loader
Samia atimiza miaka  62 ya kuzaliwa

Samia atimiza miaka 62 ya kuzaliwa

RAIS Samia Suluhu Hassan leo anasherehekea siku yake ya kuzaliwa akiwa anatimiza umri wa miaka 62. Rais Samia ambaye ni Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita akiwa mwanamke wa kwanza nchini kushika wadhifa huo, alizaliwa Januari 27, 1960 Makunduchi, Zanzibar.

Aidha, ni mwanamke wa tatu kushika nafasi za juu za uongozi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), baada ya Sylvie Kinigi nchini Burundi na Agathe Uwilingiyimana wa Rwanda.

Aliingia madarakani Machi 19, mwaka jana baada ya kifo cha Rais John Magufuli kilichotokea katika Hospitali ya Mzena Machi 17, mwaka jana kutokana na matatizo ya moyo.

Kabla ya kuwa Rais kutokana na kifo cha Dk Magufuli, mwanamama huyo alikuwa Makamu wa Rais kwa sababu ya kuwa mgombea mwenza katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Novemba 5, 2015 aliapishwa kama Makamu wa Rais wa Tanzania akiwa mwanamke wa kwanza kufikia cheo hicho, akarudia baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2020.

Sasa ni Rais wa Kwanza mwanamke na wa pili kutokea upande wa Zanzibar. Rais mwingine aliyetokea Zanzibar alikuwa Rais wa Awamu ya Pili Tanzania, Ali Hassan Mwinyi aliyetawala kwa miaka 10 kutoka mwaka 1985 mpaka 1995. Kielimu, Rais Samia alisoma shule za msingi za Chwaka (Unguja), Ziwani (Pemba) na Mahonda (Unguja) katika miaka ya 1966 hadi 1972.

Aliendelea na masomo ya sekondari shule za Ngambo, Unguja (1973-1975) na Lumumba, Unguja (1976). Baada ya kumaliza masomo yake ya sekondari mwaka1977, aliajiriwa na Wizara ya Mipango na Maendeleo kama karani.

Mwaka 1986 alihitimu katika Taasisi ya Usimamizi wa Maendeleo (IDM) Mzumbe mkoani Morogoro (sasa Chuo Kikuu cha Mzumbe), akipata Stashahada ya Juu katika Utawala wa Umma.

Baada ya kuhitimu, aliajiriwa kwenye mradi uliofadhiliwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani na kati ya 1992 na 1994, alisoma kwenye Chuo Kikuu cha Manchester, Uingereza na kuhitimu Stashahada ya Uzamili katika Uchumi.

Mwaka 2015, alipata Shahada ya Uzamili katika Maendeleo ya Uchumi wa Jamii kupitia mpango wa pamoja kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire.

Katika kazi na siasa, mwaka 2000 alijiunga na siasa akiteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa Mbunge wa Viti Maalumu katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na kisha aliteuliwa na Rais Amani Karume kuwa Waziri wa Utalii na Biashara. Alikuwa mwanamke pekee kwenye ngazi ya mawaziri.

Alichaguliwa tena mwaka 2005 kwenye Viti Maalumu na aliteuliwa tena Waziri katika Wizara ya Kazi, Jinsia na Watoto. Mwaka 2010 aligombea kwenye uchaguzi akiwania nafasi ya ubunge katika Jimbo la Makunduchi na kushinda kwa zaidi ya asilimia 80.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano). Mwaka 2014 alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba iliyokuwa na jukumu la kuandaa Katiba mpya ya nchi. Aprili 30, mwaka jana alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa akiwa Mwenyekiti wa Kwanza mwanamke.

Rais Samia katika maisha yake binafsi, aliolewa mwaka 1978 na Hafidh Ameir ambaye wakati huo alikuwa Ofisa wa Kilimo na wamejaliwa watoto wanne.

Akiwa anakaribia kutimiza mwaka mmoja tangu aingie madarakani, amekuwa akisifika na kupongezwa kwa jitihada zake za kuimarisha uchumi, kudumisha amani na utulivu na ushirikiano wa kimataifa.

Kwa kipindi hicho kifupi amefanikiwa kuitangaza Tanzania kupitia ziara zake mbalimbali na hotuba alizotoa kimataifa jambo lililomjengea sifa ndani na nje ya nchi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/42ee2d1841b6bcaca25b83aed688b84e.jpg

MKUU wa Mkoa wa Mara, Ally ...

foto
Mwandishi: Na Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi