loader
Bandari ya Mtwara yasifiwa kwa huduma bora

Bandari ya Mtwara yasifiwa kwa huduma bora

WAFANYABIASHARA wanaotumia Bandari ya Mtwara wameelezea kuvutiwa kwao na huduma bora na za kisasa zinazotolewa na bandari hiyo.

Miongoni mwa wafanyabiashara hao ni Kampuni ya Mafuta ya Oilcom Tanzania Ltd tawi la Mtwara, Kampuni ya Meli ya Alghubra Marine Services ya Zanzibar, Kampuni ya Uwakala wa Meli ya Southern Shipping Services Ltd na Kampuni ya Makaa ya Mawe ya Ruvuma Coal Ltd tawi la Mtwara.

Mwakilishi wa Kampuni ya Mafuta ya Oilcom Tanzania Ltd, Jackson Tumwanga, aliliambia HabariLeo kuwa Oilcom ni wadau wakubwa wa Bandari ya Mtwara katika uingizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi kwa ajili ya matumizi kwa mikoa ya Kusini mwa Tanzania.

Tumwanga alisema kabla ya kupanuliwa kwa Bandari ya Mtwara, meli zao zilikuwa zikitumia Bandari ya Dar es Salaam ambapo mafuta yalipakuliwa na kupakiwa tena kwenye meli ndogo na kuletwa Mtwara hali iliyowafanya watumie gharama kubwa, lakini kwa sasa meli zao za mafuta zinakwenda moja kwa moja katika Bandari ya Mtwara ambayo imeboreshwa kwa kujengwa gati jipya na kufungwa mitambo ya kisasa.

“Hivi sasa tunaleta mzigo wa mafuta kutoka nje ya nchi moja kwa moja mpaka hapa Bandari ya Mtwara. Tunaridhika na huduma za bandari, vipimo vya ubora wa mafuta, kwa hiyo wafanyabiashara wenzetu waje kutumia Bandari ya Mtwara kwa sababu hakuna foleni ya meli na nafasi ipo ya kutosha,” alisema Tumwanga.

Aliongeza kuwa: “Kila mwezi Oilcom tunapokea meli ya mafuta katika bandari hii, tunaingiza lita milioni 4.8 za petroli na lita milioni 4.8 za dizeli, tupo kwenye mchakato wa kujenga matangi mawili ambapo tangi moja litakuwa la lita milioni 12.5, kwa hiyo tutakuwa na matangi ya lita milioni 25, tunaishukuru Serikali kwa kutuwekea ‘flow meter’ hapa inatusaidia kujua kiasi halisi cha mafuta tunachoingiza.”

Mkurugenzi wa Kampuni ya Meli ya Alghubra Marine Services, Abdulsamad Mohamed Suleiman, alisema kampuni yao inasafirisha saruji kutoka Mtwara kwenda Zanzibar na Comoro.

Suleiman alisema kabla ya upanuzi, mazingira ya kazi yalikuwa magumu lakini baada ya maboresho hayo, Bandari ya Mtwara imekuwa miongoni mwa bandari bora hapa nchini kwa kutoa huduma za uhakika na kwa muda mfupi.

“Tangu Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli mpaka sasa tumeshuhudia upanuzi wa bandari hii. Bandari ya Mtwara kwa sasa hakuna foleni, kuna mashine za kisasa na za kutosha za kushusha na kupakia mzigo, hakuna foleni, gati lina kina kirefu cha maji, meli yetu ina uwezo wa kubeba tani 880 za saruji na tumekodi meli nyingine yenye uwezo kama huu, huduma ya bandari ni nzuri sana,” alisema Suleiman.

Ofisa Utekelezaji wa Kampuni ya Uwakala wa Meli ya Southern Shipping Services Ltd, Esthersia Mallya, alisema tangu kujengwa kwa gati jipya, kumekuwa na mabadiliko makubwa katika Bandari ya Mtwara.

Mallya alisema hivi karibuni walipokea meli ya tani 5,000 iliyochukua saruji kutoka Mtwara kwenda Comoro na waliipakia kwa siku moja tu tofauti na zamani walikuwa wakiipakuwa kwa siku saba hadi kumi.

Mwakilishi wa Kampuni ya Makaa ya Mawe ya Ruvuma Coal Ltd, Saidi Gadafi, alisema kabla ya maboresho ya Bandari ya Mtwara, walikuwa wakisafirisha tani 30,000 za makaa ya mawe kwenda China na India kila baada ya miezi mitatu, lakini sasa wanasafirisha tani 55,000 kila baada ya mwezi mmoja na nusu.

“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inatuunga mkono na tunatarajia kufungua soko jipya Mashariki ya Kati. Wafanyabiashara wengine waje kuitumia Bandari ya Mtwara ina huduma bora, hakuna ucheleweshaji, ushirikiano na menejimenti ni mzuri,” alisema Gadafi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/7033658a1c447ec3d470e9885bc781f2.jpg

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera, Mtwara

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi