loader
Maduka ya dawa yaliyo ndani,  karibu na hospitali kuondolewa

Maduka ya dawa yaliyo ndani, karibu na hospitali kuondolewa

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amesema ifi kapo Julai Mosi, mwaka huu maduka yote ya dawa yaliyopo ndani ya hospitali na ndani ya mita 500 kutoka mahali zilipo hospitali yataondolewa ili kutekeleza sheria iliyopitishwa miaka miwili iliyopita.

Ummy alisema hayo wakati wa ziara yake katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jana, ambapo pamoja na mambo mengine alisema wizara yake inaangalia uwekezakano wa ujenzi wa hospitali nyingine kubwa itakayoweza kuwahudumia Watanzania kipindi cha miaka 50 ijayo.

Alisema agizo hilo litakalohusisha pia zahanati pamoja na vituo vya afya nchi nzima, linapaswa kuchukuliwa kwa uzito wake kwani limelenga zaidi kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi hasa wanapokwenda hospitali na kukosa dawa.

“Nimerudi wizarani (Wizara ya Afya), tulitengeneza kanuni maduka yote ya nje ya dawa yanatakiwa kuwa nje umbali wa mita 500, sheria hii niliipitisha kabla sijaondoka wizarani, wenye maduka wote nawatumia salamu kuwa tunakwenda kuyaondoa,” alisema na kuongeza: “Maduka hayo yapo kinyume cha sheria kwa sababu wakati mwingine unakuta hospitalini hakuna dawa na badala yake mgonjwa anaambiwa akanunue katika maduka hayo jambo linalowapa tafsiri tofauti wananchi.”

Waziri huyo alisema anaamini kwa kufanya hivyo kutapunguza wizi na udokozi wa dawa katika hospitali, lakini pia kutaongeza imani kwa wananchi kuwa kuna usimamizi mzuri wa dawa katika hospitali za serikali.

Alisema serikali ilitoa muda wa mpito wa miaka miwili inayoishia Juni 30, mwaka huu ili kutoa fursa kwa baadhi ya wenye maduka hayo ambao walikata leseni zao za biashara kabla ya kupitishwa kanuni hizo, suala alilosema isingekuwa busara kama wangeitekeleza sheria hiyo mara moja.

“Kwa hiyo tumebakisha miezi kama mitano, hakuna cha ‘msalia Mtume’ wala kupeana muda tena, kanuni tumezitunga na zimeshapitishwa kinachotakiwa sasa ni utekelezaji wake,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Ummy alisema serikali inakusudia kujenga hospitali kubwa ya taifa katika Jiji la Dar es Salaam itakayotoa huduma katika kipindi cha miaka 50 ijayo.

Alisema hatua hiyo imelenga kuipunguzia mzigo Hospitali ya Taifa Muhimbili ambayo tangu kujengwa kwake miaka 70 iliyopita, imekuwa ikizidiwa kutokana na kuwahudumia wananchi wengi.

Alisema anaamini Rais Samia Suluhu Hassan atalishughulikia suala la ujenzi wa hospitali hiyo itakayotoa huduma kwa Watanzania wote, huku Hospitali ya Muhimbili ikibadilishwa na kuwa Hospitali ya Kanda ya Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, Ummy alisema wizara yake inashughulikia malalamiko mbalimbali yanayotolewa na wananchi kuhusu utoaji wa huduma katika hospitali mbalimbali ikiwamo ya Muhimbili.

Alisema wizara yake imepokea taarifa mbalimbali zinazolalamikia huduma zisizoridhisha na wakati mwingine juu ya watoa huduma ambapo ameahidi kuzifanyia kazi na kuzitaka hospitali zote za mikoa kuboresha huduma kwa ajili ya kuipunguzia mzigo Hospitali ya Muhimbili.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/096abeca223cbadf0860c359dd35162b.jpg

MKUU wa Mkoa wa Mara, Ally ...

foto
Mwandishi: Na Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi