NAIBU Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi amesema Serikali itawachukulia hatua kali za kisheria wananchi wa wilaya ya Kilombero wanaoendelea na vitendo vya kung’oa mawe ya kuonesha mipaka ya vyanzo vya maji kwa lengo la kujiongezea ardhi kwa matumizi ya kibinadamu ikiwemo kilimo.
Mahundi ametoa tahadhari hiyo hwakati wa mkutano na wananchi wa Kata ya Mbingu iliyopo wilaya ya Kilombero , mkoani Morogoro, ambapo amesema vitendo hivyo ni kosa la jinai kwani siku za karibuni tabia ya wananchi kung'oa mawe hayo kwenye mipaka imejitokeza eneo la Bonde la maji la Rufiji.
Onyo la Naibu Waziri ni baada ya kupatiwa taarifa na Serikali ya wilaya ya Kilombero ya kwamba baadhi ya wananchi wa vijiji vya Chiwachiwa na Kisegese wilayani humo wameng’oa mawe 180 kati ya 200 kwa lengo la kupata maeneo ya kilimo na makazi .
“ Ni kosa kwa mwananchi kuingia katika vyanzo vya maji na kufanya shughuli za kibinadamu na ninazitaka mamlaka husika kuwaondoa wananchi wote waliovamia maeneo hayo na wakikaidi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao” amesema Mahundi.
Kwa upande wa miradi ya maji inayoendelezwa katika wilaya hiyo amesema ,kasi ya utekelezaji inaridhisha na serikali ya awamu ya sita itahakikisha inaendelea kutoa fedha ili miradi yote iliyoanzishwa ikamilike kwa wakati.
Naibu waziri amesema , mradi wa maji wa Mbingu , Serikali imetoa Sh bilioni 3.2 ambao kwa sasa unatekelezwa katika vijiji sita vya kata mbili ya Mbingu na Igima na kwa miezi michache iliyopita zilitolewa Sh milioni 400 kwa ajili ya kulaza mabomba na kukamilisha ujenzi wa tenki na shughuli hizo zimeshaanza kwa kasi.
Pamoja na hayo amesema pia serikali itatoa tena kiasi kingine cha fedha Sh milioni 500 ili kuendeleza mradi huo kwa awamu.