loader
Serikali yatenga ekari 400,000 walio tayari kuhama Ngorongoro

Serikali yatenga ekari 400,000 walio tayari kuhama Ngorongoro

SERIKALI imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari 400,000 ambazo kati yake ekari 220,000 zimeshapimwa kwa ajili ya wafugaji wanaoishi kwenye Hifadhi ya Ngorongoro walio tayari kuhama.

Hayo yalibainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipozungumza na wabunge, mjini Dodoma juzi.

Alisema eneo hilo lipo katikati ya wilaya za Handeni, Kilindi, Kiteto, Simanjiro na Korogwe.

“Katika hizo ekari 400,000 zilizopimwa ni ekari 220,000 zitakazoanza kupokea wale walioamua kuhama kwa hiari na katika ekari hizo 220,000 vimepimwa viwanja 2,476 mpaka 2,500 ambavyo viko tayari kupokea watu 2,467,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema kati ya viwanja vilivyopimwa vimegawiwa vya makazi pamoja na maeneo ya huduma maalumu.

Alieleza kuwa viwanja vya makazi vipo 2,070 na kuna viwanja 300 kwa ajili ya huduma mbalimbali kama vile kujenga shule, zahanati, kituo cha afya, kituo cha polisi na miundombinu ya maji.

“Kwa wale watakaohamia katika eneo hilo, watapewa maeneo ya kutosha ambapo kila mmoja atapewa ekari tatu kwa ajili ya kujengea nyumba,” alisema na kuongeza kuwa serikali imeanza na nyumba 101 zenye vyumba vitatu vya kulala kwa wale watakaotaka kuhama.

Alisema hali katika Hifadhi ya Ngorongoro ikiendelea kubaki kama ilivyo sasa iko hatari kubwa ya hifadhi hiyo kuendelea kuporomoka na utalii kutokuwepo kabisa.

Alitaja sababu tatu zitakazoharibu hifadhi hiyo kuwa ni ongezeko kubwa la idadi ya watu wanaokadiriwa kufikia 110,000, ongezeko la idadi ya mifugo inayokadiriwa kufikia 813,000 na ujenzi wa nyumba za kudumu zilizojengwa kiholela.

“Haya yote yanasababisha hatari ya kutoweka maeneo yote ambayo taifa limepata heshima na dunia kulitambua eneo la Ngorongoro inayoambatana na eneo la Serengeti,” alisisitiza.

Alisema serikali imefanya jitihada kubwa za kuelimisha wafugaji wanaoishi eneo la Ngorongoro na kuwaeleza umuhimu wa eneo hilo. “Lakini nafurahi na wao wanapopata nafasi ya kuchangia wanasisitiza uhifadhi uendelee,” alisema.

Hivi karibuni, akihitimisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2022/23 na Mfumo wa Ukomo wa Bajeti 2022/23, Waziri Mkuu Majaliwa alisema tayari wananchi 436 kutoka katika kaya 86, wameamua kuondoka wenyewe kwa hiari katika eneo hilo la Ngorongoro.

Hifadhi ya Ngorongoro ilitambuliwa na Unesco mwaka 1979 kama moja ya sehemu ya urithi wa dunia, kutokana na kuwa na sifa mbalimbali ikiwemo ikolojia yake.

Kwa mujibu wa Mtafiti Mstaafu wa Afya ya Mfumo wa Ikolojia, Dk Robert Mfumagwa historia ya hifadhi hiyo inaanzia tangu mwaka 1914 ambapo wenyeji wake walikuwa ni Waharzabe miaka 3,000 iliyopita, Datoga miaka 400 iliyopita na Masai kuanzia miaka 250 iliyopita.

Alibainisha umuhimu wa hifadhi hiyo kuwa ni mfumo wake wa ikolojia inayoiunganisha na hifadhi nyingine za karibu kupitia mzunguko wa kuhama kwa nyumbu.

Nyumbu ni mnyama anayehama ambapo huzaa akiwa katika Hifadhi ya Ngorongoro na kuhama kwa msimu na kuingia katika Hifadhi ya Serengeti, Hifadhi ya Mara, Kenya, Loliondo na kurejea tena Ngorongoro.

Alisema sifa nyingine ni kwamba hifadhi hiyo ni chimbuko la mwanadamu baada ya kukutwa mabaki ya mwanadamu katika eneo la Olduvai Gorge yanayoaminika kuwepo miaka milioni tatu iliyopita.

Alieleza kuwa pia hifadhi hiyo ina kreta yenye uhai wa wanyama yenye ukubwa wa kilometa za mraba 250 na pia ndio eneo lenye faru wengi kuliko hifadhi nyingine nchini.

Kwa mujibu wa Dk Robert, Hifadhi ya Ngorongoro ni eneo la pili kwa uhifadhi wa miamba Afrika baada ya eneo la M’goun Morocco lakini pia ina mchanga unaohama.

Alisema moja ya mafanikio makubwa ya Hifadhi ya Ngorongoro ni pamoja na kutajwa kuwa ni urithi wa duniani, pia ni hifadhi yenye urithi mchanganyiko kwa maana ya malikale na wanyama.

“Mwaka 2013 ilipewa sifa ya kuwa moja ya maajabu saba duniani na ndio hifadhi inayopendwa na watalii wengi kuliko hifadhi nyingine,” alisema.

Hata hivyo, alieleza changamoto zinazoikabili hifadhi hiyo kuwa ni ongezeko kubwa la watu kutoka watu 8,000 mwaka 1959 hadi watu 110,000 mwaka jana, ongezeko la makazi ya watu yanayofikia 21,000, kati yake 5,000 ni kaya masikini zinazotegemea shughuli za kibinadamu kama vile kilimo.

Alitaja changamoto nyingine ni ongezeko la mifugo inayofikia zaidi ya milioni moja inayosababisha kuharibika kwa nyanda za malisho na faru weusi kupungua kutoka faru 108 mwaka 1960 hadi faru 78 mwaka jana.

Tayari hivi karibuni, Unesco kupitia ripoti yake imetishia kuiondoa hifadhi hiyo katika orodha ya maeneo ya urithi duniani kutokana na kukithiri kwa shughuli za kibinadamu, msongamano wa magari na ujenzi ndani ya hifadhi hiyo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika hifadhi hiyo hivi karibuni, alieleza kuwa serikali haitawahamisha kwa nguvu waliojenga ndani ya hifadhi na kuwataka wajiandikishe kwa hiari na kwamba serikali itagharamia mahitaji yao.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/69e4fcf9c838f1ddf7d847b947248bb8.jpg

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi