loader
RAIS SAMIA SULUHU HASSAN:  Mwanamke hodari Afrika Mashariki na Kati

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN: Mwanamke hodari Afrika Mashariki na Kati

MWANAMKE shujaa, mtoto wa Tanzania kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi na ya Afrika Mashariki na Kati, amekuwa kiongozi wa ngazi ya juu kabisa ya kiutawala katika taifa.

Samia Suluhu Hassan, mwanamke mwenye mvuto wa kipekee katika uongozi aliyebadili fikra kwamba mwanamke hawezi baada ya kuwafunga wengi vinywa kutokana na umahiri wake katika kuongoza nchi anaouonesha mpaka sasa.

Katika kuandika historia ya wanawake maarufu waliowahi kuishi au kuvuma kabla na baada ya ukoloni Zanzibar na Tanzania Bara ilikuwa inaishia kwa Sitti binti Saad (kabla ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar).

Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 wanawake wengi walijitokeza katika uongozi nyanja za siasa, burudani, uchukuzi, habari na mengine.

Katika makala haya mwandishi anaongelea baadhi yao waliofanya vizuri katika maisha yao na kujulikana sana hasa katika siasa, wanahabari, uongozi na burudani hadi leo tunaye Rais Samia ambaye amevuka ngazi zote za utawala wa nchi hadi kuwa rais.

Hatua ya Rais Samia kuwa Rais wa Tanzania na kuhutubia Baraza la Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza akiwa Rais wa nchi kumemsababisha   kuongeza ubora wake na umashuhuri katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wanawake wachache walijulikana katika siasa kama Sitti, Bibi Titi Mohamed, Lucy Lamek, Sofia Kawawa, Maria Nyerere na kwenye muziki wa taarabu ni pamoja na Bi Kidude na Shakila Said.

Kwa Zanzibar walioanza  harakati za  siasa  ni wengi miongoni  mwao ni  akina  Fatuma Karume, Mwanaidi Dai, Mwapombe Haji, Mariam Mohamed Ali, Khadija Jabir Mohamed, Mwashamba Khamis Haji, Nasra Mohamed, Johari Yusuph Akida na wengine. 

Baada ya Muungano wanawake waliongezeka kwenye siasa na uongozi kama Getrude Mongella, Anne Makinda, Anna Abdallah na Sofia Simba.

Kuchomoza kwa jina Samia Suluhu Hassan

Jina hili lilianza kutikisa akili za watu katika siasa visiwani Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Muungano (SMT) kuanzia miaka ya 2000 alipoteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mjumbe Baraza la Wawakilishi na kuteuliwa kuwa Waziri wa Afya wa SMZ. Mwaka 2005 aligombea ubunge Jimbo la Makunduchi na kushinda.

Serikali ya Awamu ya Nne ya SMT  ilimteua kuwa Waziri  katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira na kuanza  kuungana na wanawake wenzake waliokuwa wanavuma kama akina Asha-Rose Migiro, Amina Salum Ali, Anna Kilango Malechella, Anna Tibaijuka, Sofia Simba, Anna Abdallah na wengine kusukuma gurudumu la maendeleo.

Akiwa ndani ya SMT, Samia alionekana ni mchapa kazi wa kuigwa na kusababisha wajumbe wa Bunge la Katiba kumchagua kuwa Makamu Mwenyekiti chini ya Mwenyekiti Samwel Sitta (marehemu).

Nyota zaidi iling’aa kwa Samia baada ya Rais wa Awamu ya Tano SMT, Dk John Magufuli kumteua kuwa mgombea mwenza na baada ya ushindi wa CCM wa kiti cha Urais mwaka 2015, akawa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke katika historia ya Tanzania.

Baada ya kifo cha Dk Magufuli, Machi mwaka huu, kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, Samia aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania na kuandika historia nyingine kwa nchi na Afrika Mashariki.    

Ethiopia, nchi iliyo katika ukanda wa Mashariki ina Rais mwanamke, Sahle-Work Zewde ambaye aliwahi kuja nchini pia. Ethiopia mtendaji mkuu wa nchi ni Waziri Mkuu.

Samia ni mwanadiplomasia mwenye uzoefu ambaye sasa amekuwa kiongozi wa kipekee mkuu na mtendaji wa nchi barani Afrika.

Pamoja na kwamba ameupata urais kwa mujibu wa Katiba, huenda wengi baada ya miaka mitano ijayo, tukapenda aendelee ili kuendeleza mazuri ya watangulizi wake, kuondoa yasiofaa na kubuni mapya kwa ustawi wa Watanzania.

Wito kwa Samia  

Samia amekuwa mwanamke wa kwanza kutoka Tanzania na Afrika Mashariki na Kati kuhutubia Baraza la UN kama rais wa nchi na kugusa mioyo ya watu wengi duniani.  

Ameingia katika orodha ya wanawake maarufu duniani ambao ni viongozi wakuu wa nchi waliopo sasa. Anaingia katika orodha ya wanawake maarufu duniani kama Halimal Yacob wa Singapore, Angela Merkel wa Ujerumani, Zewde wa Ethiopia, Bibi Indira Gandhi na Bemazir Bhutto, Dk Joyce Banda (Malawi), Hellen Johnson Sirleaf (Liberia) na wengine.  

Aidha, tunamkumbusha mama yetu kuwa kuzaa si kazi, kazi ni kulea, Watanzania na dunia nzima wanasubiri na kumuombea malezi bora kwa taifa la Tanzania na Watanzania wote na ushirikiano ndio hitaji lake kuu kumuwezesha kufikia malengo.

Binadamu huishi au kuongoza kwa kutumia mitindo mingi lakini muhimu ni mitatu ambayo ni kurithi, kuiga na kuamua mwenyewe yote hayo yana uzuri na ubaya wake.

Anategemewa kuendeleza miradi mikubwa ya kuikomboa nchi kiuchumi, kupambana na mafisadi bila woga, rushwa, dawa za kulevya, uvivu na wahujumu uchumi ili rasilimali za nchi ziwanufaishe wananchi.

Kwa kuwa Samia alishasema hakuna tofauti kati yake na Dk Magufuli, Watanzania hawana hofu kuwa anaendelea kutekeleza Ilani ya CCM (2020-2025). 

Kikubwa Rais Samia afanye kazi na wenye sifa, utayari, uwezo, uzalendo na ari bila kuangalia jinsia ili afanikiwe.

Nawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano, Kazi Iendelee.

Mwandishi ni mchangiaji wa makala wa gazeti hili.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/a260f2fe7bf1fb88ab0071419ca60231.jpg

Chama cha wanafunzi wa Kike wa Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Ligwa Paulin 

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi