loader
Serikali yapongezwa utulivu nchini 2021

Serikali yapongezwa utulivu nchini 2021

WADAU wa siasa wakiwemo viongozi wa vyama wameipongeza serikali kwa kuweka mising imara iliyoiwezesha nchi kuendelea kuwa na amani na utulivu mwaka huu.

Mwanasiasa mkongwe, Mwenyekiti wa chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema amesema suala la uvumilivu wa kisiasa na kutanguliza maslahi ya nchi ni muhimu ili nchi iendelee kuwa na amani na utulivu.

“Mwaka 1995 nilikuwa maarufu kuliko hata mgombea wa Chama Cha Mapinduzi lakini sikupata umaarufu huo kwa kutoa kauli za vitisho na matusi, bali kwa siasa safi na zenye ustaarabu,” alisema Mrema.

Mwenyekiti wa Chama cha Ada – Tadea, John Shibuda alisema viongozi wa kisiasa wanapaswa kutanguliza mbele maslahi ya taifa pamoja na kusema kwa dhati mambo yanayoweza kuwa msaada kwa nchi.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilindi, Bakari Kingalangala alisema Serikali ya Awamu ya Sita inasikiliza wanyonge na inapenda maridhiano, hivyo kuiwezesha nchi kuwa na utulivu.

Alisema mwaka huu nchi ilipita kwenye kipindi kigumu baada ya kifo cha Rais John Magufuli, lakini uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umekuwa makini kuhakikisha inaendelea kuwa na amani.

“Dunia nzima ilikuwa inatuangalia kama tutaweza kudumu na amani yetu lakini kwa uimara wa Rais Samia tumeendelea kuwa taifa lenye amani na mshikamano pamoja na umoja,” alisema.

Kingalangala alisema wanasiasa wanapaswa kupongeza kasi ya maendeleo na watoe ushauri kwenye upungufu baadala ya kulaumu tu.

Alitoa mwito kwa wanasiasa waache siasa zisizo na tija na wathamini amani, umoja na uzalendo kwa nchi yao.

“Serikali hii ni sikivu hivyo niwashauri wanasiasa wenzangu tunapoona mambo hayaendi sawa tusiwe wepesi wa kulaumu bali tutoe ushauri wa nini kifanyike hapo tutakuwa tumemsaidia Rais wetu,” alisema Kingalangala.

Mchambuzi wa siasa na uchumi, Majjid Mjengwa alisema tangu Januari hadi Desemba, mwama huu Tanzania imepiga hatua kubwa kisiasa kutokana na maamuzi yaliyofanywa na serikali.

“Tulizoea kuona wanasiasa wakizuiwa kufanya shughuli za siasa hadi wakati mwingine kuburuzwa mahakamani kutokana na makosa mbalimbali waliyofanya, lakini tunachokiona sasa hivi ni tofauti, kesi za kisiasa zisizo na msingi zinafutwa na mikutano ya siasa inaruhusiwa,” alisema Mjengwa.

Alipongeza juhudi za serikali kuchagua mazungumzo na majadiliano zaidi kuhusu mustakabali wa siasa katika kujenga siasa safi na demokrasia nchini.

Mjengwa alisema mwaka 2021 unamalizika huku ikionekana nia ya dhati ya serikali ya kutaka kujenga siasa itakayoruhusu ujenzi wa diplomasia ya uchumi.

Diwani wa Kata ya Mwika Kaskazini (CCM), Samuel Shao alisema mwaka 2021 ulikuwa ni wenye majaribu makubwa ikiwamo kupatwa na msiba mkubwa wa kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Dk John Pombe Magufuli pamoja na viongozi wengine mashuhuri.

“Mwaka 2021 hatutausahau kamwe kwani tuliondokewa na aliyekuwa Rais wetu mpendwa Dk Magufuli, tutaendelea kumkumbuka uthubutu wake na uzalendo wake, lakini kwa mwaka 2022 tunategemea serikali iendelee kuwasaidia wananchi na kuondoa umasikini na pia nishauri serikali ione umuhimu wa kuwekeza katika miradi ya kilimo ili kusaidia vijana wetu kujiajiri wenyewe katika sekta hiyo,” alisema Shao.

Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoa wa Kili-

manjaro, Basil Lema alisema mwaka 2021 ulikuwa na changamoto za kisiasa.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, uchumi na diplomasia, Gabriel Mwang’onda alisema maono ya Rais Samia kuifungua nchi kidiplomasia yameimarisha siasa na uchumi wa nchi kutokana na kuwavutia wawekezaji na wafanyabiashara.

“Tumeshuhudia mambo mengi yakifanyika mwaka 2021, kuna kesi nyingi za kisiasa zimefutwa, mikutano ya siasa imeruhusiwa na pia tumeona siasa za maridhiano zikiasisiwa na mkuu wa nchi. Hii maana yake ni kuwa maamuzi ya aina ya siasa tuitakayo yapo mikononi mwetu kwa kushirikiana na Rais,” alisema Mwang’onda.

Imeandikwa na Selemani Nzaro (Dar es Salaam), Amina Omari (Tanga), Upendo Mosha (Moshi).

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/904ff3eb5cc73143f284ee37afbea8af.jpeg

MKUU wa Mkoa wa Mara, Ally ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi