loader
Ujenzi Soko Kariakoo waanza, kuchukua miaka 2

Ujenzi Soko Kariakoo waanza, kuchukua miaka 2

UJENZI na ukarabati wa Soko la Kariakoo Dar es Salaam, umeanza rasmi mwezi huu na unatarajiwa kukamilika baada ya mwaka mmoja na miezi 10, litakapokamilika litafanya kazi kwa saa 24.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Hassan Rugwa alisema hayo wakati akizungumza na HabariLEO kuhusu ujenzi na ukarabati wa soko hilo ulioanza Januari 7, mwaka huu.

Alisema mkataba wa ujenzi na ukarabati wa soko hilo ulisainiwa Desemba 22 mwaka jana kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam na Kampuni ya Ujenzi ya Estim Construction kwa gharama ya Sh bilioni 26.3.

Akizungumzia soko hilo kufanya kazi kwa saa 24, alisema ni kwa kuwa linatarajiwa kufungwa kamera za ulinzi za kutosha na taa za ulinzi ili kuhakikisha kunakuwepo na ulinzi wa kutosha ili kuruhusu watu kuuza na kununua bidhaa kwa muda huo uliopangwa.

Uwezo wa soko la zamani kubwa na dogo ulikuwa ni kuchukua wafanyabishara 680 waliokuwa kwenye maeneo rasmi, lakini wakijumlishwa na wale waliokuwa kwenye maeneo yasiyo rasmi wanakuwa 1,650.

“Soko jipya na la zamani(litakalokarabatiwa) sasa litakuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 2,300, hii maana yake wale wote waliokuwepo kwenye maeneo rasmi watarudi, na wale waliokuwa kwenye maeneo yasiyo rasmi watapata nafasi. “Na wale ambao hawakuwepo kwenye maeneo hayo 650 watapata nafasi,”alisema.

Akifafanua kuhusu soko jipya la Kariakoo alisema litakuwa na ghorofa za chini ya ardhi mbili(shimoni) kwa ajili ya kuegesha magari ambazo zitakuwa na uwezo wa kuchukua magari 200 kwa wakati mmoja.

Pia alisema soko hilo limebuniwa kwa namna rafiki ambayo itawezesha wateja kufanya manunuzi ya bidhaa kwenye meza mbalimbali wakiwa wanapandisha ghorofa moja baada ya nyingine bila kuhisi kama wanapanda juu.

“Pia kutakuwepo na lifti za huduma mbalimbali. Vilevile ghorofa zitazingatia aina na uzito wa bidhaa kama vile nafaka, mbogamboga, matunda, vyombo, vifaa vya umeme na vinginevyo, kila bidhaa itakuwa na ghorofa yake,”alisema.

Alisema pia katika soko hilo juu kabisa kutakuwa na kumbi za harusi na migahawa. Alisema kazi ya ukarabati na ujenzi imeanza kwa wakati mmoja, pia itakamilika kwa wakati mmoja kwa kuwa eneo ni finyu linategemeana kwenye shughuli zake.

Julai mwaka jana Soko la Kariakoo liliteketea kwa moto uliozuka majira ya saa 3:00 usiku ambao ulianza katika eneo la paa la juu na kusambaa katika maeneo mengine.

Aliyekuwa Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu alisema taarifa za awali moto huo uliathiri wafanyabiashara 224.

Baada ya soko hilo kuungua Rais Samia Suluhu Hassa aliwapa pole wafanyabiashara wa soko hilo kwa hasara waliyoipata iliyosababishwa na moto huo, hivyo aliagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina kujua chanzo cha moto huo.

Mwishoni mwa Julai mwaka jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokea taarifa ya Kamati ya Uchunguzi wa tukio la moto uliotokea katika soko hilo la Kariakoo Julai 10 mwaka jana, taarifa ambayo bado haijawekwa hadharani mpaka sasa.

Kariakoo ni soko kubwa mkoani Dar es Salaam ambalo linawakutanisha wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, lakini pia ni kitovu cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki.

Shughuli za wafanyabiashara wa soko kuu la Kariakoo, Dar es Salaam zimelazimika kusimama na wafanyabiashara waliokuwepo walihamishwa katika masoko mengine likiwemo la Kisutu pamoja na Machinga Complex.

Historia ya jina la soko la Kariakoo inaanzia tangu enzi za ukoloni wa Mjerumani wakati Tanzania Bara ikiitwa Tanganyika. Mahali lilipo soko hilo palijengwa jengo la utawala wa Mjerumani ambalo lilikusudiwa litumike kama ukumbi wa kuadhimisha sherehe za kutawazwa kwa Mfalme Kaiser Wilheim wa Ujerumani kwa wakati huo.

Hata hivyo baada ya jengo kukamilika halikutumiwa kama ilivyokusudiwa badala yake lilitumika kama kambi ya kikosi cha wapagazi waliobeba mizigo ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia waliojulikana kama ‘Carrier Corps’.

Jina hilo la wapagazi wabeba mizigo katika lugha ya Kiswahili lilitamkwa ‘Kariakoo’ na liliendelea kutumika kama jina la eneo lote linalozunguka eneo hilo la Soko la Kariakoo.

Baada ya Vita Kuu ya Dunia kuisha rasmi mwaka 1919 na nchi ya Tanganyika kuanza kutawaliwa na Waingereza, jengo hilo lilianza kutumika kama soko na kuhudumia wakazi wa Dar es Salaam, wakati huo wafanyabiashara walikuwa wakiuza bidhaa zao sakafuni kwa sababu hapakuwa na meza.

Wafanyabiashara waliendelea kufanya biashara zao sakafuni hadi mwaka 1960, meza za saruji zilipojengwa. Kwa kadiri Dar es Salaam ilivyokua na wakazi wake kuongezeka, ndivyo soko hilo lilivyozidiwa na kushindwa kumudu kutoa huduma nzuri kwa Wananchi.

Hali hiyo iliwafanya viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuona haja ya kuwa na soko kubwa na la kisasa kulingana na maendeleo ya jiji, na hivyo uamuzi wa kujenga Soko Kuu Kariakoo ulifanywa na serikali mwaka 1970 ambapo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliagizwa kujenga soko jipya la kisasa ambalo lingechukua nafasi ya Soko la zamani.

Matarajio ya serikali ya kujenga soko yalikuwa kuwapatia wakazi wa Jiji soko kubwa la chakula ambalo lingetosheleza mahitaji yao kwa muda wa miaka 50 hadi 70. Mipango ilikamilika na ujenzi ulianza rasmi Machi 1971.

Ramani ya jengo la soko ilitayarishwa na mchoraji wa ramani za majengo Mtanzania Beda Amuli ambaye alifariki Julai 10, 2016 Dar es Salaam. Kwa mujibu wa machapisho yanayoelezea historia ya soko hilo, mkandarasi huyo alitakiwa kwenda kujifunza nchi za Accra-Ghana na Lusaka -Zambia, kuangalia masoko yaliyojengwa katika miji hiyo miwili, ndipo atengeneze ramani yake.

Ujenzi wa soko ulikamilika mwaka 1975 kwa gharama ya Sh milioni 22 na kufunguliwa rasmi Desemba mwaka huo huo na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere.

Jengo la Soko Kuu la Kariakoo lipo katika kiwanja namba 32 Kata ya Kariakoo, katikati ya makutano ya mtaa wa Mkunguni na mtaa wa Nyamwezi na limezungukwa na mitaa ya Nyamwezi, Mkunguni, Sikukuu na Tandamti.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/21c0a29eb6001c9d937837da0e824889.jpg

MKUU wa Mkoa wa Mara, Ally ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi