loader
‘Uteuzi wa Samia Forbes wairejesha Tanzania kimataifa’

‘Uteuzi wa Samia Forbes wairejesha Tanzania kimataifa’

KUCHAGULIWA kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa miongoni mwa wanawake 100 wenye ushawishi na nguvu kubwa duniani mwaka 2021, kumeelezwa kuirudisha Tanzania katika nafasi yake kimataifa kama taifa lenye ushawishi mkubwa duniani.

Wachambuzi wa masuala ya kidiplomasia na siasa wamesema ushawishi wa Tanzania siku zote unatokana na utekelezaji wa maazimio ya kimataifa, ikifanya hivyo tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere.

Waliyasema hayo jana walipozungumza na HabariLEO kuhusu mafanikio aliyoyapata Rais Samia kwa kutajwa mwanamke mwenye nguvu na ushawishi mkubwa duniani na jarida linaloheshimika duniani la Forbes.

Mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya diplomasia nchini, Abbas Mwalimu alisema kutokana na hayo, diplomasia ya Tanzania itazidi kuheshimiwa na kuthaminiwa duniani na kuwa Tanzania itazidi kuwa mfano bora.

“Mafanikio haya ya Rais wetu, yatazidi kuimarisha, kuthamini na kuheshimu nafasi ya Tanzania katika diplomasia ya kimataifa kutokana na utekelezaji wa maazimio ya pamoja ya kimataifa,” alisema Mwalimu.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba alisema hatua ya Rais Samia kuchaguliwa mwanamke mwenye ushawishi mkubwa duniani, imethibitisha kuwa Tanzania inaheshimu nafasi ya mwanamke katika jamii.

“Kutokana na ukweli huo nawasihi wana-CCM nchini katika uchaguzi wa 2025 asijitokeze yeyote kumpinga mwenyekiti wetu kwa kuwa amethibitisha kuwa yale tuliyodhani yanaweza kutekelezwa na wanaume kumbe hata wanawake wanaweza,” aliongeza Kamba.

Taarifa iliyochapishwa na Forbes na kunukuliwa na vyombo vya habari duniani, ilisema Rais Samia ameshika nafasi ya 94 huku nafasi ya kwanza ikichukuliwa na Mackenzie Scott aliyewahi kuwa mke wa mtu tajiri zaidi duniani, Jeff Bezos.

Mhariri wa Jarida la Forbes, Maggie McGrath alitaja sababu iliyompa Rais Samia umaarufu mkubwa duniani kuwa ni juhudi alizochukua kudhibiti virusi vya corona kwa kufuata taratibu za kupambana na corona zilizoidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

McGrath alisema kilichoangaliwa kwa wanawake hao sio tu kuwa wana fedha au nafasi za madaraka katika nchi zao, bali kitu kikubwa ni namna anavyotumia fedha zake au nafasi ya madaraka yake katika kutumia fedha alizonazo, sauti yake au majukwaa ya umma kuimarisha jamii.

“Haitoshi tu kuwa na pesa au nafasi ya madaraka katika taifa, sharti awe anatumia fedha alizonazo, sauti yake au majukwaa ya umma kulingana na nafasi yake kuwawezesha wananchi kufikia malengo yao,” alisema McGrath.

Scott ambaye aliachana na bilionea Jeff Bezos na kuolewa na Mwalimu wa Sayansi katika shule zake ndiye mwanamke wa tatu kwa utajiri duniani. 

Nafasi ya pili katika orodha hiyo ni Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris ambaye amepanda juu nafasi moja na kumpiku Christine Lagarde ambaye ni Rais wa Benki Kuu ya Ulaya ambaye ameshuka hadi nafasi ya tatu.

Kwa mujibu wa Mhariri wa Forbes, orodha ya mwaka huu ni ya 18 na hutolewa kila mwaka kutoka katika mataifa 30 duniani na inawahusu wanawake wanaofanya kazi katika idara za fedha, teknolojia, siasa, uvumbuzi, burudani na wote wakiwa na lengo moja.

Orodha hiyo pia inamshirikisha Rais wa Taiwan, Tsai Ing-wen ambaye juhudi zake za kupigania uhuru wa taifa lake na demokrasia imemuweka katika nafasi ya 28 duniani.

Kwa mujibu wa Forbes, wanawake 10 wa mwanzo ni MacKenzie, Kamala Harris, Christine Lagarde, Mary Barra, Melinda French, Abigail Johnson, Ana Patricia Botin, Ursula von der Leyen, Tsai Ing-wen na Julie Sweet.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/d278fb8b64392af1f401f1fec0d85895.jpeg

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mradi wa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu 

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi