loader
Simba vs Yanga:  Ni mechi ya heshima, kisasi

Simba vs Yanga: Ni mechi ya heshima, kisasi

UNAPOTAJA michezo mikubwa inayoteka hisia za wapenzi wa soka Afrika, huwezi kuukosa mchezo wa wapinzani wa jadi Simba na Yanga ambao umepewa jina la ‘Kariakoo Derby’ kutokana na timu hizi kuwa na mashabiki wengi nchini na nje ya nchi.

Mchezo huu umekuwa ukifuatiliwa zaidi kila mahali ili kuhakikisha kila timu inapata kile inachostahili na kupunguza lawama kwa viongozi wa soka pamoja na kuepusha vurugu.

Sio siri soka la nchi hii limebebwa na timu hizi mbili licha ya Ligi Kuu ya Tanzania kuwa na timu 16 ambazo zinatoka mikoa tofauti na kujikusanyia mashabiki wa huko lakini ni nadra kukuta mtu hazishangilii timu hizi pacha zinazotoka Kariakoo.

Njia rahisi ya kung’amua hili ni timu hizo zinapocheza nje ya jiji la Dar es Salaam, ajabu ilioje uwanja hujaa na kupambwa na rangi mbili kijani na nyekundu kuonesha sapoti ya miamba hiyo ya soka nchini Tanzania.

Yakiwa yamebaki masaa machache kabla ya timu hizo kukutana tena katika mchezo wa Ligi Kuu Bara mzunguko wa kwanza Yanga iko kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 19 huku watani wao wa jadi wakiwa nafasi ya pili na pointi 17.

Mara ya mwisho timu hizi kukutana katika mchezo wa Ligi ilikuwa msimu wa 2020/21, Julai 3, ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Zawadi Mauya.

Rekodi zinaonesha kuwa timu hizi zimekutana mara 106 katika michezo ya Ligi Kuu ambapo Yanga imeshinda mara 38 huku Simba ikiibuka na ushindi mara 31 huku wakitoka katika mitanange 37.

Katika Mabao ya kufunga pia Yanga imeendelea kuwa kinara kwa Simba ikiwa imefunga mabao 151 huku watani wake wakiwa wamefunga mabao 136 tangu walipoanza kukutana katika michezo ya Ligi Kuu.

Yanga pia imeweka rekodi ya kuondoka uwanjani bila kufungwa katika michezo 44 ya watani wa jadi wakati Simba haijaruhusu wavu wake kuguswa mara 32 pekee katika michezo 106 waliyoshuka uwanjani.

Zinapokutana timu hizi rekodi nyingi huandikwa na kuvunjwa lakini haya ni baadhi ya mambo ambayo yametokea na huenda yakatokea leo kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.

Rekodi ya Mkude:

KIUNGO wa kati wa Simba, Jonas Mkude, ameweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee ndani ya kikosi cha Simba ambaye amecheza michezo mingi zaidi ya watani wa jadi baada ya kudumu katika kikosi hicho kwa miaka 11.

Mkude ambaye aliibuliwa na Simba katika michuano ya Uhai Cup mwaka , 2012 akiwa chini ya kocha Suleiman Matola na nyota kama Said Ndemla, Miraji Athuman, Hassan Khatib, Hassan Isihaka, Ramadhan Singano, hadi sasa nyota huyo amecheza michezo 20 dhidi ya Yanga.

Mkude mara ya mwisho

kucheza dhidi ya Yanga ilikuwa katika ushindi wa mabao 4-1, mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam mwaka 2020 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Nani kuvunja rekodi Kibadeni mwaka 1977 Miongoni mwa rekodi ambazo zimedumu kwa muda mrefu ni ile iliyowekwa na mshambuliaji wa zamani wa Simba na timu ya taifa, Taifa Stars, Abdallah Kibadeni ‘King Kibadeni’ kwa kufunga mabao matatu katika mchezo wa watani wa jadi.

Licha ya kupita washambuliaji mahiri kama Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ , Amis Tambwe, Boniface Ambani, Emmanuel Okwi, Hamis Kiiza, Benard Mwalala, Laudit Mavugo na wengine wengi, lakini rekodi ya Kibadeni hadi leo imeendelea kudumu.

Je leo rekodi hiyo itavunjwa na mchezaji gani wakati Simba itakapoikaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa?.

2021 zakutana mara tano Miongoni mwa rekodi nyingine iliyoandikwa mwaka 2021 ni timu hizo kukutana mara tano katika mashindano tofauti, kitu ambacho hakikuwahi kutokea tangu timu hizi zilipoanzishwa.

Miamba hii ilianza kukutana katika fainali ya michuano ya Mapinduzi na Yanga kuibuka na ushindi wa penalti 4-3 baada ya kutoka suluhu katika dakika 90 za mchezo huo hivyo Yanga kutawazwa kuwa mabingwa.

Nyota sita waliocheza timu zote mbili Wachezaji sita wanaenda kukutana na waajiri wao wa zamani huku kati yao watano kutoka Simba waliowahi kucheza Yanga na mmoja kutoka Msimbazi anayecheza Jangwani.

Nyota ambao wamecheza Yanga na sasa wapo Simba ni Hassan Dilunga, Benard Morrison, Ibrahim Ajibu, Gadiel Michael na Yusuph Mhilu huku Adeyun Saleh anakutana waajiri wake wa zamani Simba.

Yanga na bahati ya namba 11 Yanga ni hatari zaidi wanapocheza na Simba katika dakika 11 -15 za kipindi cha kwanza. Michezo mitatu ndani ya dakika hizo, Wekundu wa Msimbazi walifungwa.

Mwaka 2019 mchezo wa mzunguko wa pili, Yanga waliwafunga Simba kwa faulo mfungaji akiwa Morrison ndani ya dakika 11, bao ambalo lilidumu hadi dakika 90.

Yanga iliendelea kuwa na bahati katika dakika 11 za mwanzo msimu wa 2020/21 Yanga waliifunga tena Simba bao la Zawadi Mauya ambaye huo ulikuwa mchezo wake wa kwanza wa watani wa jadi.

Miamba ya Jangwani iliendelea kuwa mwiba kwa Simba ndani ya dakika 11 kwani safari hii kwenye mechi ya ngao ya jamii mwaka huu, alikuwa mshambuliaji mpya wa Yanga raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Fiston Mayele ambaye alipeleka kilio kwa Wekundu wa Msimbazi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/9f838456ff4d3391ad515aab86b599fe.png

TAMASHA la muziki wa dansi ...

foto
Mwandishi: Martin Mazugwa

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi