loader
NMB yazindua huduma 3, Majaliwa atoa neno

NMB yazindua huduma 3, Majaliwa atoa neno

BENKI ya NMB imefanya mapinduzi makubwa ya kibenki baada ya kuzindua huduma kubwa tatu kupitia kampeni yake ya Teleza Kidijitali, zinazomwezesha mteja kupata mkopo kupitia simu ya mkononi bila kufika kwenye ofisi yoyote ya benki hiyo nchini bila dhamana.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika jana jijini hapa na kushuhudiwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga.

Katika hotuba yake, Waziri Mkuu amezitaka taasisi za fedha kubuni mikakati na mbinu zitakazowezesha Watanzania wengi zaidi kupata huduma rasmi za kibenki kwa gharama nafuu ili wajiongezee kipato na kujikwamua na umaskini.

Alisema benki nchini hazina budi kubuni zaidi namna ya kutafuta suluhisho zilizo katika sekta za kifedha kwa manufaa ya wananchi.

“Hongereni NMB kwa ubunifu huu ambao utavutia makundi yote ya kijamii, huduma hii itawezesha wateja wenu kupata huduma ya mikopo kiganjani,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema amevutiwa na huduma hizo ikiwemo ya MshikoFasta ambayo inakwenda kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa haraka kwa mama lishe na baba lishe, bodaboda, wafanyabiashara wadogo na wananchi wote wa kawaida.

Alisema hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan alipozungumza na wamachinga aliziasa taasisi za fedha kulizingatia kundi hilo muhimu na zihakikishe huduma za kifedha zinakuwa rafiki kwao, hivyo ameipongeza NMB kwa utekelezaji huo.

“Ninaipongeza NMB kwa kuja na suluhisho hili, naamini asilimia kubwa ya Watanzania watanufaika sana na huduma hii katika kipindi hiki ambacho dunia inapambana na changamoto ya ajira kwa vijana. Hii ni fursa ya vijana kujipatia mitaji,” alieleza.

Alisema huduma hiyo ya mikopo ya kidijiti inakwenda kumaliza kabisa tatizo la ugumu wa kupata mikopo.

“Hii ni hatua kubwa sana kwenye sekta ya kibenki Tanzania. Tukio hili linapeleka ujumbe kwa Watanzania wa kuwataka wasihangaike kupata mikopo ya kuanzisha biashara zao kwa kuwa fedha ipo NMB,” alisema.

Pia, alisema serikali kwa upande wake inaendelea kuimarisha usalama wa mtandao kwa kuwajengea uwezo wataalamu wa Tehama pamoja na kujenga mazingira wezeshi ya kisera, sheria, mifumo, miundombinu na kuhakikisha uwepo wa wataalamu hao kwenye nyanja zote muhimu za ubobezi.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande alisema uzinduzi wa Teleza Kidijiti ni ishara NMB imejipanga kupanua wigo wa huduma kote nchini.

Alisema maboresho yaliyofanyika katika sekta ya fedha yameleta matokeo chanya ikiwamo mikopo kwa sekta binafsi kuimarika na kuongezeka kutoka Sh trilioni 20.31 mwaka 2020 hadi kufikia Sh trilioni 22.34 mwaka jana sawa na ukuaji wa asilimia 10 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.1 mwaka 2020.

Aidha, mwaka jana, amana za benki za biashara ziliendelea kuongezeka hadi kufikia Sh trilioni 26.81 ikilinganishwa na Sh trilioni 23.81 mwaka 2020, sawa na ukuaji wa asilimia 13.0. Kati ya amana hizo, sekta binafsi ilifikia Sh trilioni 26.39 sawa na asilimia 98.4 ya amana zote.

Akizungumza katika uzinduzi huo ambao ni wa kwanza kufanywa na sekta ya benki nchini, Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna alisema huduma hizo zitaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya kibenki nchini.

Aliitaja huduma ya kwanza ni ya mikopo kwa njia ya kidijiti walioipa jina la MshikoFasta.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, huduma hii ya mikopo kidijiti itamwezesha mteja wa Benki ya NMB kujipatia mkopo kwa uharaka na kwa urahisi kabisa kupitia simu yake ya mkononi bila kufika kwenye tawi lolote la Benki ya NMB na bila kuweka dhamana,” alisema Zaipuna.

“Huduma hii itapatikana kupitia NMB mkononi kwa simu za aina zote, simu janja (kwa App) ama kwa kutumia simu za kawaida (kwa kutumia USSD). Mteja wa Benki ya NMB, kwa kutumia huduma hii ataweza kukopa mpaka shilingi 500,000 ndani ya muda mfupi kupitia simu yake ya mkononi,” alieleza.  

Aliitaja huduma ya pili ni NMB Pesa Wakala, ambayo ni wakala atakayetumia simu yake ya mkononi kuwa wakala kuwezesha wateja wake kuweka na kutoa fedha kupitia simu zao za mkononi kama walivyo mawakala wa huduma za fedha kupitia mitandao ya simu.

Alitaja huduma ya tatu kuwa ni huduma ya Lipa Mkononi ambayo ni huduma ya malipo kwa njia ya QR code au Lipa namba.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, Dk Edwin Mhede alisema lengo la NMB ni kuboresha na kurahisisha huduma zao na kuzifanya kuwa za kidijiti zaidi, wakienda sambamba na maendeleo ya kiteknolojia duniani na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa NMB (2020-2025).

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/4f456a8c6563c7a037bdcf01a28a18d6.jpg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi