loader
Simba yagomea nembo ya GSM

Simba yagomea nembo ya GSM

KLABU ya Simba imegomea kuvaa nembo ya mdhamini mwenza wa Ligi Kuu GSM, ikiandika barua Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) kuomba ufafanuzi juu ya uhalali wa mkataba ulioingiwa kati ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na GSM.

Hivi karibuni GSM iliingia mkataba kudhamini Ligi Kuu kama mdhamini mwenza wenye thamani ya Sh Bilioni 2.1 kwa mkataba wa miaka miwili. Pia, ndio wadhamini wa klabu ya Yanga, Coastal Union na Namungo.

Barua hiyo imekuja baada ya TFF kuwaeleza kuwa nembo ya GSM inahitajika kuvaliwa na timu hiyo katika mechi ijayo ya Ligi Kuu dhidi ya Yanga.

Kwa mujibu wa barua hiyo iliyoandikwa na Mtendaji Mkuu wa Simba Barbara Gonzalez kwenda TPLB,Simba inahoji kwanini GSM idhamini Ligi Kuu wakati ni mdhamini wa Yanga.

Na kwanini siku ya kutangaza udhamini, walijaa viongozi wa Yanga na si klabu zingine na kwamba Simba inanufaika vipi kuitangaza GSM? Kwanini hawakushirikishwa kwenye mchakato.

Mbali na barua hiyo, pia kulikuwa na sauti ya Babra kwenye mitandao ya kijamii jana akizungumzia uamuzi wao: “Hatuwezi kutekeleza tuliloambiwa hadi tupate ufafanuzi na hadi sasa tumelazimishwa kupokea nembo na siku mbili tatu kabla ya mechi ,”.

Alisema kutakuwa na kikao cha maandalizi Bodi ya ligi hivyo, ataenda na wanasheria kuweka mambo sawa.

“Hatutatekeleza kile ambacho wameandika, kikanuni wanaweza kutaka milioni tatu na maamuzi ya mwisho ni kutushusha daraja,”alisema.

Gazeti hili lilimtafuta Mtendaji Mkuu wa TPLB Almas Kasongo kutoa ufafanuzi wa barua hiyo simu yake iliita bila kupokelewa.

Katika hatua nyingine, Simba imemtambulisha Kocha mpya magolikipa Tyron Damos kuziba nafasi ya Milton Nienov.

Tyron amewahi kucheza katika nafasi hiyo katika klabu ya Bidvest Wits kabla ya kuwa Kocha wa magolikipa katika timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini.

Kocha huyo (43) raia wa Afrika Kusini ana elimu ya ukocha wa leseni C ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Kozi ya ukocha wa magolikipa kutoka Shirikisho la Soka Uholanzi na Afrika Kusini.

Amewahi pia kufundisha timu nyingine kama TS Galaxy na Chippa United za huko. Tayari yupo Dar es Salaam kwa ajili ya kazi hiyo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/a3e2c4a6b1822d26bb3906c1a72b9bcb.png

ZIMEBAKI pointi mbili, Mbeya City iwafikie Simba SC ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments