WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso ameiagiza Mamlaka ya maji na usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA), kuhakikisha kuwa miradi yote ya maji inakamilika kwa wakati.
Pia amewataka wale wote wanaofanya miradi hiyo kuhakikisha wanalipwa kwa wakati kwani huu si wakati wa kuweka maneno kwenye miradi ya maji bali iwe ni vitendo zaidi ili serikali ijivunie kufanya kazi na wakandarasi wazawa.
Aweso,ametoa agizo hilo Jijini Dodoma wakati akishuhudia utiaji saini wa mikataba ya ununuzi wa pampu za maji 301, zinazolenga kufungwa katika mikoa mbalimbali nchini.
Mkataba huo umesainiwa kati ya Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa) na wazabuni Wazawa kampuni nne moja ikiwa na kandarasi mbili ambapo Sh bilioni 8.89 zitatumika kununua mashine pampu hizo
Aidha, Aweso amesema ili kuleta ufanisi katika miradi ya maji ambayo imetumia kiasi kikibwa cha fedha zilizotolewa katika awamu hii ya sita anapanga kuitisha kikao kati ya wizara hiyo na makandarasi wanaotekeleza miradi ya maji kote nchini.