loader
Upendo msingi wa mafanikio kwa Watanzania

Upendo msingi wa mafanikio kwa Watanzania

NDUGU msomaji katika makala yangu ya leo nimeyakumbuka maneno ya waliowahi kuwa viongozi wetu wa kitaifa na jinsi walivyosisitiza umoja wetu Watanzania udumu katika upendo.

Katika maisha ya kawaida neno upendo limezoeleka sana. Watu wengi tunalitumia hata kama wakati mwingine hatumaanishi. Kwa mantiki ya makala haya niruhusu nieleze kidogo maana ya upendo na aina zake.

Upendo ni kitendo cha kuonesha hisia za tofauti za ndani kwa mtu mwingine. Ni hisia zinazoonesha pengine umeridhishwa na mtu huyo, umemkubali, umemhurumia, unataka kuwa karibu naye na mengine kama hayo. Kimsingi kuna aina nne za upendo:

Aina ya kwanza ni ile ya upendo wa agape yaani upendo wa ki-Mungu. Wa pili ni ule upendo wa kirafiki au ‘Phileo. Wa tatu ni ule upendo wa mahaba ya ‘upendo eros’. Huu ni upendo baina ya mume na mke na mwisho ni upendo storge au familia.

Kipindi fulani Dk John Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, alitamka maneno haya, naomba kunukuu: “Hili ndilo ombi langu kwenu, ‘pendaneni’. Maneno haya yanafanana sana na maneno yaliyoandikwa kwenye vitabu vitakatifu kwamba tupendane sisi kwa sisi. Swali la kujiuliza ni sisi akina nani? Je, viongozi tu? Je, wananchi wa hali ya chini tu? Haya maswali ni ya msingi sana.

Aliongeza; ‘na hasa upendo miongoni mwetu. Tupendane wote. Tushikamane katika umoja wetu wa Watanzania. Tukiweka Mungu mbele katika maisha yetu’

Kimsingi, upendo aliokuwa akiuzungumzia hapa ni wa kindugu yaani storge love. Tunaamini kwamba Watanzania wote ni ndugu. 

Katika maandiko matakatifu yanasema Nabii Musa alipoona Muebrania mwenzake anapigwa na Mmisri alishikwa na hasira ya kuona ndugu yake anaonewa hivyo akaamua kumuua Mmisri. Upendo wa kindugu. Swali ni tunauelewa na kuuishi? 

Katika hali ya kawaida ni ngumu kuwatumikia watu kama kiongozi huna upendo na taifa lako; huna upendo na wananchi wa hali zote. 

Ndugu msomaji, wewe na mimi tutakubaliana kwamba penye upendo hakuna fitina, chuki wala usaliti. 

Dhana ya uongozi ni kuwatumikia wananchi wa aina zote yaani masikini kwa matajiri, wasomi kwa wasio wasomi, waajiriwa na wasio na ajira, wafanyabiashara na wakulima. 

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipata kusema: “Njia pekee ambayo uongozi unaweza kutunzwa kama uongozi wa watu ni pale viongozi wanapokuwa na sababu ya kuogopa hukumu kutoka kwa watu”. 

Katika maneno haya wewe na mimi tutakubaliana kwamba ili kiongozi awe na hofu na wananchi lazima kwanza awe na upendo nao. Akiwapenda atahofu hukumu yao kwa kuwa atakosa upendo huo ambao ni muhimu. 

Viongozi wa sasa kuanzia ngazi za familia, kijiji/mtaa, kata, tarafa, wilaya, mkoa na taifa ni lazima kujipima katika kauli hii ya Mwalimu Nyerere katika uongozi wetu.

Rais Samia juzi amezivunja bodi za Mamlaka ya Bandari (TPA) na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kutokana na kutoridhishwa na uendeshaji wa bandari.

Najiuliza hivi bado kuna watu hawajaamua kuwa wazalendo kwa nchi yao? Bado kuna madudu namna hiyo bandarini?

Faida ya miradi isipoenda kwa wananchi wanyonge bali kwa matajiri tu inakuwa haina maana. Tunahitaji kujenga nchi isiyo na ubaguzi na njia pekee ya kuondoa ubaguzi ni kwa kuwajali wananchi wote sawa na kutumia rasilimali kwa ajili ya wote. 

Bahati mbaya makala haya leo inaweza kutopendwa sana lakini kuna umuhimu wa kuwa na mapenzi mema baina yetu Watanzania. 

Hatuna haja ya kuchafua mtu au kazi aliyoifanya kwa wakati ili uweze kuanzisha ajenda inayokufaidisha wewe. Kufanya hivyo ni sawa na kujinafiki mwenyewe. 

Bahati mbaya wanasiasa wetu katika Bara la Afrika, wengi hujitanguliza wao na maslahi yao. Tena wakati mwingine hutenganisha wananchi na viongozi wao. Hutengeneza kila njia kuwepo ombwe kati ya mtawala na mtawaliwa. 

Hupenda kujipendekeza sana ili wapate nafasi za kiuongozi. Hoja yangu ni je, watu wa namna hii wana upendo kweli na wananchi wenzao?

Upendo kwa unaowaongoza ni kufikiria maumivu yao na kutafuta bila kuchoka njia sahihi ya kuwaponya.

Viongozi wafikirie namna nzuri ya kuwasaidia wananchi kuishi kwa amani na upendo katika nchi yao. Viongozi ngazi za chini, wawasaidie viongozi wa kitaifa kufikia malengo mema na kamwe tusirudi kwenye majanga ya kuumizana, kupigana na kuwekeana uchungu unaosababisha watu kuichukia serikali yao, bali wawaweke karibu na kutatua changamoto zao.

Huduma za maji, umeme, dawa hospitalini, barabara bora, masoko ya mazao, pembejeo kwa gharama nafuu, kilimo cha kisasa, elimu bora na miundombinu bora kwa ujumla wake ndio mambo Watanzania wanayataka, yakikosekana watajenga ukuta kati ya watawala na watawaliwa. 

Serikali msikubali hili, kama kuna wanaokwamisha kama alivyosema Rais Samia, wasifumbiwe macho.

Tusijifiche katika kauli za kujipendekeza kwa wakuu wa nchi, bali tuwasaidie kuongoza kwa tija na mafanikio, tusiwe sababu ya wao kushindwa bali kushinda.

Nilisikitika kusikia mmojawapo wa wanasiasa akisema kwamba mikopo ya siku hizi iko wazi lakini ya awali haikuwa wazi! Sasa nikajiuliza mikopo ya awali ipi? Katika awamu ipi ya uongozi? 

Ndugu msomaji wangu, kwa wale Waislamu Kuruani Tukufu katika ‘Hud, 11/90 inasema hakika Mola wangu mlezi ni mwenye kurehemu na mwenye upendo’. Maneno haya yako sawia na yale ya kwenye Biblia Takatifu yanayosema Mungu wetu ni mwingi wa rehema na upendo. Kama Mungu ametupenda Watanzania kuifanya nchi yetu iwe nchi ya ahadi, tusiiharibu.

Watanzania wenzangu hatuna haja ya kuchukiana. Kwanza kwa imani ya Kiafrika walio hai na walio tangulia mbele ya haki huitalifiana. Haifai kuwasema vibaya badala yake kuungana, kuthaminiana ili kuleta maendeleo ya taifa letu pasipo kubaguana.

Sidhani kama wanasiasa wanapaswa kutufarakanisha sisi kwa sisi badala yake tushikamane katika kuleta maendeleo ya taifa letu kwa upendo wa kindugu ambao una manufaa makubwa kwetu sote na Mungu atusaidie.

Mwandishi ni mchangiaji wa makala wa gazeti hili +255 712 246 001;  HYPERLINK "mailto:flugeiyamu@gmail.com" flugeiyamu@gmail.com

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/133617d63c52557d0bfe2038579a13b9.jpg

Chama cha wanafunzi wa Kike wa Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Felix Lugeiyamu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi