loader
Machine mpya Ocean Road kuingiza mabilioni ya fedha

Machine mpya Ocean Road kuingiza mabilioni ya fedha

TAASISI ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) itaingiza Sh bilioni 3.2 kwa mwaka kutokana na kuhudumia wagonjwa 2,000 kutoka nje ya nchi watakaofika nchini kupatiwa huduma kwa kutumia mashine ya kisasa ya kupima saratani mwilini.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk Julius Mwaiselage wakati akizungumza na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii  ilipotembelea taasisi hiyo jana kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo itakapofungwa mashine hiyo.

Alisema kwa ukanda wa Afrika Mashariki ni Tanzania pekee itakuwa na mashine hiyo ambayo inatarajiwa kuanza kutoa huduma kuanzia Agosti, mwaka huu na kuwa utafiti unaonesha nchi nyingi za Afrika zinapeleka wagonjwa kupatiwa huduma hiyo India.

“Kutokana na gharama kubwa za kupeleka wagonjwa kupatiwa huduma hiyo India, nchi nyingi za Afrika zitaona umuhimu wa kuwaleta hapa nchini kwa kuwa kwanza gharama haitakuwa kubwa, hivyo yatakuwa mazingira mazuri zaidi kwao na tumejipanga kuwahudumia kwa ufanisi zaidi kitiba na hata kwa malazi,” alisema Dk Mwaiselage.

Alisema kwa sasa kuna mkakati wa kuongeza wodi za kuhudumia wagonjwa hasa wa wodi maalumu (VIP) na kuwa mkakati unaendelea wa kupata sehemu nyingine kwa ajili ya malazi ya ndugu watakaowasindikiza wagonjwa wao.

Alisema wagonjwa 1,000 walio katika mfumo wa bima ya afya hatua itakayoiingizia taasisi Sh bilioni 1.6 na wagonjwa wa ndani 3,000 wasiokuwa na bima watahudumiwa katika taasisi hiyo na kuingiza mapato ya takribani Sh bilioni 4.8. Alisema gharama ya kuhudumia mgonjwa mmoja ni Sh milioni 1.6.

Akizungumzia zaidi kuhusiana na mashine hiyo, Dk Mwaiselage alisema ndiyo ya kisasa zaidi duniani kwa uchunguzi wa saratani, hivyo itaboresha huduma za saratani nchini kuwa za kiwango cha kimataifa.

Alisema hiyo inatokana na uwezo wa mashine hiyo kugundua saratani mapema zaidi kwa kuwa inaweza kuona chembechembe za saratani kabla hata ya uvimbe kutokea.

Alisema pia itapunguza rufaa za nje ya nchi hasa kwenda India ambako serikali imekuwa ikitumia hadi Sh bilioni tano kwa mwaka ambazo kwa sasa zinaweza kutumika katika miradi mingine ya maendeleo.

Alisema mradi mzima unagharamiwa na serikali, ambapo imetoa Sh bilioni 14.5 na ORCI imeongeza Sh bilioni moja kutokana na mapato yake ya ndani.

Naye Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel alisema  serikali itagharamia wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa gharama hizo Sh milioni 1.6 kwa kuwalipia, huku akiwasisitiza wananchi kukata bima ya afya.

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi