loader
…Samia, Uhuru waondoa vikwazo 46

…Samia, Uhuru waondoa vikwazo 46

TANZANIA na Kenya zimekubaliana kuondoa vikwazo 46 vya kibiashara kati ya 64 vilivyokuwa vikikabili biashara baina ya nchi hizo.

Hatua hiyo imechukuliwa ili kuimarisha biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo hali itakayoimarisha zaidi ushirikiano wa kibiashara, uwekezaji na kiuchumi baina ya mataifa hayo makubwa kiuchumi Afrika Mashariki.

Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya waliyasema hayo jana wakati walipozungumza na waandishi wa habari Ikulu, Dar es Salaam baada ya kushuhudia shughuli ya utiaji saini wa hati sita na mkataba mmoja iliyofanywa na mawaziri wa nchi zao.

Rais Samia alisema kumalizwa kwa vikwazo hivyo kunathibitisha kuwa Kenya sio tu majirani wa Tanzania, bali pia ni ndugu wanaounganishwa na mambo mengi yakiwemo ya kihistoria, utalii na Lugha ya Kiswahili inayozungumzwa katika mataifa hayo mawili.

Alisema biashara ya Tanzania na Kenya imekua kutoka Sh bilioni 45 hadi kufikia Sh trilioni moja ambapo biashara hiyo ilikua maradufu baada ya ziara yake nchini Kenya katikati ya mwaka huu iliyowezesha milango ya biashara kufunguliwa kati ya mataifa hayo mawili.

Alisema mkutano wake na Rais Uhuru umewezesha kukubaliana mambo kadhaa yakiwemo kuendelea kushirikiana katika

kupambana na ugonjwa wa Covid-19 kwa sababu ni janga linalorudisha nyuma maendeleo ya kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.

“Tumekubaliana kuendelea kuimarisha mipaka yetu na kuimarisha alama za mipaka yetu ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano katika sekta ya utalii,” alisema Rais Samia.

Alisema wamekubaliana kuwaagiza mawaziri wa pande husika wakutane na kujadili ili kuona ni kwa namna gani nchi zote zinaweza kuimarisha sekta ya utalii kwa kuendelea kupunguza vikwazo vya kibiashara vilivyobaki.

Katika hafla hiyo, Rais Samia alimkabidhi Rais Uhuru cheti maalumu cha ruhusa ya kupewa ndege aina ya korongo 20 kupelekwa Kenya ili kuongeza idadi ya ndege hao nchini humo ambao wamepungua na kubaki 12 pekee.

Katika hatua nyingine, Rais Uhuru alikubali ombi la Rais Samia la kupatiwa faru jike wawili watakaoungana na wenzao madume walio katika hifadhi za taifa za Ngorongoro na Serengeti nchini Tanzania.

Makubaliano mengine yaliyofikiwa na viongozi hao ni pamoja na ujenzi wa bomba la gesi kutoka Tanzania hadi Kenya, hatua iliyosifiwa na Rais Uhuru aliyesema hakutakuwa na ulazima wa Kenya kununua mafuta Uarabuni na badala yake watategemea gesi ya Tanzania ambayo itaokoa mazingira nchini humo.

Aidha, viongozi hao wamekubaliana kukamilisha Barabara ya Ushoroba wa Kaskazini Mashariki kutoka Bagamoyo hadi Malindi, Kenya itakayozidisha ushirikiano

wa kibiashara baina yao na mataifa ya Kusini mwa Afrika.

Pia wamekubaliana kushirikiana katika kudhibiti uhalifu unaovuka mipaka kama vile ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu na dawa za kulevya.

Kwa upande wake, Rais Uhuru alisema tangu Rais Samia afanye ziara Kenya, vikwazo vingi vya kibiashara vimeondolewa na biashara za nchi hizo mbili imepanda mara sita zaidi ya ilivyokuwa hapo awali, akieleza kuwa Tanzania imefaidika zaidi kutokana na hali hiyo. “Ni ukweli kuwa kufunga mipaka hakusaidii nchi yoyote kwa sababu maendeleo ya nchi zetu yanategemeana kama ni hasara ni kwa nchi zote na faida pia ni kwa nchi zote,” alisema Rais Uhuru.

Alisema viongozi wa sasa wa mataifa hayo wanatakiwa watimize malengo ya waasisi wao akiwamo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyesema yuko tayari kuchelewesha Uhuru wa Tanganyika kusubiri wenzake ambao ni Kenya na Uganda.

Aliongeza kuwa lengo la Mwalimu Nyerere ni kuyafanya mataifa hayo kuwa kitu kimoja ambapo siku ya Uhuru yaani miaka 60 iliyopita Mzee Jomo Kenyatta alihudhuria.

Mapema Rais Samia alimkaribisha rasmi Rais Uhuru katika Viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam ambako alikagua gwaride la heshima na kupigiwa mizinga 21.

Rais Uhuru aliwasili nchini juzi asubuhi na kuwa miongoni mwa viongozi wa kimataifa waliohudhuria sherehe za miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika kwenye Uwanja wa Uhuru mkoani Dar es Salaam.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/4a017b636b3659ce8c5abfebbc4ed94a.jpeg

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi