loader
Watoro, wajawazito 909 warejea shuleni

Watoro, wajawazito 909 warejea shuleni

SERIKALI imevunja rekodi katika uandikishaji wanafunzi wa elimu ya awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza huku kukiwa na mwitikio mzuri wa waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali kurejea shuleni.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Gerald Mweli (anayeshughulikia elimu) alisema hayo jana Dodoma wakati wa mafunzo elekezi kwa maofisa elimu watu wazima wa mikoa na halmashauri Tanzania Bara yanayofadhiliwa na taasisi kutoka Ujerumani ya DVV International.

Mweli alisema uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha watoto wote wanakuwa shule na kuwarejesha walioacha shule kwa kujenga madarasa umeongeza uandikishaji wa wanafunzi.

Alisema kwa mwaka huu wa masomo, hadi Februari 28 mwaka huu uandikishaji wa wanafunzi katika elimu ya awali umefikia asilimia 99, wakati wale wa darasa la kwanza wamefikia asilimia 107 na wa kidato cha kwanza wamefikia asilimia 99.

Mweli alisema pia wanafunzi ambao Rais Samia ametoa fursa ya kurudi shule tayari wanafunzi 909 wamerejea shuleni.

Alisema kati ya hao, 384 ni wale walioacha shule kutokana na ujauzito na 525 ni kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za utoro.

“Pamoja na changamoto ya ujauzito lakini tumeona kuna wanafunzi wengine wameacha shule kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo za utoro na ninyi ndio vinara wa kutekeleza programu hii na azma ya Rais Samia ya kuhakikisha watoto wote walioacha shule wanarejea shuleni,” alisema na kuongeza:

“Ingawa mpaka sasa watoto 909 ndio waliorejea shuleni wapo watoto wengine ambao wako mitaani hivyo tuwatie moyo na kuendelea kuwatafuta watoto wote ili azma ya Rais ya kuwarejesha watoto shuleni itimie kwa ukamilifu wake.”

Alisema kutokana na uamuzi wa Rais wa kuruhusu uanzishwaji wa vituo vya watu wazima katika maeneo yote nchini, Maofisa Elimu ya Watu Wazima wanatakiwa kuhakikisha wanasimamia utoaji elimu kwa wanafunzi wanaorejea shuleni na wale walio nje ya mfumo.

Aidha, Mweli alisema kwa sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kutanua Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana Walio nje ya Shule (IPOSA) ambayo kwa sasa inatekelezwa katika mikoa michache.

Awali akifungua mafunzo hayo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, David Silinde aliwataka maofisa elimu watu wazima kuhakikisha wazazi au walezi na jamii wanawapeleka shule wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali.

“Hakikisheni wazazi au walezi na jamii kwa ujumla wanawapeleka shule wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali,” alisema Silinde.

Aliagiza wakurugenzi wa halmashauri zote watenge fedha za kutosha kwa ajili ya programu za Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi na wasimamie utekelezaji wake.

Alihimiza maofisa hao wahakikishe sheria, miongozo na taratibu katika usimamizi wa sekta ya elimu zinazingatiwa ili kufikia malengo ya serikali na kuimarisha usimamizi mzuri wa programu zote za Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi ili ziweze kuwa na tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/ada9d50a5e92726fde8c8c132d7a3a9c.JPG

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi