loader
Kikwete apongeza uimara wa Samia

Kikwete apongeza uimara wa Samia

RAIS Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiongoza nchi bila ya kutetereka baada ya kuchukua madaraka kufuatia kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli.

Kikwete aliyasema hayo Chalinze wilayani Bagamoyo wakati wa sherehe za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutimiza miaka 45 ambako alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo kimkoa.

Alisema kutokana na kifo cha ghafla cha Rais Magufuli na yeye kushika kijiti, tusingeshangaa kama angeyumba lakini yeye kasimama imara kwani alilala Makamu wa Rais kaamka Rais.

“Unajua unapochaguliwa ukiwa umejiandaa siyo tatizo kwani unakuwa tayari una mipango umeshaiandaa, lakini unapochaguliwa kabla hujajiandaa ni changamoto mimi mwaka 1995 niliomba lakini kura hazikutosha, lakini baada ya hapo nilijipanga kwa kuweka mipango yangu vizuri kwenye sekta mbalimbali,” alisema Kikwete

Alisema baada ya kukabidhiwa nchi alijiamini na alijipa ujasiri, ujuzi, maarifa na uwezo na aliithibitishia Tanzania na dunia kwani amani na utulivu vipo na nchi inapiga hatua za maendeleo.

“Amefanya mambo makubwa na chama kimebaki vile vile na mambo mazuri yanakuja kwani maono yake na mtazamo wake unaonesha njia kwani hiyo ndiyo sifa ya kiongozi kwani ni kiongozi mchapa kazi, hodari na jasiri kikubwa tumuunge mkono,” alisema Kikwete.

Kuhusu chama, alisema angependa kuona chama kinajengwa na kuhamasisha kiwe na uhai kwa kulipa ada na kufanya mikutano na kuongeza wanachama na jumuiya za chama kazi yake ni kutafuta marafiki na kushiriki kazi za chama.

“Chagueni viongozi ndani ya chama ambao wazuri na tusichague viongozi ambao wanatanguliza maslahi yao binafsi bali maslahi ya chama watakaotupeleka mbele na ambao hawatatukwamisha, tuwakatae watakaotusababishia migogoro,” alisema Kikwete.

Awali, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bagamoyo, Abdul Sharifu alisema wanaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutekeleza ilani kwa kiasi kikubwa ambapo wamepatiwa miradi mingi ya maendeleo.

Sharifu alisema wanachoomba ni Chalinze kuwa wilaya kwani ina sifa ya kuwa wilaya na ombi hilo waliomba kipindi cha Rais Magufuli alipopita Chalinze kwenye ziara zake za kikazi.

 

foto
Mwandishi: John Gagarini, Chalinze

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi