loader
Samia:Punguzeni matumizi ya nafaka kwenye pombe

Samia:Punguzeni matumizi ya nafaka kwenye pombe

RAIS Samia Suluhu Hassan ametaka mikoa inayotengeneza pombe kwa kutumia nafaka kupunguza matumizi hayo ili kuepusha nchi kukabiliwa na baa la njaa iwapo hakutakuwa na mvua za kutosha mwaka huu.

Vile vile Rais Samia ameiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuandaa mkakati wa pamoja wa kubaini matamasha ya kimkoa na kitaifa ya utamaduni yatakayoboreshwa ili yatumike kufundisha maadili, kutangaza utalii na masuala ya kiuchumi ndani na nje ya nchi.

Rais Samia alitoa rai hiyo jana Mjini Moshi wakati akizindua tamasha la utamaduni mkoani Kilimanjaro, linaloendelea katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, ambapo kutakuwa na maonesho ya mila na utamaduni wa Wachaga, Wapare na Wamasai.

“Tumemsikia mkuu wa mkoa hapa, hili la ukame ni changamoto, niombe mkoa huu  mtengeneze pombe ya mbege kwa kiasi ili tusikabiliwe na njaa kama hakutakuwa na mvua za kutosha,” alisema.

Rais Samia alisema pamoja na kwamba utamaduni ndio utambulisho wa taifa pia ni ajira, kivutio cha utalii na uchumi na kwamba nchi huheshimika kutokana na utamaduni wake.

“Ni wakati sasa wa kuzionesha na kutangaza tamaduni zetu nzuri ili dunia izijue na kuja kuziona. Wizara na wadau wengine waendelee kuratibu, kuvikuza na kuviendeleza vikundi vya burudani za kiutamaduni, kuzalisha kazi za mikono za utamaduni wetu kama vile ufinyanzi, ususi, upishi na uchungaji,” alisema.

Alisema Baba wa Taifa Julius Nyerere aliwahi kusema utamaduni ni kiini na roho ya taifa lolote na kwamba nchi isiyokuwa na utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu wasiokuwa na roho inayowafanya kuwa taifa.

Alimnukuu Nyerere kuwa alisema “katika makosa yote ya ukoloni hakuna lililobaya kupita lile la jaribio la kutufanya tuamini kuwa hatukuwa na utamaduni wetu utamaduni tuliokuwa nao haukuwa na thamani yeyote jambo ambalo ingelifaa tulionee haya badala ya kuwa kitovu cha majivuno.”

Aidha, aliagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ihamasishe mashindano ya tambo, tenzi, nahau na ushauri kwa kutumia mila na usarifu wa lugha ya Kiswahili.

“Nafurahi kusikia wizara imeandaa mwongozo wa matamasha hayo unaoonesha namna ya kuratibu na kuendeleza au kuyaendesha na Mei, mwaka huu katika wiki ya utamaduni litafanyika tamasha kubwa la kitaifa utamaduni litakayoleta mikoa yote. Naagiza katika matayarisho ya tamasha hilo kubwa kuwe na ushirikishi mzuri na machifu na viongozi wa kimila na wadau wengine,” aliagiza.

Aliagiza katika tamasha hilo pia waalikwe mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania na watu wengine mashuhuri ili iwe njia ya kuutangaza utamaduni wa Tanzania na iwe pia njia ya kuutangaza utamaduni duniani kote.

Alisema uzoefu unaonesha matamasha hayo yakiandaliwa kimkakati yanaweza kuvutia wageni wengi kutoka nje kuja nchini kuyaona na kutolea mfano nchini Brazil ambako kuna tamasha la Rio Samba na Ujerumani kuna tamasha la  Oktoba First yanayovutia watalii wengi hadi milioni tano hadi sita kwa wiki moja tu ya tamasha.

Rais Samia alisema katika kuheshimu na kuthamini kwa nia ya kuendeleza utamaduni sanaa zetu na michezo serikali yake iliona haja ya kuongeza nguvu katika sekta hizo kwa kuunda wizara mahsusi itakayosimamia moja kwa moja shughuli hizo bila kuitwisha wizara hiyo jukumu lingine.

Alieleza kuwa walichukua uamuzi huo kwa kutambua umuhimu wa sekta hizo tatu katika kutoa ajira na kukuza uchumi wa nchi lakini pia kuitangaza nchi kimataifa.

Pia, alisema waliamua kuikabidhi wizara hiyo kwa vijana wenye sifa za kielimu, ari na mori wa kuleta mageuzi katika sekta hizo na tayari mageuzi hayo yameanza kuonekana.

Alieleza kuwa tangu, tamasha la Mwanza ambalo machifu walimpatia jina la Hangaya, serikali imekuwa ikibuni na kuratibu matamasha ya utamaduni mbalimbali ikiwemo tamasha la utamaduni na utalii Tanga na tamasha la utamaduni na Sanaa Bagamoyo, tamasha la tambiko la Chifu Kingalu Morogoro na tamasha la utamaduni, maonesho na biashara Mwanza.

Alieleza kuwa tamasha hilo la Kilimanjario  pamoja na kuwa la kipekee kwa kuwa la kwanza  kufanyika kimkoa linafungua milango kwa mikoa mingine kuandaa matamasha zaidi.

Aidha, Rais Samia alijibu hoja tano zilizoibuliwa na Mwenyekiti wa Machifu Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Machifu Mkoa wa Kilimanjaro, Chifu Frank Marealle ambazo ni kuomba kuanzishwa kanzidata sahihi ya machifu nchini na kutambua taarifa za machifu na mchango wao katika mapambano dhidi ya ukoloni.

Hoja nyingine ni kuomba mapango yaliyotumika na machifu kutambuliwa na kutumika kama sehemu za utalii na kuomba kuibuliwa kuimarishwa na kuhifadhiwa kwa majengo na zana za zamani za kimila pamoja na kurejesha mafuvu ya machifu nchini yaliyopelekwa nchi za nje.

Akijibu hoja hizo, Rais alieleza kuwa tayari serikali imeanza kusajili machifu ambapo hadi mwezi huu, machifu 92 walisajiliwa, kazi ya kuwatambua machifu walioshiriki katika mapambano dhidi ya ukoloni imeanza kwa kuwahoji na maeneo 36 yaliyotumiwa na machifu yametambuliwa na uchunguzi unaendelea.

“Kuhusu kutambuliwa kwa majengo na zana za zamani, taarifa zilizopo zaidi ya majengo 200 ya machifu ya kimila yametambuliwa. Pia zana zilizokuwa zikitumiwa nyakati hizo zimehifadhiwa katika makumbusho ya taifa na tafiti zinaendelea. Kurejesha nchini mafuvu ya machifu ili zitumike kitalii, wizara inaendelea na majadiliano juu ya urejeshwaji wa mafuvu hayo,” alisema.

Rais Samia pia alieleza nia yake ya kuongoza jukwaala pamoja la machifu ambalo lilikubaliwa kuanzishwa katika kikao cha machifu kilichofanyika hivi karibuni.

Wakati huohuo, Rais Samia ametoa pole kwa wafugaji na wakulima walipoteza mifugo yao na kushindwa kulima kutokana na janga la ukame.

“Kwa upande wa wakulima nina taarifa kwamba walishindwa kulima na kupanda kutokana na ukame uliokuwepo. Ukame huo ulitokana na kuchelewa kunyesha kwa mvua na kusababisha wananchi kupoteza maelfu ya mifugo yao…. Kwa Mkoa wa Kilimanjaro najua wilaya za Marangu na Same ndio zimekumbwa sana na tatizo hili na mikoa mingine iliyoathirika sana ni Manyara na Arusha,” alisema.

Alisema anaatarajia mvua zilizoanza kunyesha hivi sasa zitaendelea ili ziitoe nchi katika ukame na kuwaomba wafugaji washirikiane na serikali na kutumia mafunzo ya kuona namna bora ya ufugaji wa kisasa usiotegemea mvua katika malisho.

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul aliahidi wizara yake itaendelea kuandaa matamasha ya utamaduni katika kila mkoa kwa lengo la kuwakumbusha watanzania kuhusu mila njema na kutokomeza mila zote zisizo nzuri.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e1e80d0339ad5b3f6476414cbfa215cb.jpg

MKUU wa Mkoa wa Mara, Ally ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi