WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amevita vyuo vya Ufundi nchini kutimiza wajibu ikiwa ni pamoja na kuzalisha wanafunzi watakao weza kujiajiri ama kuajiriwa katika soko la ajira ndani na nje na nchi.
Prof. Mkenda amesema hayo Jijini Arusha alipofanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) ambapo amesema ili kuwezesha wanafunzi wanaomaliza katika vyuo hivyo kukubalika katika miradi mikubwa ya kimataifa ni lazima mitaala ikidhi vigezo vya elimu ya ufundi vya kimataifa.
Waziri Mkenda amesema Mitaala ya Vyuo vya Ufundi lazima iwawezeshe wanafunzi kujiamini katika kujiajiri ama kufanya kazi nje ya mipaka ya nchi na itoe wanafunzi wenye uwezo wa kutumia vifaa na mitambo ya kisasa kwa kuwa Sayansi na Teknolojia duniani inakua kwa haraka sana.
"Uhuishaji wa mitaala ya Vyuo vya Ufundi nchini ni lazima uangalie mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi pamoja na kuhakikisha inafikia viwango vya kimataifa ili kuwezesha vijana wanaopata mafunzo kuwa na maarifa, stadi na ujuzi unaokubalika kimataifa," amesisitiza Prof. Mkenda.