawasiliano ya simu.

Anasema changamoto hizo zilisikika kupitia vyombo vya habari kwamba wananchi wa vijiji hivyo wanalazimika kutumia mti uliopo Kijiji cha Matuli kupata mawasiliano.

Mashiba anasema baada ya Bodi ya mfuko huo kufanya ziara katika kijiji hicho na kujiridhisha kuhusu mahitaji halisi ya huduma za mawasiliano katika Kijiji cha Matuli, uliingia makubaliano na Airtel kufikisha huduma hizo kupitia mradi wa awamu ya tano ya miradi ya mawasiliano vijijini.

Pia hadi sasa mfuko umepeleka huduma ya mawasiliano kwenye kata 1,068 nchi nzima na utaendelea kuongeza matumizi ya intaneti kutoka asilimia 45 ya sasa hadi kufikia 80.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando anasema kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya watahakikisha miundombinu inalindwa ili kuepuka uharibifu na wizi katika eneo hilo.

Naye Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Shaabani ‘Babu Tale’, anaishukuru serikali, mfuko huo na Airtel kwa ujenzi wa mnara wa mawasiliano ya simu uliowaondolea wananchi kero na changamoto walizokuwa wakizipata.

Said Mohamed maarufu kwa jina la Kifuto, mkazi wa Kijiji hicho aliishukuru serikali kwa kutimiza ndoto za wananchi kupata huduma za mawasiliano ya simu kwani sasa watapata maendeleo makubwa ya kijamii na kiuchumi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/767b39343f4dc778eac884bd22b81c1f.JPG

Chama cha wanafunzi wa Kike wa Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: John Nditi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi