loader
Wapongeza kurejeshwa mafuvu  ya machifu waliokabili ukoloni

Wapongeza kurejeshwa mafuvu ya machifu waliokabili ukoloni

WADAU mbalimbali wa utalii nchini wamepongeza uamuzi wa serikali wa kusaidia urejeshwaji nchini wa mafuvu ya machifu waliopigana dhidi ya utawala kuchagiza maendeleo ya utalii nchini.

Juzi Rais Samia Suluhu Hassan akizindua tamasha la utamaduni katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi mkoani Kilimanjaro alisema kuwa serikali itarejesha mafuvu hayo nchini, ikiwa ni kama sehemu ya kuenzi mchango wao katika uhai wa taifa.

Mdau wa Utalii ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Pongo Safari, Scholastica Ponera alibainisha kuwa uamuzi wa Rais Samia wa kutaka kurejeshwa kwa machifu hao ni wa kizalendo kwa kuwa unaenzi jitihada zilizochukuliwa na mashujaa hao katika kupigania uhuru wa taifa.

Alisema kwa miaka mingi kumekuwa na harakati kama hizo lakini kwa sasa serikali kuona umuhimu kutawezesha pia wanafunzi kujifunza kwa urahisi kuhusiana na mchango wa mashujaa hao katika nchi.

Alisema: “Mafuvu haya yakirejeshwa yatachagiza mapato ya nchi kupitia fedha zitakazokuwa zikitozwa na mamlaka husika ili watu waone mafuvu ya mashujaa wao hawa wa zamani, lakini kikubwa ni kuwa yakirejeshwa yawekwe sehemu za wazi kumwezesha kila mtalii kufika. Lakini pia hata mabaki ya wale mijusi wakubwa kule Ujerumani ambayo kwao inawaingizia fedha za kigeni na kama wakiletwa nchini nasi fedha zitaingia.” Naye Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa, Dk Noel Luoga alisema kwa sasa katika makumbusho hayo kuna nafasi za kutosha kwa ajili ya kuhifadhi kila aina ya historia na mafuvu ya chifu husika.

Alisema, Tanzania ina historia nzuri ya mashujaa wake na namna walivyopigana dhidi ya ukoloni, wengi wamekuwa wakiandikwa tu katika sehemu mbalimbali za makumbusho na vitabuni ila kwa sasa mafuvu yao yakiwekwa hadharani itawawezesha wanafunzi, watalii na hata watafiti kuona ushahidi wa mashujaa.

“Ni wakati sasa wa kutekeleza urejeshwaji wa mashujaa wetu na ninafuraha kusikia Rais Samia ameonesha nia hiyo ambayo hakika utekelezwaji wake unaenda kuwa na tija kubwa,”alisema Dk Luoga.

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro alibainisha kuwa wizara yake imepokea kwa umakini maelekezo hayo na kuwa utekelezaji wake umeshaanza na kuwa mafuvu hao yatarejeshwa.

“Kauli ya rais ni amri na kwa upande wa wizara kwa muda mrefu tuliona umuhimu wa hilo na hakika kwa kauli ya Rais Samia imepokelewa kwa mapenzi makubwa na wadau wa utalii nchini, hawa ni mashujaa wa Tanzania na wanapaswa kuenziwa,”alisema.

Tamasha hilo la utamaduni la Kilimanjaro lilienda sambamba na maonesho ya mila za wachaga, wamasai na wapare. Pia siku hiyo ya uzinduzi Rais Samia alieleza kuwa tayari serikali imeanza kusajili machifu ambapo hadi mwezi huu, machifu 92 walisajiliwa, kazi ya kuwatambua machifu walioshiriki katika mapambano dhidi ya ukoloni imeanza kwa kuwahoji na maeneo 36 yaliyotumiwa na machifu yametambuliwa na uchunguzi unaendelea.

“Kuhusu kutambuliwa kwa majengo na zana za zamani, taarifa zilizopo zaidi ya majengo 200 ya machifu ya kimila yametambuliwa. Pia zana zilizokuwa zikitumiwa nyakati hizo zimehifadhiwa katika makumbusho ya taifa na tafiti zinaendelea,”alisema.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/d9ef406cdc389e0a6024bb05458c90a5.PNG

MKUU wa Mkoa wa Mara, Ally ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi