loader
Mfumo anwani za makazi, postikodi mapinduzi utoaji wa huduma  

Mfumo anwani za makazi, postikodi mapinduzi utoaji wa huduma  

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu yote muhimu ili yaweze kuifikia na kuiwezesha jamii katika kunufaika na kuondokana na changamoto zinazoikabili jamii.

Tanzania kama yalivyo mataifa mengine duniani, imeweka bayana katika kushiriki kikamilifu katika kupambana na changamoto zinazowakabili wananchi wake ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wa kielimu, kifikra, kiuchumi ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za uzalishaji mali.

Ni kwa mantiki hiyo serikali imeamua kuwekeza na kuanzisha rasmi mfumo wa anwani za makazi na postikodi ikiwa ni moja ya njia muhimu ya uharakishaji wa ukuaji uchumi, biashara kwa wananchi wake.

Mfumo wa matumizi wa anwani za makazi ulizinduliwa hivi karibuni kitaifa jijini Mwanza na Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi na Spika Mstaafu wa Bunge, Anne Makinda na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.

Mradi huo wa anwani za makazi unatekelezwa na serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Akizungumza baada ya kuwasha kitufe kuashiria uzinduzi huo, Makinda alisema mradi huo una umuhimu mkubwa katika kuharakisha shughuli za maendeleo na ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja, kaya, kijiji, kata, wilaya na taifa.

Amewataka watendaji wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri kuhakikisha wanakamilisha uwekaji wa anwani za makazi ikibidi kabla ya Oktoba mwaka huu kurahisisha kazi ya Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti mwakani.

Anasema mfumo wa anwani za makazi umetokana na maelekezo ya Sera ya Taifa ya Posta ya Mwaka 2003 ambayo imeagiza kuwepo kwa anwani za makazi zinazotaja jina la barabara, mtaa na namba ya mtu anapoishi au anapopatikana. 

Pia anasema ni utekelezaji wa Ibara ya 61(m) ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya miaka mitano (2020-2025) inayoelekeza kuhakikisha anwani za makazi zinawekwa nchini ili kurahisisha upatikanaji na utoaji wa huduma mbalimbali.

“Ni utekelezaji wa makubaliano ya Umoja wa Posta Afrika na Umoja wa Posta Duniani ambapo Tanzania ni mwanachama,” anasema Makinda.

Anafafanua kuwa makubaliano hayo yanataka kila nchi mwanachama kuwa na mfumo wa kitaifa wa anwani za makazi unaoharakisha na kurahisisha upatikanaji, utoaji na ufikishaji wa huduma na bidhaa mpaka mahali stahiki alipo mwananchi sambamba na kuwezesha kufanyika kwa biashara mtandao.

Anafafanua kuwa uwekaji wa matumizi ya mfumo huo katika nchi yoyote duniani si hiari ni lazima katika kuharakisha maendeleo na ukuaji wa uchumi.

Makinda anasema kuwa mikopo ya benki inayotolewa kwa wananchi wa kada tofauti nchini inakuwa na riba ya juu ya kuanzia asilimia 10, 16, hadi 20 kutokana na watu wanaoomba mikopo hiyo kutokuwa na anwani za makazi zinazotambulika.

GHARAMA ZA MRADI

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Ashatu Kijaji anaishukuru serikali kwa kutoa fedha kiasi cha Sh bilioni 45 zinazotumika katika utekelezaji wa mradi huo kwenye halmashauri 194 nchi nzima, Bara na Visiwani.

Anasema dhamira ya serikali ni kuwafikia wananchi wote kwenye maeneo yao ili mwananchi anapopata tatizo, ikiwemo nyumba kuungua moto iwe rahisi kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kufika haraka eneo la tukio.

Dk Kijaji anasema mfumo huo ni mama wa mifumo mingi ya utambuzi iliyopo nchini na umeunganishwa na mifumo mingine ya afya, vitambulisho vya taifa na wa Mamlaka ya Mapato (TRA) kupitia Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN).

“Mfumo huu pia umeunganishwa kwenye mifumo ya usajili wa kampuni na usimamizi wa viwanja, lengo kubwa ni kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi,” anasema Waziri Kijaji.

UNAVYOFANYA KAZI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Jim Yonazi anasema mfumo wa utambuzi wa anwani za makazi na postikodi ni miundombinu ya utambuzi unaotambulisha ama unaotoa taarifa mahali mwananchi alipo ili aweze kuhudumiwa.

Anasema anwani ya makazi inaundwa na namba ya nyumba/jengo Jina la Barabara/Mtaa na Postikodi. Postikodi ni utaalamu wa kugawa maeneo ili kurahisisha utambuzi.

“Hapa Tanzania ugawaji wetu unaendana na mipaka ya kiutawala ya Kata ambapo kila Kata ina Postikodi yake,” anasema na kuongeza kuwa jiji la Mwanza limeandika historia kwa kuwa jiji la kwanza ambapo mfumo wa matumizi ya anwani za makazi umezinduliwa kitaifa.

Anasema mfumo huo unapatikana kupitia “Programu tumizi” ya simu za mkononi inayoitwa NAPA Mobile App ambayo inaingizwa taarifa zote za makazi ya watu, majengo ya ofisi za serikali na binafsi, barabara, njia, majina ya vituo vinavyotoa huduma za kijamii kama hospitali, shule, zahanati na vingine.

“App hiyo inafanya kazi kama google map, ambapo mwananchi anaweza kuingia kwenye programu hiyo kupitia simu ya mkononi na kuandika mahali anapotaka kwenda kutoka mahali alipo kwa muda huo na programu hiyo itamuonesha njia ya kupita mpaka kufika sehemu husika,” anaeleza Dk Yonazi.

Anasema wavuti ya mfumo tayari imeundwa na imehifadhiwa katika Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC) na inapatikana kupitia napa.mawasiliano.go.tz.

Kwa mujibu wa Dk Yonazi, kasi ya utekelezaji wa mfumo hususani kusimika nguzo zenye majina ya barabara/mitaa na kubandika vibao vya namba za nyumba si ya kuridhisha.

Anasema katika kushughulikia changamoto hiyo, uelewa unaendelea kutolewa ambapo, wajumbe wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT), makatibu tawala na wakuu wa mikoa, viongozi na watendaji wa halmashauri wamepewa uelewa na kuonesha utayari wa kutekeleza mfumo huo.

“Ili kuongeza kasi ya utekelezaji, tunashirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kujumuisha utekelezaji wa mfumo huo katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022,” anasema Dk Yonazi.

Anasema hadi sasa utekelezaji wa mfumo huo umezifikia kata 135 kati ya 4,067 ambayo ni asilimia tatu zikiwemo halmashauri 21 kati ya 196 sawa na asilimia 12 na mikoa 13 kati ya 31 sawa na asilimia 42.

“Vilevile miongozo miwili imeandaliwa ambayo ni Mwongozo wa Anwani za Makazi na wa Postikodi, orodha ya postikodi imekamilika ambapo kila kata kwa sasa ina postikodi yake,” anasema.

MAONI YA WADAU

Mwakilishi wa Ofisi ya Rais–Tamisemi, Ofisa Mipango wa Miji Mwandamizi, George Joseph anasema nchi zilizo na mfumo wa anwani za makazi duniani zimekuwa zinapunguza kwa kiasi kikubwa majanga na vifo ikiwemo misongamano ya utoaji wa huduma za kijamii na maeneo ya utawala.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula anaishukuru serikali kwa kuanzisha mradi huo kwani anwani za makazi zitahuisha maswala ya ardhi na majengo kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel anasema mfumo huo uliozinduliwa utekelezaji wake umekamilika katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambapo kata zote 18 zenye jumla ya mitaa 175 zimefikiwa na jumla ya nguzo 5,823 zimesimikwa, vibao vya majina ya barabara/mitaa 8,500 na namba za nyumba 109,330 zimefungwa na barabara 9,094 zilizokidhi vigezo zimeshasajiliwa.

Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Julius Peter ameipongeza serikali kwa kuanzisha mfumo huo kwa wananchi ikiwa ni moja ya agizo la Ilani ya CCM ambao utasaidia kuboresha na kuongeza huduma kwa wananchi.

Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Ngusa Samike anasema hadi kukamilika kwa mfumo huo kwa halmashauri ya Jiji la Mwanza, mradi umegharimu Sh 1,655,064,832.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Profesa Faustine Kamuzora anaomba elimu zaidi iendelee kutolewa kwa watendaji na viongozi ili mpango huo muhimu uweze kutekelezwa nchi nzima.

Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Murshidi Ngeze anasema mpango huo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na ameshauri uende sambamba na urasimishaji wa makazi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/46ead57e2494a31332512662b9ec9942.JPG

Chama cha wanafunzi wa Kike wa Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi