loader
Pablo, Nabi wakiri ubora

Pablo, Nabi wakiri ubora

MAKOCHA wa timu za Simba na Yanga, Pablo Franco na Nasriddine Nabi, kila mmoja amesifu ubora wa kikosi chake. Simba na Yanga juzi zilikutaka kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara katika uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam na kutoka suluhu.

Kabla ya Mechi, Yanga ilipewa nafasi kubwa ya kushinda kutokana na ubora iliona nao msimu huu, huku Simba ikionekana kushuka kiwango msimu huu. Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti na mechi hiyo kumalizika kwa suluhu. Akizungumza baada ya mechi hiyo kocha Nabi alisema, timu yake ilikosa bahati siku hiyo, na kukiri kuwa Simba imeimarika.

“Tulicheza vizuri na kuutawala mchezo kwa asilimia kubwa na tumetengeneza nafasi kadhaa lakini tumeshindwa kuzitumia na huwezi kumlaumu mchezaji yeyote kwa hilo sababu ni jambo la kawaida kwenye mpira na hao waliokosa ndio wanaotufungia kwenye mechi zilizopita,” alisema Nabi.

Kocha huyo pia alimsifu kocha Pablo Franco wa Simba kwa aina ya uchezaji wa timu yake wa kukaa nyuma na kutegemea zaidi mashambulizi ya kustukiza jambo ambalo lilikuwa tofauti chini ya makocha wawili waliomtangulia, Sven Vandenbreack na Didier Gomes ambao timu yao ilikuwa ikicheza kwa kupandisha mashambulizi na kuruhusu mabao.Aidha kocha huyo hakuacha kuwapongeza wachezaji wake kwa kucheza kwa kujituma na kupata matokeo hayo ambayo alisema wameyapokea ingawa siyo waliyoyakusudia kutokana na malengo waliyokuwa nayo msimu huu.

Kocha huyo alisema anafurahi kuona timu yake imekuwa ikiendelea kuimarika siku baada ya siku na hilo linamfanya kuanza kuwaza ubingwa ingawa bado ni mapema kwa idadi ya mechi zilizosalia lakini tayari ameanza kuona nyota ya mafanikio.

Yanga imeendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 20 katika mechi nane ilizocheza msimu huu huku watani zao Simba wakibaki nafasi ya pili na pointi zao 18. Naye Pablo alimesema sababu ya timu yake kucheza kwa kujihami katika mechi dhidi ya Yanga juzi, ni kutokana na ubora wa wapinzani wao siku za karibuni.

Timu hizo zilikutana juzi kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa na kutoka suluhu, matokeo yaliyomvutia kocha huyo ambaye hiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza kuiongoza Simba dhidi ya Yanga. Akizungumza baada ya mpambano huo Pablo alisema alitumia kipindi cha kwanza kuwasoma watani zao sababu haina ubishi kwa sasa ni timu bora kwenye ligi ya Tanzania, siyo tu kwasababu inaongoza ligi lakini hata uwezo wa mchezaji mmoja mmoja unadhihirisha hilo.

“Kupata pointi moja mbele ya timu bora siyo kitu kidogo, nawapongeza wachezaji wangu kwa kufuata maelekezo naamini mechi ya mzunguko wa pili tutawafunga Yanga sababu tayari nitakuwa nimekiweka sawa kikosi changu na nimewajua vizuri wapinzani wangu,” alisema Pablo.

Kocha huyo raia wa Hispania, alisema haikuwa kazi rahisi hivyo kuwazuia Yanga kutokana na ubora wa safu yao ya ushambuliaji lakini wachezaji wake wa nafasi ya ulinzi wakiongozwa na Hennock Inonga walitimiza majukumu yao vizuri na ndio maana hawakuruhusu bao.

Pablo alisema, waliingia kwenye mchezo huo lengo lao namba moja likiwa ni kuondoka na pointi tatu lakini mambo hayakwenda kama walivyokuwa wamekusudia, ila hakuna kilichoharibika bado anaendelea kukijenga kikosi chake na anaamini muda siyo mrefu mashabiki wataanza kukiona kile anachokitaka.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/f3177ec85cccd129f5e21a2ea41753a0.jpeg

TAMASHA la muziki wa dansi ...

foto
Mwandishi: Na Mohamed Akida

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi