loader
AfDB yawekeza dola bil 2.47 miradi ya maendeleo nchini

AfDB yawekeza dola bil 2.47 miradi ya maendeleo nchini

SERIKALI imeishukuru Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa kuwekeza Dola za Marekani bilioni 2.47 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alitoa shukrani hizo jijini Dodoma alipokutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Kipronoh Cheptoo.

Alisema benki hiyo imeipatia Tanzania mikopo nafuu na misaada kwenye miradi 23 ya maendeleo na kwamba asilimia 87 ya miradi hiyo iko katika sekta ya miundombinu ikiwamo nishati, barabara, maji na usafi wa mazingira na asilimia 13 imeelekezwa kwenye sekta za kilimo, sekta binafsi na utawala wa kiuchumi.

"Kwa niaba ya serikali na wananchi, ninapongeza uungaji mkono wa Benki ya Maendeleo Afrika katika maendeleo ya nchi kwa kuwa miradi hiyo mikubwa imesaidia kukuza uchumi wa nchi ikiwamo miradi ya barabara ya Ukanda wa Mtwara, Katavi na Tabora," alisema.

Dk Mwigulu aliitaja miradi mingine inayofadhiliwa na AfDB kuwa ni, Kituo cha Pamoja cha Forodha katika mpaka wa Kenya na Tanzania-Namanga ambacho kimesaidia kukuza biashara kati ya nchi hizo na mradi wa maji na usafi wa mazingira Arusha.

Aliitaja miradi mingine ambayo benki hiyo imetoa fedha ni wa barabara za mzunguko katika Jiji la Dodoma na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato.

Cheptoo aliipongeza Tanzania kwa kutekeleza miradi ya kimkakati inayochangia ukuaji wa uchumi wa nchi na maendeleo ya watu.

Alisema benki hiyo ipo tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania ambayo ni mshirika ama mwanachama wa benki hiyo kwa kutoa fedha zaidi zitakazosaidia kukamilisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Cheptoo alisema AfDB itatoa fedha pia kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mipya inayohusu sekta tatu ikiwamo programu ya kuendeleza mapinduzi ya viwanda katika kilimo, uendelezaji wa stadi za kazi na ajira kwa vijana pamoja na mradi wa ujenzi wa Barabara ya Ifakara-Malinyi-Londo hadi Lumecha unaokusudiwa kuiunganisha mikoa wa Morogoro na Ruvuma kwa ajili ya kukuza fursa za sekta ya kilimo katika maeneo hayo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/f32d71d5cb88c313cf0490e7a8722296.jpg

MKUU wa Mkoa wa Mara, Ally ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi