loader
Wazee Dodoma  wampongeza Samia

Wazee Dodoma wampongeza Samia

BARAZA la Wazee la Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma Mjini, limempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uthubutu wake wa kuendelea kujenga makao makuu ya Serikali Dodoma.

Hali kadhalika, wazee hao wamesema fedha za wananchi zimetumika vizuri katika kujenga miradi ya kitaifa. Kutokana na uthubutu huo, baraza hilo limeahidi kuendelea kumpa ushirikiano katika kutimiza dhamira njema aliyonayo kwa Watanzania.

Akizungumza jijini hapa akiwa kwenye ziara ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali ikiwemo Mji wa Serikali na Reli ya Kisasa (SGR), Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Dodoma Mjini, Peter Mavunde alisema dhamira ya Rais Samia ni kielelezo cha kuenzi maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

“Dhamira ya Rais Samia ni kielelezo cha kuenzi maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere,” alisema. Akizungumza kwa niaba ya wazee wa Dodoma, Mavunde alisema: “Sisi kama wazee tupo pamoja naye na tunaahidi kuendelea kumpa ushirikiano na kila aina ya baraka ili aendelee kutengeneza mambo mazuri katika mkoa na Taifa kwa ujumla.” Mavunde alitoa mwito kwa wote waliopewa dhamana ya kujenga majengo ya mji wa serikali kuwa waaminifu kwa kujenga majengo mazuri kama ilivyokusudiwa ili wananchi waone thamani ya pesa iliyotumika.

Akizungumza nyumbani kwake baada ya kutembelewa na wajumbe wa baraza hilo, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda alisema miezi 10 ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani amefanya mambo mengi makubwa.

Baadhi ya mambo hayo alisema ni ujenzi wa madarasa 15,000 nchi nzima, mpango uliowezesha kwa mara ya kwanza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na shule kuanza kwa wakati mmoja.

Pinda ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, alisema kutokana na uamuzi wa Rais Samia kutumia fedha zilizopatikana kwenye Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Coivd-19, umesaidia kuwa na madarasa ya ziada.

“Tunamshukuru Rais Samia, nilikuwa napiga hesabu tangu ameingia madarakani kumbe hata mwaka hajamaliza ni kama miezi kumi hivi kiukweli rais wangu amejitahidi sana hasa kwenye ndoto ya kutuondoa kwenye mgogoro wa kila mwaka kutopata madarasa ya kutosheleza watoto, lakini mama wa watu alivyopata fedha akasema mi nataka nimalize tatizo la madarasa,” alisema. Pinda alisema, uamuzi huo umeweka historia maana kwa mara ya kwanza watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wamejiunga kwa wakati mmoja.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/f5bf26feb42e4df42fc41ca37fab120a.jpg

MKUU wa Mkoa wa Mara, Ally ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi