loader
Samia atoa mwelekeo Sera ya Nje

Samia atoa mwelekeo Sera ya Nje

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema sera mpya ya mambo ya nje itazingatia masuala kadhaa ikiwamo kukitumia Kiswahili kama nyenzo ya diplomasia na biashara.

Alisema hayo jana Ikulu, Dar es Salaam wakati akizungumza na jumuiya ya wanadiplomasia wakiwemo mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini, ikiwa ni ishara ya kuuaga mwaka 2021 na kuukaribisha mwaka 2022.

Alisema serikali ipo kwenye hatua za mwisho za kuibadili Sera ya Mambo ya Nje kwa kuzingatia mabadiliko mbalimbali duniani. Alisema sera hiyo pia itazingatia masuala kadhaa ikiwamo diplomasia ya uchumi, maendeleo mapya ukiwamo uchumi wa buluu, uchumi wa kidijitali, kushirikisha diaspora kwenye maendeleo ya nchi, mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Alilishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni (Unesco) kwa kuiteua Julai 7 kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani na akawashukuru wote waliounga mkono azimio hilo.

Rais Samia alisema Tanzania inathamini uamuzi huo kwa kuwa Kiswahili si tu nyenzo ya mawasiliano ya kila siki lakini pia ni fahari na utambulisho wa mtu.

Alisema Tanzania itaendelea kushirikiana na mataifa mengine kuongeza wigo wa matumizi ya lugha hiyo duniani na akasema pia anaamini kuwa sera mpya ya mambo ya nje ni hatua muhimu ya kuimarisha uhusiano na mataifa mengine katika sekta mbalimbali za kiuchumi.

Aidha, Rais Samia alisema anatambua balozi za nchi zenye uwakilishi nchini zimepata maeneo ya kujenga ofisi na makazi Dodoma, hivyo akawahimiza wazitumie fursa za uwekezaji zilizopo kwenye jiji hilo.

Alisema serikali imefanya juhudi kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini kwa kumaliza vikwazo zikiwamo kodi zinazoweza kuepukwa, sera zisizo rafiki na vikwazo vingine.

Aliwahakiishia viongozi hao kuwa serikali itaendelea kushirikiana nao, nchi zao na mashirika ya kimataifa na anaamini wataendelea kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia kanuni na taratibu za kidiplomasia kwa maendeleo zaidi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/a5403e2bd342501e298d91e43b119754.jpg

MKUU wa Mkoa wa Mara, Ally ...

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi