loader
FORVAC ‘ngazi’ Kilindi kutatua migogoro ya ardhi, kupanga misitu

FORVAC ‘ngazi’ Kilindi kutatua migogoro ya ardhi, kupanga misitu

WILAYA ya Kilindi ni mojawapo ya wilaya 11 zinazounda Mkoa wa Tanga. 

Ni kati ya wilaya mbili zinazotekeleza Programu ya Kuongeza Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC) mradi wa miaka minne unaofadhiliwa na Serikali ya Tanzania na Finland. Wilaya nyingine ni Handeni

Mradi huu ambao kwa sasa umeshafanya shughuli kadhaa unajibu changamoto kubwa ya uanzishwaji wa makazi/mashamba ndani ya misitu ya hifadhi za vijiji ambapo programu imewezesha upandaji wa miti ya mbao na matunda kama parachichi ili kurejesha uoto wa asili.

Kilindi inayopakana na Handeni kwa upande wa Mashariki, Wilaya ya Simanjiro kwa upande wa Kaskazini, Wilaya ya Kiteto kwa upande wa Magharibi na Wilaya za Gairo na Mvomero kwa Kusini ina ukubwa wa kilometa za mraba 6,442.8 wastani wa asilimia 8.8 za eneo lote la Mkoa wa Tanga lenye ukubwa wa kilometa za mraba 84,594.

Wilaya ya Kilindi ni miongoni mwa wilaya 12 zinazotekeleza programu ya kuongeza thamani ya mnyororo wa mazao ya misitu nchini. Programu inatekelezwa katika vijiji vitano vya Tuliani kwedijero, Mnkonde, Kwamwande, Komnazi na Vunila.

Ofisa Misitu Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Adamu Sylivester anasema kwenye vijiji vyote vitano vyenye programu hiyo wamewezesha upandaji miche ya miti zaidi ya 3,000 katika eneo la shule na Kijiji cha Kwamwande, Mei 2019 na pia kuandaa mafunzo kwa wataalamu wa halmashauri katika kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ngazi za vijiji.

"Programu imewezesha kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji vitatu vya Komnazi, Mnkonde na Tuliani kwedijero na pia kutatua mgogoro wa mpaka wa kijiji kati ya Kijiji cha Mnkonde na Mzunguwasala," anasema Sylivester.

Aliyasema haya wakati akiwasilisha mada ya utekelezaji wa mradi huo katika wilaya hiyo kwa viongozi na watendaji wa mikoa mitatu inayoitengeneza kongano ya Tanga katika mradi huo. Mikoa hiyo ni Tanga, Manyara na Dodoma.

Akizungumza katika warsha kuhusu mpango huo Mratibu wa Forvac kongano ya Tanga, Petro Masolwa, anasema lengo kuu la programu ni kuhakikisha kunakuwa na hifadhi ya misitu na pia kutokana na misitu hiyo faida za kiuchumi zinaonekana kwa jamii na taifa kwa usimamizi endelevu wa rasilimali hizo.

Masolwa anasema ili kuwezesha mnyororo wa kuongeza thamani mazao ya misitu kuanzia mwanzo mpaka mwisho kwa maana ya kuwezesha mchakato wa umiliki wa rasilimali za misitu kwa wanavijiji, kuongeza thamani mazao ya misitu na kuuza na wamekuwa wakiendesha programu ndogo za elimu na uwezeshaji.

Anasema Forvac inayofadhiliwa na Serikali za Tanzania na Finland na kutekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, Tanzania ilianza Julai mwaka 2018 na inatarajia kukamilika Juni mwakani.

Masolwa anasema utekelezaji wa programu hiyo kwa kongano ya Tanga umepangiwa zaidi ya Sh bilioni 1.4 na ndani yake kutakuwa na urejeshaji wa uoto wa asili, uvunaji endelevu, uhifadhi misitu na pia kuanzisha utaratibu wa kusaidia wajasiriamali na vikoba ili kuwapo na mnyororo unaoeleweka na wenye tija kwa wananchi wanaozunguka misitu hiyo.

Kupitia programu ya Forvac Kilindi wamefanya utatuzi wa mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Komnazi na Vunila pamoja na Kijiji cha Komnazi na Kimbe.

Aidha, mafunzo kwa wajumbe 74 wa serikali za vijiji na kamati za maliasili za vijiji vya Komnazi, Tuliani kwedijero na Mnkonde, juu ya Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002 imewezesha kuleta utulivu katika vijiji hivyo na kuanza kujali maslahi ya umma kwa kuendesha doria katika misitu.

"Mradi umetoa mafunzo kuhusu misitu ya hifadhi ya jamii, aina ya doria na jinsi ya kujaza taarifa kwenye daftari la doria ikiwa ni pamoja na mbinu za ukamataji wahalifu wa mazao ya misitu na utunzaji wa vielelezo kwa mujibu wa sheria," anasema Ofisa Misitu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Sylivester.

Katika kuimarisha doria programu imewezesha pikipiki mbili aina ya Yamaha 150 Ybr. Pikipiki moja wamepewa Kijiji cha Mnkonde kwa ajili ya kusaidia usimamizi wa msitu na ya pili imebaki wilayani kwa ajili ya uratibu wa shughuli za usimamizi wa misitu.

Wawakilishi 12 wa vikundi vya ufugaji nyuki, Wilaya ya Kilindi waliwezeshwa kushiriki kwenye sherehe za Nanenane Morogoro mwaka 2019 na mwaka 2020 washiriki sita.

Programu imewezesha wataalamu wawili (mkurugenzi wilaya na ofisa misitu wa wilaya pamoja na wawakilishi wawili (mwenyekiti wa kijiji na mwenyekiti wa kamati ya maliasili ya kijiji) kushiriki mkutano wa mwaka wa usimamizi shirikishi wa misitu ya jamii katika Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi pamoja na ziara ya mafunzo katika Kijiji cha Nanjilinji kilichopo wilayani Kilwa, mkoani Lindi.

Kijiji cha Nanjilinji kimekuwa cha mfano cha utunzaji wa misitu na uvunaji endelevu uliowezesha kufanya mabadiliko makubwa katika kijiji hicho hasa katika miundombinu ya serikali na kuwa msaada mkubwa kwa wajawazito.

Fovarc imewezesha kutambua zaidi faida za uhifadhi wa misitu kutoka kwenye magogo na kuanzishwa kwa ufugaji nyuki na kuwa na makundi ya ufugaji wa nyuki na uchakataji wa mazao ya nyuki.

Aidha, Forvac kupitia mtoa huduma Asasi ya Uhifadhi na Maendeleo ya Mpingo (MCDI) imewezesha kuandaa andiko la biashara la Msitu wa Hifadhi ya Mbwego katika Kijiji cha Mnkonde ili kuanza uvunaji endelevu wa mazao ya misitu.

Kutokana na andiko hilo programu imekiwezesha kijiji hicho kuanza uvunaji endelevu wa mazao ya misitu (mbao na magogo) katika msitu wa Mbwego ambapo magogo 60 yanatarajiwa kuvunwa baada ya maombi ya uvunaji kuridhiwa na kikao cha kamati ya uvunaji wilaya. 

Forvac kupitia Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Ndaki ya Misitu na Wanyamapori imewezesha uandaaji wa mpango wa usimamizi shirikishi wa Msitu wa Mbwego, kijijini Mnkonde.

Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Abel Busalama, anataka mradi huo kujikita zaidi katika ufugaji nyuki na mazao ya nyuki badala ya kuvuna miti kwa ajili ya mbao akitaka misitu ihifadhiwe kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

foto
Mwandishi: Beda Msimbe

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi