loader
Wananchi 453 wakubali kuhama Ngorongoro

Wananchi 453 wakubali kuhama Ngorongoro

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amepokea orodha ya majina ya awali ya kaya 86 zenye watu 453 waliokubali kwa hiari yao kuondoka kwenye Hifadhi ya Ngorongoro.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa mazungumzo ambayo Majaliwa aliyafanya na wadau wa uhifadhi kwenye vikao vilivyofanyika Februari 14 na 17 mwaka huu kwenye tarafa za Loliondo na Ngorongoro wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.

Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa vyombo vya habari jana ilieleza kuwa Majaliwa alipokea majina hayo jana mara baada ya kumaliza kikao na viongozi wa kimila wa jamii ya Kimasai (Laigwanak) kwenye mkutano uliofanyika eneo la Oretei Loongaik – Marya, kwenye Chuo cha Ufundi Arusha jijini Arusha.

Eneo hilo hufanyika Bunge la viongozi hao na hutumika pia kufanyia ibada za kimila.

Akikabidhi orodha hiyo kwa Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela alisema majina hayo ni ya awali na yalihakikiwa mara baada ya wakazi hao kujiandikisha. “Tutawasimamia vizuri hadi waende kule wapate hati za mashamba, nyumba na maeneo ya kulisha mifugo yao,” alisema Mongela.

Akizungumza na Malaigwanak hao zaidi ya 350, Majaliwa alisema Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara mkoani humo alilieleza taifa iko hatari ya kutoweka kwa hifadhi ya Ngorongoro ndani ya muda mfupi na akatoa maagizo viongozi waende kuwasikiliza wananchi kuhusu hatua za kuchukua ili tunu hiyo isipotee.

“Ile hatari aliyosema Mheshimiwa Rais ni ipi? Zamani watu waliweza kuishi na wanyama bila tatizo kwa sababu kulikuwa na wakazi 8,000 tu wenye ng’ombe 20 hadi 30. Leo hii kuna wakazi 110,000 na mifugo zaidi ya 813,000 wakiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo. “Zamani maboma yalikuwa yamesambaa lakini leo hii nyumba zimejaa, tena za bati na tofali.

Idadi ya watu imeongezeka, idadi ya mifugo imeongezeka na makazi yameongezeka. Hakuna huduma za afya au shule wakati ni hitaji muhimu kwa wananchi,” alisema.

Majaliwa aliwaeleza viongozi hao kwamba serikali imetenga eneo la kilometa za mraba 400,000 wilayani Handeni ambalo kati ya hizo, kilometa za mraba 220,000 zilitumika kwa kujenga nyumba, kupima viwanja na kutenga maeneo ya malisho.

“Tumepima viwanja 2,406 ambapo kati ya hivyo, viwanja 2,070 tumeandaa kwa ajili ya makazi na kila kimoja kina ukubwa wa ekari tatu.

Tumeanza na nyumba za kuanzia 101 za vyumba vitatu vya kulala kwa wale wanaotaka. Tuna viwanja 336 kwa ajili ya huduma kama shule za msingi na sekondari, zahanati na vituo vya afya.

Ujenzi wa mifumo ya maji kazi unaendelea,” alisema na akaongeza: “Umeme wa REA pia utakuwepo.

Huku mlipo hakuna umeme. Haya tutayafanya na Mheshimiwa Rais Samia amesisitiza tuyafanye ili wananchi msipate bugudha,” alisema Waziri Mkuu.

Aliwaeleza viongozi hao wa kimila kwamba Rais Samia ameridhia eneo lao la kufanyia ibada za kimila liendelee kutumika kwa sababu ni jambo jema. “Maeneo yote ya kimila, wananchi waruhusiwe kuendesha mila zao.

Mkuu wa Mkoa simamia hili, ilimradi Mkuu wa chuo apewe taarifa mapema kwamba mnakuja lini kufanya shughuli yenu,” alisema Majaliwa.

Mapema, Kiongozi Mkuu wa Jamii ya Wamasai Tanzania, Isack Ole Kisongo alisema kwa nafasi yao viongozi wa kimila wako tayari kushirikiana na serikali kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha Watanzania wote.

“Kwa kunyanyua rungu zetu tumekula kiapo kwa kukubali kuwa Ngorongoro na hifadhi nyingine nchini zilindwe kwa nguvu zote ili hadhi yake irudi kama zamani,” alisema Kisongo.

Alisema suala la kuhama Ngorongoro halina tofauti na maeneo mengine ambako wananchi waliondoka kwa amani kupisha miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa reli ya kisasa, bomba la mafuta la kutoka Tanga hadi Uganda na ukuta wa Mererani.

Naye Laigwanani wa Malaigwanani wa Ngorongoro, Mzee Matengway Ole Tauwo alimweleza Majaliwa kuwa anasubiri kwa hamu tarehe ya kuhamia huko kwa sababu alikwenda hadi Handeni na akaona mipango ya serikali ina lengo zuri. “Nataka uniambie leo tarehe gani Mkuu wa Mkoa ananipeleka huko, niko tayari kwenda.

Mke wangu alipoona ile nyumba alitaka kugoma kurudi tena Ngorongoro. Nataka nijue tarehe ya kwenda sababu hapa sina hatimiliki, siwezi kulima lakini kule naweza,” alisema mzee huyo mwenye umri wa miaka 70.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/ccfe5318c72af78293ae73d3fab0d8a2.PNG

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi