loader
Diwani asimulia mauaji  wanafamilia watano

Diwani asimulia mauaji wanafamilia watano

WATU watano wa familia moja waliouawa katika Kijiji cha Zanka, Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma wamezikwa.

Waliouawa ni baba wa familia hiyo, Hosea Kapande (54), mkewe Paulina (53), watoto wao wawili, Isack Hosea (13), Agnes Hosea (10) na mjukuu, Isack Antony (10).

Isack alikuwa ameanza kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Zanka, Agnes na Isack walikuwa wanafunzi katika Shule ya Msingi Zanka.

Akizungumza na HabariLEO jana, Diwani wa Kata ya Zanka, Deo Jeuza alitoa mwito kwa wananchi watoe taarifa ili waliofanya mauaji hayo wakamatwe.

Akisimulia tukio hilo la kusikitisha, Jeuza alisema watu hao waliuawa usiku wa Alhamisi iliyopita na miili yao iligundulika Jumamosi jioni baada ya kuanza kutoa harufu na kwamba imezikwa juzi kwenye makaburi matano.

“Jumamosi jioni nilipigiwa simu na Mtendaji Kata, nilifika eneo la tukio na kukuta watu wameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali na wengine wana alama za kupigwa na nyundo kichwani, watoto walikuwa wametobolewa shingoni na kubondwa kichwani,” alisema.

Alisema baada ya kufanya unyama huo wauaji waliondoka na kufunga mlango kwa nje kwa kutumia komeo.

“Tunasikitika tumepoteza watu watano wakiwemo wanafunzi watatu, mmoja akiwa ameanza kidato cha kwanza mwaka huu na wengine wawili wa shule ya msingi, ni tukio baya sana kwani wameuawa kikatili,” alisema.

Jana mdogo wa marehemu Hosea aliyejitambulisha kwa jina la Jackson alidai kuwa, Jumamosi wakati wakiwa shambani wakilima, walipata taarifa kutoka kwa watoto kuwa katika nyumba ya Mzee Hosea kulikuwa na harufu mbaya.

Kwa mujibu wa Jeuza, tukio kama hilo la mauaji lilitokea mwaka juzi katika Kitongoji cha Zamahero, Kijiji cha Mayamaya, Kata ya Zanka, ambako watu watatu waliuawa akiwemo baba, mkewe na mtoto wao.

Alisema marehemu hao walizikwa kwenye kaburi moja na mpaka sasa wauaji hawajafahamika. Mbunge wa Bahi, Kenneth Nollo alisema katika siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio mengi ya mauaji na kuiomba serikali itekeleze sheria ya kunyonga wanaopatikana na hatia ya kuua.

“Bado kuna tatizo la sheria, mtu anaua halafu anakwenda gerezani kustarehe, nchi kama Marekani muuaji akipatikana na hatia ananyongwa hadharani na watu wanaona, hapa kwetu pamoja na maelekezo ya dini lakini watu wanatakiwa kubanwa na sheria,” alisema Nollo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Onesmo Lyanga alisema Jeshi la Polisi linaendelea kuchunguza mauaji hayo na kuwataka wananchi wawe wavumilivu.

“Kumekuwa na matukio mengi ya mauaji ya kificho, jeshi limejipanga kuwasaka wahalifu wa matukio hayo,” alisema Kamanda Lyanga.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza matukio ya mauaji ya watu wakiwemo wanafamilia wa Zanka.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/1152fecac71ac6ab75e598a89da76523.jpg

MKUU wa Mkoa wa Mara, Ally ...

foto
Mwandishi: Na Sifa Lubasi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi