loader
Samia : Ataka sababu, mbinu kumaliza rushwa

Samia : Ataka sababu, mbinu kumaliza rushwa

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema rushwa ni tatizo kubwa si serikalini tu bali hata kwenye siasa ikiwa ni pamoja na wakati wa uchaguzi.

Alisema hayo jana Ikulu Dar es Salaam baada ya kupokea taarifa ya kikosi kazi alichounda kwa ajili ya kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa.

Taarifa hiyo iliwasilishwa na Mwenyekiti wa kikosi kazi hicho, Profesa Rwekaza Mukandala.

Rais Samia alisema suala la rushwa linataka elimu, hivyo kuna kazi ya kufanya ili wajumbe na watoaji wasitoe au kupokea rushwa.

“Sisi viongozi tunasimama hapa kusema rushwa jamani rushwa, lakini nataka niwaambie wajumbe leo hii mkipewa majimbo kasimamieni mtazitoa kwa njia moja au nyingine, kwa sababu kuna ninyi kuzitoa na kuna wajumbe kuzitaka, kwa hiyo hapa kuna kazi kubwa ya kufanya. Tufunge mioyo ya wajumbe na tufunge mioyo ya watoaji,” alisema.

Rais Samia alisema lazima kuna mambo yanayowafanya watu watoe na kupokea rushwa wakati wa uchaguzi hivyo ibainishwe kwanini na zifanyiwe kazi kwa kuziondoa au kuzipunguza.

“Kwa hiyo hilo dude hilo, siyo kwa serikali, siyo kwa vyama vya siasa, ni tatizo letu Watanzania. Tumepunguza kwa kiasi kikubwa kwa ripoti za ulimwengu, lakini hii ya ndani bado kuna kazi ya kufanya, kwa hiyo nendeni chemsheni kichwa, muainishe sababu kwa nini, zinaondokaje, zinapunguzwaje ili mikono isikunjuke kiasi hicho, vinginevyo wasio na kitu hawataingia kwenye nafasi yoyote,” alisema.

Kuhusu rushwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), alisema taasisi hiyo bado haifanyi kazi yake vizuri, hivyo akakitaka kikosi kazi hicho kulifanyia kazi na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuondoa tatizo hilo.

“Hilo mlilosema siyo la uongo ni la kweli, lakini tuambieni ingawa ukisema wenyewe wanakasirika. Ukisema Jeshi la Polisi hamfanyi kazi vizuri unakwenda kujibiwa, hatufanyi kazi vizuri, huamini vyombo vyako? Kwa hiyo hii kwamba Takukuru hawafanyi kazi vizuri ni kweli, semeni kwa sababu tusiposema hatujengi nyumba nzuri, tutakaposema tutarekebisha, tutajenga nyumba nzuri,” alisema.

Kuhusu ushirikiano kati ya vyama vya siasa na vyombo vya habari, alisema uchaguzi unapoisha uhusiano kati ya vyombo vya habari na vyama vya siasa siyo mkubwa sana kwa kipindi chote cha miaka minne isipokuwa katika mwaka wa mwisho wa kuelekea uchaguzi.

Alisema katika kipindi cha miaka minne kazi kubwa inayofanywa na vyombo vya habari ni kuisema serikali tu.

“Nisisitize kweli, vyama vya siasa na vyombo vya habari tuwe na uhusiano wa karibu. Vyombo vya habari msiwe na maslahi ya kuegemea upande mmoja. Ninyi mnatakiwa kuwa katikati, vyama vya siasa vikifanya vizuri mnavisemea vizuri na kuvipa moyo, serikali imefanya vizuri muiseme serikali vizuri na mnaipa moyo,” alisema Rais Samia.

Aliongeza: “Na tukikosea mnafanya hivyohivyo, mnakosoa vyama vya siasa na mnawaambia makosa yao, na sisi mnatukosoa na mnatuambia makosa yetu. Lakini miaka minne yote ni vyombo vya habari na serikali, mwaka wa mwisho ndiyo vyombo vya habari na vyama vya siasa, tumesema tunaanza ukurasa mpya si ndiyo? Tuanzeni upya. Balile nakutegemea.”

Pia alikitaka kikosi kazi kulifanyia kazi suala la ruzuku kwa vyama vya siasa na kutoa mapendekezo japo siyo rahisi kwa kila chama cha siasa kupata ruzuku. Alisema mtu anapounda chama cha siasa anapaswa kujipima namna atakavyokiendesha.

“Unategemea serikali ikuendeshee chama cha siasa? No! (Hapana), ni chama chenu cha siasa mmejiunda mkasema sisi itikadi yetu ni hii, tutaendesha chama chetu kwa misingi hii. Ruzuku sawa, ipo kwa wale ambao kweli wanafanya kazi, wako bungeni wanachapa kazi, wale unawapa ruzuku wafanye zaidi, lakini hivi vingine je, tuviue? Kwa hiyo kachemsheni kichwa tuone tunafanya nini kwenye vyama vya siasa na ruzuku,” alisisitiza Samia.

Pia Rais Samia alikitaka kikosi kazi hicho kufanyia kazi na kupendekeza namna gani uchaguzi wa serikali za mitaa ufanyike ikiwemo taasisi inayopaswa kuusimamia kama ni Tamisemi peke yake au Tamisemi na Taasisi nyingine.

Aliagiza waziri mwenye dhamana aendelee kulifanyia kazi suala la kanuni za mikutano ya hadhara na kuwepo na kanuni za maadili za kitaifa kwa vyama vyote vya siasa.

Rais Samia alizitaka asasi za kiraia au mashirika yasiyo ya kiserikali zikiwemo taasisi za dini, kushirikiana na kikosi kazi hicho kutoa elimu ya sheria ya vyama vya siasa na elimu ya uraia kwa wananchi ili waelewe masuala ya uzalendo na siasa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/5039953a2f08b49311eafa35c60e954e.jpg

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi