loader
Tanzania yafungua rasmi  soko la parachichi India

Tanzania yafungua rasmi soko la parachichi India

TANZANIA imefungua rasmi soko lake la zao la parachichi nchini India baada ya juzi Naibu Waziri wa Kilimo Antony Mavunde kusindikiza sehemu ya mzigo wa zao hilo uliosafirishwa kwenda nchini humo.

Akizungumza katika Kiwanja cha Ndege cha  Julius Nyerere muda mfupi kabla ya kusafirishwa kwa zao hilo kwa kutumia ndege ya Kampuni ya ATCL, Mavunde alisema hatua hiyo ni muhimu na zaidi inakwenda kufungua soko la zao hilo kwa wakulima nchini.

“Hatua hii ni historia kwa nchi yetu hasa tunapotekeleza maelekezo ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan ya kuwatafutia masoko ya uhakika wakulima wetu… tumeanza kutimizaa kwa vitendo wakati huu ambapo bidhaa hii imeanza kusafirishwa rasmi,” alisema Mavunde.

Alisema hatua hiyo inatokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na India ambazo kwa pamoja zilikaa na kukubaliana na Novemba 25, 2021 Idara ya Afya ya India ilitoa kibali cha kuiruhusu Tanzania kuanza kusafirisha maparachichi kwenda kwenda nchini humo.

Mavunde alisema nchi ikiwa mzalishaji wa kiwango  kikubwa wa zao hilo, ilipokea kwa umuhimu mkubwa jambo hilo na mwanzoni mwa mwezi huu imesafirisha zaidi ya tani mbili kwenda nchini humo.

Aliwataka wakulima wa maparachichi kulichukua jambo hilo kwa umuhimu mkubwa na zaidi waweke mkazo kuhakikisha wanazalisha kwa wingi kwa kuwa soko la uhakika limepatikana nchini humo.

Mtendaji Mkuu wa ATCL, Ladslaus Matindi alisema kutokana na makubaliano yaliyopo baina ya ATCL na mfanyabiashara anayesafirisha zao hilo kwenda India, Sameer Gupta, mwezi huu pekee watasafirisha wastani wa tani 20 .

Alisema hayo ni mafanikio kwa ATCL pamoja na serikali kwa ujumla hasa baada ya juhudi za muda mrefu za kutafuta masoko ya bidhaa hiyo katika mataifa mbalimbali likiwemo la India huku akiwataka wafanyabiashara wengine kujitokeza na kutumia fursa hiyo.

Mfanyabiashara wa zao hilo, Sameer Gupta alisema ameamua kusafirisha kutokana na mahitaji makubwa ya parachichi yaliyopo India na ni fursa kwake.

Gupta alisema alianza mchakato wa kuomba ridhaa ya kusafirisha bidhaa hiyo tangu mwaka 2018 hadi mwaka huu alipopata rasmi kibali hicho huku akiamini kuwa kusafirishwa kwa zao hilo kutoka Tanzania kutaongeza mapato na kuinua uchumi wa nchi na kuitangaza kimataifa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/92a07b647346b969bed1c648fe09fbbd.jpg

MKUU wa Mkoa wa Mara, Ally ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi